Rais Dkt.Samia ashiriki mkutano wa kujadili hali ya usalama DRC

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amehudhuria Mkutano wa kujadili hali ya Usalama wa Mashariki mwa nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Organ Troika, SADC Troika na Nchi zinazochangia Vikosi vya Jeshi katika Force Intervention Brigade (FIB) Windhoek nchini Namibia tarehe 08 Mei, 2023. Mkutano huo utajadili hali ya Usalama Mashariki mwa nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). (Picha na Ikulu).

Mkutano huo wa dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Troika na Nchi zinazochangia Vikosi vya Jeshi vya Force Intervention Brigade (FIB) umefanyika leo mjini Windhoek nchini Namibia.

Aidha, mkutano huo umetoa tena wito kwa vikundi vyenye silaha kusitisha uhasama na kujiondoa bila masharti katika maeneo wanayoyashikilia nchini humo.

Mkutano huo pia umewasihi wanachama wa SADC kuunga mkono Serikali ya DRC na kushughulikia hali ya usalama ya Mashariki mwa nchi hiyo kabla ya Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Desemba 2023.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa amesimama pamoja na Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wakati Wimbo wa Taifa wa Namibia pamoja na ule wa SADC ukiimbwa kabla ya kuanza kwa Mkutano wa Dharura wa Wakuu hao wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Organ Troika, SADC Troika na Nchi zinazochangia Vikosi vya Jeshi katika Force Intervention Brigade (FIB) Windhoek nchini Namibia tarehe 08 Mei, 2023.

Vile vile mkutano huo umesisitiza uungwaji mkono wa DRC katika mapambano dhidi ya makundi ya kijeshi Mashariki mwa nchi hiyo ili kuleta amani endelevu, usalama na ustawi kwa wananchi wa Kongo na Jumuiya ya SADC kwa ujumla.

Kwa upande mwingine, mkutano huo umeidhinisha kupeleka Kikosi cha Jeshi la SADC kutoka katika Kikosi cha Kudumu cha Jumuiya hiyo ili kuiunga mkono DRC iweze kurejesha amani na usalama. Mkutano huo pia umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Rais wa Namibia Mhe. Dkt. Hage Geingo; Rais wa Afrika Kusini Mhe. Cyril Ramaphosa; Rais wa DRC Mhe. Félix Antoine Tshisekedi; Waziri wa Mahusiano ya Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Angola Mhe. Balozi Téte António; Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Malawi Mhe. Harry Mkandawire; pamoja na Balozi wa Zambia nchini Namibia Mhe. Stephen Katuka

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news