Rais Dkt.Samia atoa maagizo kwa waajiri nchini

NA MWANDISHI WETU

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameagiza waajiri kuwasilisha michango ya wafanyakazi kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii mara moja ili wapate stahiki na haki zao.
Akihutubia kwenye maadhimisho ya sherehe za Mei Mosi Kitaifa 2023 Mjini Morogoro, Rais Samia amemuagiza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kushughulikia suala la waajiri wa kutopeleka michango katika mifuko ya jamii na michango ya bima za afya ya wafanyakazi wao.

“Waziri Mkuu amesema akitoka hapa anaenda kuitisha mkutano wa waajiri lazima walie michango ya wafanyakazi hasa wale ambao serikali imewapa wao hawawasilishi …Malimbikizo yote ya bima ya afya yalipwe ndani ya siku 60 kama kuna mtu analimbikiza alipe ndani ya siku 60 ziwe zimelipwa waajiriwa waweze kupata haki zao,”amesisitiza Rais Samia.

Aidha, Rais Samia amerudisha nyongeza za mshahara za kila mwaka ambazo zilikuwa zimesitishwa kwa muda mrefu.

“Lakini niseme pia kuna nyongeza za mishahara ambazo muda mrefu zilisitishwa, nimeona mwaka huu tuzirudishe. Kwa hiyo wafanyakazi wote mwaka huu nyongeza za kila mwaka zitakuwepo na itakuwa hivyo kila mwaka, nashukuru TUCTA mwaka huu wamenielewa hawakuja na mdomo mkali unaotoa moto mara hii wamekuwa wapole, kutokana na yaliyofanyika,”amesema.

Kadhalika, Rais Samia amesema serikali kwa mwaka 2022/23 imeendelea kuimarisha Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA) kwa kuongeza wafanyakazi 18 na kununua magari 13 huku Idara ya Kazi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu yamenunuliwa magari 17 na mchakato wa kuongeza wafanyakazi unaendelea ili taasisi hizo zifanye kazi kwa ufanisi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news