Rais Dkt.Samia awatakia kidato cha sita kila la heri

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan amewatakia wanafunzi wote wa kidato cha sita ambao wanaanza mitihani yao leo kila la heri.

Mheshimiwa Rais Dkt.Samia ameyabainisha hayo kupitia kurasa zake rasmi za mitandao ya kijamii huku akiwasisitiza kuwa, Taifa linawategemea.

"Nawatakia kila la kheri wanangu wote mnaoanza mitihani yenu ya Kidato cha Sita kesho. Tunawategemea. Tunawaamini.

"Naamini mmejiandaa vyema kwa hatua hii muhimu kwenye safari yenu ya elimu, na nawaombea kwa Mwenyezi Mungu awape utulivu na siha njema mkahitimishe salama na kwa mafanikio.

"Serikali itaendelea kuhakikisha inaandaa mazingira bora katika safari yenu kuelekea hatua zifuatazo ikiwemo Vyuo vya Ufundi, Vyuo vya Kati na Vyuo vya Elimu ya Juu,"amefafanua Mheshimiwa Rias Dkt.Samia.

Awali, Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) lilibainisha kuwa, jumla ya watahiniwa 106,956 wamesajiliwa kuanza kufanya mitihani yao ya kumaliza kidato cha sita inayoanza leo.

Watahiniwa wa kidato cha sita 96,914 watafanya mitihani katika shule za sekondari 883 na watahiniwa 10,424 wa kujitegemea watafanya mitihani yao katika vituo 257.

Pia watahiniwa 8,906 kutoka vyuo 95 wamesajiliwa kufanya mitihani ya mwisho ya kozi ya ualimu katika ngazi ya stashahada na cheti kuanzia leo Mei 2, 2023.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), Dkt. Said Ally Mohamed aliyabainisha hayo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari.

"Kati ya watahiniwa wa shule waliosajiliwa, wanaume ni 53,324 sawa na asilimia 55 na wanawake ni 43,590 sawa na 45 huku watahiniwa wenye mahitaji maalumu wakiwa ni 181 ambapo kati yao 114 ni wenye uoni hafifu, 14 ni wasioona, 28 wenye ulemavu wa viungo vya mwili na mmoja ni mwenye mtandio wa akili,"alisema Dkt.Mohamed.

Alisema, kati ya watahiniwa wa kujitegemea waliosajiliwa 10,041 wanaume ni 6,248 sawa na asilimia 62 na wanawake ni 3,793 sawa na asilimia 38 huku watahiniwa mwenye uoni hafifu akiwa ni mmoja.

Wakati huo huo, kati ya walimu watakaoketi kufanya mtihani huo 2,344 ni ngazi ya stashahada na 6562 ni ngazi cheti. Ambapo kwa ngazi ya stashahada wanaume ni 1438 sawa na asilimia 61 na wanawake 906 sawa na asilimia 39.

"Watahiniwa 6,562 wa ngazi ya cheti, watahiniwa 2885 sawa na asilimia 44 ni wanaume na wanawake 3677 sawa na asilimia 56 huku wasioona wakiwa ni watatu kwa ngazi ya stashahada na wanne kwa ngazi ya cheti na mtahiniwa asiyeona kabisa akiwa ni mmoja,"alifafanua Katibu Mtendaji wa NECTA.

Mbali na hayo, Dkt.Mohamed alisema, baraza hilo halitasita kukifuta kituo chochote cha mitihani endapo litajiridhisha kuwa kuna ukiukwaji wa taratibu za mitihani ambazo zinahatarisha usalama wa mitihani ya Taifa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news