SIMULIZI YA KUTISHA KATIKA MAISHA-20

NA WILLIAM BOMBOM

Ilipoishia...utaratibu huu uliendelea mpaka nyama za mapadri hao zilipotamatika, walikufa kwa kifo kibaya kilichokuwa na maumivu yasiyo na maelezo. Huu ukawa mwisho wa Padri huyo na wenzake watatu.

Endelea

Ilikuwa ni Jumatatu tulivu, shule ya msingi Ilongo ilikuwa imetembelewa na ugeni mkubwa. Walimu walikuwa na furaha kubwa kutembelewa na ugeni huo. Wanafunzi walikuwa wametulia madarasani wakijisomea, shule hiyo haikuwa na uongozi wa serikali ya wanafunzi.

Kila mwanafunzi alitii sheria za shule hiyo kwa kupenda, walimu walifurahia sana namna wanafunzi wao walivyokuwa wakifanya kazi kwa moyo wote.

Yote hayo yalitokana na mtoto THE BOMBOM alimwaga dawa eneo hilo lililowafanya watoto kupendana na kufanya kazi kama misukule.

Ugeni uliokuja shuleni hapo ulikuwa wa waziri wa elimu, Mheshimiwa Ndulu Ihenge Lyaza. Mheshimiwa huyu alikuwa ni mbunge wa jimbo la Itilima, baada ya kuingia bungeni aliukwaa uwaziri wa elimu kulingana na elimu yake.

Hakuwa tabula lasa mbongo zake zilikuwa safi, huyu ndiye aliyebadili utaratibu wa walimu kutoka saa kumi jioni. Alileta waraka wa walimu kufundisha hadi saa nane, ili kukamilisha vipindi vinane kisha waendelee na shughuli zao.

Waziri huyu ndiye aliyemshauri mkuu wa nchi juu ya kuwaongezea walimu posho kila inapofika katikati ya mwezi na likafanikiwa. Walimu nchi nzima walimpenda, alikuwa kiongozi hakuwa mtawala kama walivyo mawaziri wengine.

Waziri huyo alikuwa amesikia habari za mtoto THE BOMBOM, kwa kuwa yeye ndiye mwenye dhamana na kada hiyo aliamua kuja kumuona mtoto huyo.

Alianzia mkoani yaani Mwanza kisha akaambatana na watu wengine, Mkuu wa Wilaya, mkurugenzi, kamanda wa polisi wilaya, wakuu wa vitengo na viongozi wengine wazito walikuwepo.

Wazee wa heshima katika wilaya ya Magu kama Pambano Magwanji Ng'wendagwantemi alikuwepo. Baada ya waziri kuzungumza na walimu alipata muda wa kuzungumza na mtoto THE BOMBOM. Mtoto huyo aliwashangaza watu wengi kwa namna alivyokuwa akifafanua kwa kina vitu vizito.

Mazungumzo yalipotamatika ukafika muda wa waziri kuzungumza na wanafunzi wa shule nzima. Mazungumzo hayo yalifanyika kwenye eneo la wazi nje huku kila mmoja akiwa na furaha. Wakati mazungumzo hayo yakiendelea, eneo hilo lilizungukwa na kunguru makumi kwa makumi elfu.

Kunguru hao walikuwa watulivu huku macho yao yakiwa yametazama eneo la kikao cha waziri na wanafunzi ilikuwa ni maajabu kwa waziri huyo.

Kikao chao kilipokamilika waziri alipanda gari na kuondoka, wakati gari la waziri linaondoka kwa bahati mbaya lilihama njia kidogo na kugonga mwanafunzi mmoja.

Miguu yake yote ilivunjika, waziri akamtaka dreva kusimamisha gari ili waone namna ya kumsaidia mtoto huyo. Aliyegongwa alikuwa mwanafunzi wa darasa la tatu, jina lake ni Makubi michembe Shitolyo.

Ilileta simanzi kwa kila mmoja aliyekuwa maeneo hayao, viongozi walichukua maamzi ya haraka ya kumpeleka hospitali ili kunusuru maisha ya mwanafunzi huyo.

Mtoto THE BOMBOM aliwazuia na kuwaomba wamwachie muda amsaidie majeruhi huyo, hali haikuwa nzuri hata kidogo miguu ilikuwa imevunjika nyakanyaka.

Mtoto THE BOMBOM aliishika miguu ya mwanafunzi huyo, baada ya hapo alifumba macho kisha akawa anazungumza maneno fulani.

Ghafla ile miguu iliacha kuvuja damu, baada ya hapo alitema mate chini kisha akayachanganya na udongo. Alichukua mchanganyo huo kisha akaupaka kwenye miguu ya mtoto aliyepata ajari.

Punde si punde miguu ya mtoto huyo ilijiunga, mtoto huyo alisimama na kutimua mbiyo kuelekea kwao. Lilikuwa ni tukio la ajabu sana katika jamii hiyo, waziri na viongozi wengine walimfuata mtoto THE BOMBOM.

Walimkumbatia kwa furaha kwa miujiza aliyokuwa akiifanya, mtoto huyo aliwasisitiza kutoyatangaza mambo aliyokuwa akiyafanya. Wengi walisadiki kuwa mtoto huyo alikuwa ni nabii wa Mungu aliyetumwa kuja kuokoa kizazi hiki.

Hapa niseme kidogo, ndugu msomaji kilichofanyika katika ajali hiyo hakua binadamu. Aliyegongwa alikuwa mbwa aliyekuwa amewekewa sura ya yule mwanafunzi, kwa muda huo yule mwanafunzi alikuwa kafichwa kimazingara.

Watu wote waliamini kuwa aliyepata ajari alikuwa ni yule mwanafunzi wakati kiuhalisia alikuwa ni mbwa, wakati mtoto THE BOMBOM alipokuwa amefumba macho alikuwa akifanya mawasiliano na wachawi wengine. Wachawi hao ndiyo waliombadili yule mbwa na kumrudisha yule mtoto.

Hii ni taaluma ya watu wenye akili, ni vigumu kwa mtu wa kawaida kuelewa ninachozungumza. Mambo ya namna hii huwa yakifanyika kila uchwapo, lakini kwa mtu asiye na macho ya ziada ni vigumu kulibaini.

Japo mtoto huyo aliwazuia watu kutangaza juu ya miujiza aliyokuwa akiifanya, habari hizo zilisambaa mithili ya moto wa gesi.

Kila sehemu wimbo ulikuwa ni nabii mtoto THE BOMBOM, ilitia faraja kwa kiwango kikubwa kwa Waafrika kuanza kumuamini mtoto huyo. Hakuna aliyekuwa akijua juu ya nguvu za ziada zilizokuwa zikitumiwa na mtoto huyo kufanya miujiza.

Idadi ya watu kumpenda iliongezeka, wengi wakawa wakimsaka ili angalau wapate baraka zake. Siku moja usiku wa manane THE BOMBOM na wachawi wenzake walivamia kwenye nyumba ya Shekh wa kata ya Ilongo.

Siku hiyo pia walikuwa wamepanga kumtembelea mchungaji wa kanisa la Shika Maneno Tenda Maneno. Walianzia kwa Shekh huyo, walimkuta akiwa amelala usingizi wa pono.

Walimchukua na kumficha kwenye pembe ya nyumba chumbani humo. Pale kitandani waliweka mbadala wake, waliweka mgomba ambao ulichukua kabisa picha ya Shekhe huyo na umbo lake.

Baada ya hapo walimpaka Shekhe dawa za kutokuwa na kumbukumbu ya jambo lolote. Walihakikisha kumbukumbu zake zinaishia kipindi aliposinzia.

Walipokamilisha kazi hiyo walimwaga madawa chumbani humo ya kuendelea kumlinda Shekhe huyo. Baada ya hapo waliondoka na kuelekea kwa Mchungaji wa Shika Maneno Tenda Maneno.

Hapa nizungumze kidogo, ndugu msomaji kati ya watu ambao huwa wanafayiwa majaribia ya mara kwa mara ni pamoja na wale hujiita watumishi wa Mungu.

Ndiyo maana mtoto THE BOMBOM na kundi lake waliamua kuanzia kwao, labda mtu huyo asiwe na doa la aina yeyote kipindi analala. Endapo atakuwa amefanya kosa la namna yeyote, huwa hawana nguvu za ulinzi hivyo wachawi kufanya wapendavyo.

Walimkuta Mchungaji huyo amelala pia, naye walifanya kama walivyomfanyia yule Shekhe kisha wakaondoka. Kesho yake matangazo kuhusu vifo vyao yalitolewa, eneo hilo liligubikwa na simanzi.

Jamii waliwapenda sana Shekhe huyo pamoja na Mchungaji, taarifa za misiba yao ilizagaa haraka mtaani mithili ya moto wa petrol.

Kulingana na taratibu za dini ya kiislamu Shekhe huyo alipaswa kuzikwa saa kumi jioni yaani Laasiri ya siku hiyo, ndugu na jamaa kutoka pande zote walikuwa wameshafika.

Ilipofika majira ya saa tano mtoto THE BOMBOM alifika msibani hapo, aliambatana na watu wengi waliokuwa wakimuamini kuwa ni nabii wao.

Pale msibani kila mmoja alifurahia uwepo wa mtoto THE BOMBOM, wengine walikuwa wakimsikia hawakuwahi kumuona. Siku hiyo ilikuwa ni bahati kwao, kwa umri wa mtoto huyo na mambo aliyokuwa akiyafanya hakukuwa na uhusiano.

Baada ya kufika msibani hapo mtoto huyo aliwasalimia na kuwapa pole. Aliwaita ndugu wa marehemu kisha akawauliza chanzo cha msiba wa ndugu yao.

Ndugu hao walieleza kila kitu juu ya msiba wa Shekhe, baada ya maelezo yao mtoto huyo aliwauliza kama walisadiki juu unabii aliokuwa nao.

Ndugu wa marehemu walikubali juu ya kusadiki kwa nabii mtoto THE BOMBOM. Aliwaomba kumpeleka kwenye chumba alichokuwa amehifadhiwa marehemu, walimpeleka hadi chumbani humo pasi na shaka.

Walipofika chumbani humo mtoto THE BOMBOM alinyanyua mikono juu akaomba kimoyo moyo. Ghafla yule marehemu alipiga chafya, ndugu na jamaa wakakimbia kutoka nje ya chumba hicho.

Mtoto THE BOMBOM aliendelea kuomba pasi na kuchoka, hatimaye yule marehemu alisimama na kuondoa shuka alilokuwa amefungwa. Kule nje kulileta taharuki kwa waombolezaji wote, wengi wao hawakuwahi kushuhudia miujiza hiyo.

Wakiwa bado wanashangaa shangaa, mlango ulifunguliwa kisha mtoto THE BOMBOM alitokeza nje ya nyumba akiwa ameambatana na yule Shekhe akiwa mzima wa buheri.

Aliwakabidhi mtu wao kisha akawasisitiza umati huo kutotangaza miujiza yake. Aliondoka eneo hilo na kuelekea kwenye msiba wa mchungaji, watu walimfuata kwa nyuma mtoto huyo huku wakiwa na imani kubwa juu yake. Pale msibani lilibaki gumzo juu ya tukio hilo, waislamu walisilimu na kufuata dini ya mtoto huyo.

Wapagani waliamua kuwa wafuasi wa mtoto huyo, wakirsto ndiyo usiseme waliamua kuwa wafuasi watiifu kwa mtoto THE BOMBOM.

Ndugu msomaji mambo yameanza kuchanganya, je mtoto THE BOMBOM atafanikiwa kumfufua Mchungaji wa Shika Maneno Tenda Maneno? Ungana nami sehemu inayofuata katika simulizi hii ya KANISA LA KICHAWI.

BUJIKO NG'WAKA.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news