SIMULIZI YA KUTISHA KATIKA MAISHA-25

NA WILLIAM BOMBOM

Mawingu yaliyopita karibu na kijimlima hicho yaliongeza uzuri wa eneo, yalilipamba eneo hilo na kuonekana kama Paradiso.

Endelea

Kwa kifupi eneo la mji wa Kanyama lilikuwa zuri lenye kuvutia kwa mtu yeyote apitapo. Kesho yake asubuhi viongozi wa wilaya walifika, viongozi hao walikuwa ni mkuu wa wilaya ya magu, bwana wambali roho yawivu, mkurugenzi wa halmashauri, afisa ardhi wa wilaya na watumishi wote wa ardhi.

Kulikuwa na viongozi wengine waliokuwa wameambatana kwenye msafara huo, kama vile wakuu wa idara zote, kamanda wa polisi wa wilaya, askari polisi wa kituo cha kisesa, na viongozi wengine chungu nzima.

Viongozi hawa walikuwa wamevutiwa na habari za mtoto THE BOMBOM. Walitaka kuutumia mwanya huo angalau kuwa karibu na mtoto huyo, walitamani wapata baraka angalau hata kwa kuguswa naye.

Yote hii ilitokana na miujiza mikubwa aliyokuwa akiifanya mtoto huyo, miujiza hiyo ilimfanya kuwa gumzo kila kona ya nchi.

Wazee na watu wa makamo walimzungumzia, vijana kwa watoto waliimba juu ya nabii huyo. Habari zilizotawala kwenye vijiwe vya kahawa na sokoni zilimuhusu nabii huyo, kwenye daladala na misibani pia walimzungumzia mtoto huyo.

Taratibu za makabidhiano yalifanyika mbele ya makutano, eneo lote la mlima pamoja na sehemu za chini zinazozunguka mlima huo zilikuwa ni mali ya taasisi hiyo ambayo kiongozi mkuu alikuwa ni mtoto huyo.

Jina lililosajiliwa katika hati lilikuwa ni SURVIVE FROM THE DEATH, katika hati hiyo kulikuwa na jumla ya ekari 350 zilizoambaa ambaa hadi kwenye mto. Umiliki wa eneo hilo ilikuwa ni miaka tisini na tisa.

Kwa vile serikali siku zote huwa makini na mambo yake, tayari wataalamu wake walikuwa wameshatoa ushauri ngazi za juu kuhusu ya faida itakayopatikana kupitia eneo hilo.

Serikali walikuwa wakijua namna nchi ya Saudi Arabia wanavyochuma fedha kupitia Hijja kwa waamini wa Kiislamu, vilevile walikuwa wakiona faida wanayovuna Taifa la Israel bila kutumia nguvu kupitia Hijja ya Wakristo kwenye kaburi la Yesu Kristo.

Serikali iliamini uwezo aliokuwa nao mtoto huyo, kwa namna moja au nyingine lazima atapata wafuasi toka pande zote za dunia.

Kitendo hicho kitapelekea kuwepo kwa watalii wengi ndani ya nchi, sekta ya utalii itaongeza fedha za kigeni ambazo ni faida kwa nchi.

Pia uwepo wa watalii ndani ya nchi ungepanua biashara kimataifa baina ya nchi na nchi zingine. Kwa hiyo hesabu za serikali kwa nabii mtoto huyo ilikuwa kubwa, ndiyo maana walilitoa eneo hilo bure wakijua faida itapatikana baadae.
Baada ya kukamilisha taratibu zote za kusainiana, walikabidhiana hati kama ilivyo ada kisha mtoto huyo aliwashukuru serikali kwa jambo hilo. Siku hiyo kulikuwa na neema kwa makutano, mtoto huyo alifanya miujiza mikubwa kwa watu waliokuwa na matatizo.

Wagonjwa kibao walipona siku hiyo, hili lilikuwa ni rahisi kwa mtoto huyo. Asilimia kubwa ya magonjwa yanayosumbua duniani chanzo chake ni nguvu za giza, kwa kuwa mtoto huyo alikuwa kabobea kwenye nguvu za giza ilikuwa rahisi kuwaponya wagonjwa hao.

Magonjwa ya upungufu wa nguvu za kiume yanayoendelea kuwasumbua wanaume wengi, chanzo chake ni nguvu za giza.

Kuna kisukari cha kutengeneza, magonjwa ya moyo yanayotokana na nguvu za giza pamoja na tatizo la figo. Kila alipowaponya watu waliamini ilikuwa ni nguvu za mungu, waliamini kuwa alikuwa ni nabii wa kweli aliyeletwa duniani kuponya watu wake.

Wapo waliofunguliwa baraka za biashara, ufugaji, kazi, kilimo na uongozi. Siku hiyo ilikuwa ya neema kubwa kwa makutano wote.

Baadaye mtoto huyo aliwaomba walinzi wake kutangulia mji wa Ilongo, kule angelikuja baada ya siku mbili maana alipaswa kwenda eneo fulani peke yake. Hivyo hakuhitaji kuwa na mtu mwingine zaidi yake, kwa namna hiyo safari yake ilikuwa ni kwenda kambini kwao.

Wale walinzi walikubali shingo upande na kuondoka mbele ya mtoto huyo, lakini hawakufanya hivyo walikwenda kujichanganya na makutano.

Kwa kuwa ilikuwa ni jioni walitaka kumfatilia kwa karibu mtoto huyo ili kujua alikokuwa akienda. Walitamani sana kuwepo kila eneo alilokuwa nabii mtoto huyo, tayari walikuwa wameshaonja utamu wa kukaa na nabii. Miujiza aliyokuwa akiifanya ilikuwa mikubwa zaidi, hivyo kila muda walitamani sana kuwa pamoja naye.

Ilipofika mida ya saa tatu za usiku nabii mtoto huyo aliwaaga makutano, miujiza aliyokuwa ameifanya siku hiyo ilienea mkoa mzima wa Mwanza.

Watu toka wilaya za Ukerewe, Sengerema, Kwimba, Nyamagana, Ilemela na Misungwi walifulika eneo hilo. Idadi hiyo ya watu ilizagaa eneo la chini ya mlima huo, wenyeji wa mji wa Kanyama waliuita Mlima Makamelwa.

Ndugu msomaji Makamilwa ni matunda madogo madogo ya asili yenye rangi ya njano. Matunda hayo ni matamu sana, yasemekana ni matunda ya kipekee yanayopatikana eneo hilo tu dunia nzima.

Katika mlima huo makamelwa yalikuwa ni mengi sana, ndiyo maana wanyama jamii ya nyani, ngedere na wanyama wa aina hiyo walipendelea sana maeneo hayo.

Wakati mtoto huyo akiwaaga makutano, wale walinzi wake walikuwa wamejichanganya kwenye kundi la watu. Alianza kuondoka kuelekea upande wa juu wa mlima huo, mlima ulipambwa vyema na nyasi fupi zilizostawi vyema eneo hilo.

Makutano waliamua kumfuata kwa nyuma nyuma mithili ya mkia wa mbuzi, ghafla upepo wa kisulisuli ulitokea eneo hilo.

Upepo huo uliwatenga makutano na mtoto huyo, katikati ya upepo huo walitokea wanaume wawili waliokuwa wamevaa nguo nyeusi.

Walikuwa ni Waafrika asili wenye nywele za kipilipili zilizovutia, walikuwa pia na nyuso za duara huku meno yao meupe mithili ya bunzi la mahindi.

Watu hao walikuwa na upanga wa moto mikononi mwao, panga hizo zilikuwa zikiwaka pasipo kuwaunguza mikononi mwao watu hao.

Walisimama imara mithili ya mlinzi wa kimasai lindoni, hakuna mtu aliyethubutu kumfuata kwa nyuma yule nabii mtoto.

Jambo la kushanga mtoto huyo wala hakujali, alipita eneo hilo bila wasiwasi huku watu hao wakionesha kumsujudia. Alipofika katikati ya mlima, alionekana ndege aina ya jijinono mweusi mfano wa kipanga aliyekuja toka mawinguni.
Ndege huyo alikuwa mkubwa mithili ya kwale, alipofika karibu ya mtoto huyo alitua chini na kubadilika. Alitoka kwenye umbo la ndege na kuwa bibi kizee,mambo hayo yalifanyika mbele za macho ya makutano.

Yule bibi alimsogelea mtoto huyo na kumshika kichwani, ghafla kichwa cha mtoto huyo kikaanza kuwaka moto mfano wa kujenga cha nyasi kiwakavyo.

Macho ya mtoto huyo yalibadilika na kuanza kutoa cheche za moto, yule bibi kizee alimsogelea zaidi mtoto huyo na kumshika mikono yake miwili.

Mara wakapotea mbele za upeo wa macho ya makutano, punde si punde wale watu waliokuwa na panga nao walipotea.

Hali ikawa shwari kabisa, makutano wakabaki wakimshukuru mungu kwa miujiza waliyokuwa wakitendewa na mtoto huyo.

Kila mmoja alikuwa na lake la kusema, wapo waliosema kuwa mtoto huyo kachukuliwa na malaika. Wengine walisema mtoto huyo alikuwa na nguvu kuu kuliko nguvu zote, hivyo alikuwa ni nabii wa kweli kutoka kwa mungu.

Ndugu msomaji endelea kufuatilia kisa hiki cha kusisimua sehemu inayofuata. Unadhani mtoto huyo amekwenda wapi? Kwa nini alifanya miujiza hiyo mbele za makutano, je, bibi aliyemchukua ni nani? Tukutane sehemu inayofuata.

LYANGOSHA

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news