WAGOMBANAO NDIO WAPATANAO

NA LWAGA MWAMBANDE

WALIOKUWA maadui Roy Keane na Patrick Vieira waliunganishwa tena Jumapili walipokuwa wakifanya kazi Sky Sports. Gwiji wa Arsenal, Vieira alimfanyia mzaha Keane, kabla ya nyota huyo wa Manchester United kuonesha kama anampiga ngumi Vieira.

Picha na SkySports.

Mkufunzi wa zamani wa Crystal, Palace Vieira alisema kushinda taji la Ligi Kuu ya England huko Old Trafford mnamo mwaka 2002 kulifanya liwe la kipekee zaidi mbele ya Keane.

Akikumbuka ushindani wao maarufu, Vieira alisema kwenye Sky: "Bila shaka inaweza kuwa vema sana, hasa unapoenda Old Trafford na kushinda huko. Hiyo ilifanya iwe maalum zaidi."

Wakati huo huo, Keane alimtazama Vieira na kutikisa kichwa huku akionekana kukosa la kusema. Kisha akamtania Vieira.

Keane aliendelea kusema miaka aliyotumia kupambana na Vieira uwanjani ilikuwa siku kuu ambazo bado anazikosa. Alisema: "Ilikuwa nzuri sana, umeikosa sana kwa sababu ilikuwa ya fujo, ilikuwa mbaya, kulikuwa na mchezo wa hali ya juu (na) ni wazi kulikuwa na kasi ya mchezo.

"Na ulijua kila wakati ulipocheza na Arsenal kutoka kwa mtazamo wa United kwamba matokeo yangekuwa muhimu sana ikiwa ungetaka kutwaa ubingwa, na kusema kweli zilikuwa siku nzuri."

Na baadaye kwenye matangazo Keane alitishia kuzua tena ushindani kwa kujifanya kumrushia ngumi Vieira anayecheka.

Pamoja na mikwaruzano yao uwanjani, Keane na Vieira walitibuana kabla ya mkutano wa Februari Mosi, 2005 kati ya Arsenal na United huko Highbury.

Vieira alituhumiwa kwa kujaribu kumtisha Gary Neville kabla ya pambano kati ya vilabu viwili vikubwa vya soka vya Uingereza. Keane alishuhudia vitisho hivyo, na akamuonya Vieira huku akimtaka lolote ambalo anataka kumfanyia Mungereza huyo ajaribu kumfanyia yeye.

Aidha, uhusiano wa wawili hao siku hizi ni tofauti zaidi. Mwaka jana Vieira alifichua kuwa wawili hao walikuwa wametoka pamoja kwa jili ya kupata ice cream tangu kutundika njumu zao. Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, mara nyingi wagombanao ndio wapatanao. Endelea;


1.Kwa kweli wagombanao, na ndio wapatanao,
Wanafyatuana hao, hawaelewani hao,
Vijembe ni vingi hao, hata kurogana hao,
Vieira na Roy Keane, liwe ni fundisho kwetu.

2.Wakati wa enzi yao, kama wachezaji hao,
Wakiwa kwa timu zao, walivurugana hao,
Ungedhani watu hao, wasingepatana hao,
Vieira na Roy Keane, liwe ni fundisho kwetu.

3.Hawa Manchester yao, hao na Arsenal yao,
Walivyopambana hao, kurusha maneno hao,
Singetegemea hao, iwe moja kazi yao,
Vieira na Roy Keane, liwe ni fundisho kwetu.

4.Kwa sisi wa zama zao, walichemshana hao,
Yale mapambano yao, kutetea timu zao,
Kiona hasira zao, sasa moja kazi yao!
Vieira na Roy Keane, liwe ni fundisho kwetu.

5.Wakaa pamoja hao, wachambuzi wetu hao,
Ya kale yale si yao, mpya ukurasa wao,
Kuna funzo huko kwako, kukosana kama wao,
Vieira na Roy Keane, liwe ni fundisho kwetu.

6.Mwakosana kama wao, bishaneni kama wao,
Lakini igeni kwao, wamefika mwisho wao,
Washirikiana hao, kutoa ujuzi wao,
Vieira na Roy Keane, liwe ni fundisho kwetu.

7.Yale mapambano yao, kutetea timu zao,
Siyo mioyoni mwao, ilikuwa kazi yao,
Sasa wapeana wao, twaona maneno yao,
Vieira na Roy Keane, liwe ni fundisho kwetu.

8.Enzi zenu siyo zao, ugomvi wenu si wao,
Ila wafanyayo hao, kwetu ni mema mazao,
Kukosana si mafao, yamalizika mazao,
Vieira na Roy Keane, liwe fundisho kwetu.

9.Hebu tuwaache wao, na hayo maisha yao,
Turudi kwenye makao, hata yetu mitandao,
Hasira kama za kwao, jioni tuseme wao,
Vieira na Roy Keane, liwe ni fundisho kwetu.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news