Tambeni tambeni Yanga, mnavuna jasho lenu

NA LWAGA MWAMBANDE

KLABU ya Yanga ya jijini Dar es Salaam ambayo kwa mara ya kwanza imefuzu Fainali ya kwanza ya Kombe la Shirikisho barani Afrika itaanzia nyumbani Mei 28, 2023 dhidi ya USM Alger kutoka nchini Algeria.

Ni mtanange ambao utapigwa katika Dimba la Benjamin Mkapa lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam kabla ya kwenda Algeria kwa mchezo wa marudiano Juni 3, mwaka huu katika dimba la Julai 5, 1962 jijini Algiers.

Wamefikia hatua hiyo, baada ya USM Alger kuitoa ASEC Mimosas ya Ivory Coast kwa sare ya 0-0 ugenini na ushindi wa 2-0 nyumbani, wakati Yanga SC iliitoa Marumo Gallants ya Afrika Kusini, ikishinda mabao 2-0 nyumbani na 2-1 ugenini huko Afrika Kusini.

Mbali na hayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan ameahidi kuwapa ndege Yanga kwenda kwenye mchezo wa marudiano wa Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya USM Alger nchini Algeria mapema mwezi ujao.

Dkt.Samia ametoa ahadi hiyo Mei 18, 2023 wajati akizungumza kwenye hafla ya miaka 10 ya Azam Media Limited, Tabata jijini Dar es Salaam.

Pamoja na hilo, Rais Samia ameahidi kutoa shilingi milioni 20 kwa kila bao ambalo Yanga watafunga kwenye michezo miwili ya Fainali ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.

“Sasa nitumie jukwaa hili kuipongeza timu yetu ya Yanga, wameingia na timu yetu ya Simba, wamecheza kwenye hayo mashindano vizuri. Na niliwapa msukumo kidogo, wamefanya vizuri, lakini kwa bahati moja imeishia katikati, Yanga imeendelea, nawapongeza sana.

“Sasa Yanga inakwenda kwenye fainali, si ndiyo? Sasa niseme yafuatayo, nilianza na mechi hizi kwa shilingi milioni 5 kwa kila goli la ushindi, waliposogea nikasema sasa milioni 10 kwa kila goli la ushindi, tunapokwenda kwenye fainali ni milioni 20 timu ikitoka na ushindi.

“Milioni 20 hii haitakwenda kafunga mbili kafungwa moja. Hapana, yawe magoli yote yameipa timu hiyo ushindi, kila goli milioni 20.

"Lakini zaidi ya hapo, Serikali itatoa ndege kuwapeleka katika mchezo wa fainali. Sasa ndege hiyo itabeba wachezaji, itabeba washabiki, na ninaomba sana, wale viongozi wa TFF na mchezo huu kuwapa moyo kama Serikali tunavyofanya,”amesisitiza Rais Dkt.Samia. Mshairi wa kisasa Lwaga Mwambande anasema, huu ni wakati wa Yanga kutamba. Endelea;

1.Anga limejaa Yanga, inasemwasemwa Yanga,
Hata mitaani Yanga, inayosikika Yanga,
Wanatembea waringa, mashabiki wote Yanga,
Tambeni tambeni Yanga, mnavuna jasho lenu.

2.Bendera zatamba Yanga, njano kijani za Yanga,
Tisheti za wanayanga, mitaani zajipanga,
Nyoyo zao wanakonga, fainali hiyo Yanga,
Tambeni tambeni Yanga, mnavuna jasho lenu.

3.Sikiza redio Yanga, inachambuliwa Yanga,
Pia na kwenye runinga, inatajwatajwa Yanga,
Fainali wametinga, kombe lanukia Yanga,
Tambeni tambeni Yanga, mnavuna jasho lenu.

4.Mitandao yote Yanga, picha zasambaa Yanga,
Wanachekacheka Yanga, tabasamu lote Yanga,
Hakuna wa kujivunga, ni sherehe yao Yanga,
Tambeni tambeni Yanga, mnavuna jasho lenu.

5.Furahini wana Yanga, muda wa mavuno Yanga,
Mikataba yenu Yanga, iweke vizuri Yanga,
Thamani ya timu Yanga, imepanda chati Yanga,
Tambeni tambeni Yanga, mnavuna jasho lenu.

6.Wachezaji wote Yanga, mmeiinua Yanga,
Jinsi mlivyojipanga, kuiheshimisha Yanga,
Fainali mmetinga, kama vile tingatinga,
Tambeni tambeni Yanga, mnavuna jasho lenu.

7.Viongozi wote Yanga, mmeshinda kama Yanga,
Hakuna wa kuwapinga, mmeipaisha Yanga,
Kwa kweli mmejipanga, wala hamkujivunga,
Tambeni tambeni Yanga, mnavuna jasho lenu.

8.Ni mwaka wa afya Yanga, tambeni tambeni Yanga,
Mwaka wa makombe Yanga, hebu yaongeze Yanga,
Wote wanokuja funga, mnyenyue kwapa Yanga,
Tambeni tambeni Yanga, mnavuna jasho lenu.

9.Ni ya Tanzania Yanga, mmetutangaza Yanga,
Hata tusopenda Yanga, mmetutangaza Yanga,
Kila iimbwapo Yanga, sote mwatubeba Yanga,
Tambeni tambeni Yanga, mnavuna jasho lenu.

10.Heri iwe kwenu Yanga, zidisheni kujipanga,
Msije mkaboronga, kilele mshindwe gonga,
Unaonekana mwanga, chezeni vizuri Yanga,
Tambeni tambeni Yanga, mnavuna jasho lenu.

11.Historia kubwa Yanga, metinga kibabe Yanga,
Waache wanaochonga, utani si wa kupinga,
Mko anga mpya Yanga, karata zidi zichanga,
Tambeni tambeni Yanga, mnavuna jasho lenu.

12.Mama Samia katinga, kutoa pongezi Yanga,
Fainali livyotinga, asanteni sana Yanga,
Jina mwazidi lijenga, la kutambulika Yanga,
Tambeni tambeni Yanga, mnavuna jasho lenu.

13.Fungu kubwa kwenu Yanga, goli mkifunga Yanga,
Na ndege ya umma Yanga, mtasafiria Yanga,
Hakuna anayepinga, mwaibeba nchi Yanga,
Tambeni tambeni Yanga, mnavuna jasho lenu.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news