TANZANIA, BORA KUISHANGILIA-11: Karibu Lindi, mambo ni mengi tena mazuri

NA LWAGA MWAMBANDE

HISTORIA inaonesha kuwa, mwaka 1961 wakati Tanganyika inapata Uhuru wake kutoka kwa Waingereza Mkoa wa Lindi haukuwapo kabisa katika ramani.

Kilichokuwapo wakati huo ni Jimbo la Kusini ambalo lilijumuisha mikoa ya sasa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma. Makao makuu ya jimbo hilo la Kusini yalikuwa katika Mji wa Lindi.

Hadhi ya Mji wa Lindi kuwa makao makuu iliishia mara baada ya Uhuru ambapo Jimbo la Kusini likawa linajulikana kama Mkoa wa Mtwara.

Makao makuu yakawa ni Mji wa Mtwara. Inaelezwa huenda, Mkoa wa Mtwara ulikuwa mkubwa sana kwa eneo hata mkuu wa mkoa wa kwanza wa Mtwara, John Nzunda alikuwa anasema:

“Natawala kipande cha nchi toka Pwani ya Bahari ya Hindi hadi Ziwa Nyasa na kutoka Mto Ruvuma hadi karibu na mto Rufiji.”

Serikali wa Awamu ya Kwanza iliyoongozwa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere iliugawa Mkoa wa Mtwara miaka ya mwanzo ya Uhuru ambapo kukawa na mikoa ya Mtwara na Ruvuma. Mgawanyiko huu uliifanya Lindi kuwa ndani ya Mtwara.

Julai 1, 1971 ndipo Mkoa wa Lindi ulianzishwa rasmi baada ya tena kuugawa Mkoa wa Mtwara. Makao makuu ya mkoa yakawa Mji wa Lindi.

Wakati Tanzania inaadhimisha miaka 10 ya Uhuru wa Bara kwa kuwaita Waingereza kuja kuiona hatua iliyopiga Mkoa ulikuwa na umri wa miezi sita tu.

Kieneo, Mkoa wa Lindi unapakana na Bahari ya Hindi upande wa Mashariki, Mkoa wa Pwani upande wa Kaskazini, Morogoro na Ruvuma upande wa Magharibi na upande wa Kusini ni Mkoa wa Mtwara.

Mkoa una eneo la kilometa za mraba 67,000 ambalo ni sawa na asilimia 7.1 ya eneo la Tanzania Bara. Hata hivyo, karibu asilimia 27 ya eneo la mkoa lipo chini ya Hifadhi ya Taifa ya Nyerere National Park Tanzania (Selous Game Reserve) ambayo iko Magharibi mwa Wilaya ya Liwale.

Kwa wastani hali ya hewa katika mkoa huu ni ya joto la kati ya nyuzi joto 24C hadi 27C na joto hili hutegemea sana pepo za bahari zinazovuma katika kipindi husika kwa mfano pepo za Kusi ni za baridi na Kaskazi huleta joto. 

Sehemu za miinuko zilizoko kati na Kaskazini kama Rondo, Kilimarondo, Kipatimu na Mpigamiti hali ya joto hupungua na kuonesha tofauti za nyakati za joto na baridi.

Mvua hunyesha mwezi Novemba mpaka Aprili na hali ya ukame kati ya Januari na Februari, Agosti hadi Oktoba. Wastani wa mvua kwa mwaka ni milimita 750-1,200.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema Lindi kuna mambo mengi ambayo yanahitaji muda mrefu kuyachambua na kuyaeleza, lakini kwa uchache. Endelea;


1. Lindi ndiko twapitia,
Mtwara tutafikia,
Tena ziko mbili njia,
Barabara baharini.

2. Watu huko nakwambia,
Kilimo wakijulia,
Hapo nawafagilia,
Kwa uwazi bila soni.

3. Korosho imezidia,
Watu wanapalilia,
Na gesi ilotujia,
Inatufaa nchini.

4. Huko ndiko waanzia,
Umeme wa Tanzania,
Ni mwingi nakuambia,
Watufaa viwandani.

5. Kilimo wanaanzia,
Baharini malizia,
Huko wanatupatia,
Kwetu nyingi protini.

6. Mkoa metupatia,
Kiongozi nakwambia,
Majaliwa twatambia,
Ni mtu mwenye uoni.

7. Yeye limsaidia,
Rais kusimamia,
Mengi aliyachangia,
Kwa Magufuli zamani.

8. Majaliwa nakwambia,
Mambo anafwatilia,
Kitu akitamkia,
Ameshajua undani.

9. Wale amewapitia,
Mazonge wajifanyia,
Hakika watakwambia,
Kabisa hana utani.

10. Mpole kimwangalia,
Msafi mwilini pia,
Ukizembea sikia,
Kwake uko msambweni.

11. Hacheki cheki sikia,
Mambo anapopitia,
Kooni awakalia,
Wale wasio makini.

12. Hata Rais Samia,
Bado anamwaminia,
Jahazi kushikilia,
La uongozi nchini.

13. Mema tunamtakia,
Azidi tutumikia,
Nchi yetu Tanzania,
Ing'are kama Japani.

14. Wale wanaopania,
Kilimo kujifanyia,
Lindi mtajipatia,
Ardhi mkitamani.

15. Wafugaji Tanzania,
Ndani mnaofugia,
Huko Lindi tarajia,
Malisho yalosheheni.

16. Wale wanaovamia,
Ili ng’ombe kulishia,
Msije kujaribia,
Huko Lindi si sokoni.

17. Ni bora kuzingatia,
Vile wanavyotwambia,
Kule ndani kufugia,
Mazao yende sokoni.

18. Lindi tumejipatia,
Gesi ni nyingi sikia,
Kwa kweli twajivunia,
Kwa matumizi nchini.

19. Hiyo gesi yachangia,
Viwanda kuzalishia,
Ajira vinachangia,
Na kodi serikalini.

20. Gesi imewavutia,
Wawekezaji sikia,
Dangote Mnijeria,
Lindi-Mtwara nyumbani.

21. Kiwanda chatupatia,
Saruji ya kutumia,
Ajira twajipatia,
Na bei za wastani.

22. Jinsi gesi asilia,
Ilivyo ya kuvutia,
Matumizi mengi pia,
Inatufaa nchini.

23. Ni njema kwa kupikia,
Miti tunajitunzia,
Kama watusambazia,
Ni bora sana jamani.

24. Hivi tunapigania,
Mazingira jitunzia,
Twaweza kuitumia,
Si kuni za msituni.

25. Pia gesi asilia,
Kule imetufikia,
Waweza kuitumia,
Kuendeshea injini.

26. Vile tunajichimbia,
Vile tumeijulia,
Bei nzuri nakwambia,
Ni bora sana garini.

27. Bei za kujipandia,
Petroli kutumia,
Siyo gesi asilia,
Kutoboa mifukoni.

28. Wito wenzetu sikia,
Hii gesi asilia,
Fanya kutusambazia,
Ifike kote nchini.

29. Kwa wingi kujipatia,
Uchumi tutachangia,
Pia kujipunguzia,
Bei kubwa duniani.

30. Petroli yatujia,
Malori tusambazia,
Pia gesi asilia,
Sambaza kote nchini.

31. Wale wanaitumia,
Kweli wanafurahia,
Bei waifurahia,
Kwa jinsi ni ahueni.

32. Selous twajivunia,
Watalii watujia,
Wengine wajiwindia,
Wanyama walo mwituni.

33. Tena tumejipatia,
Urani tajichimbia,
Dola tutajipatia,
Tuzitumie nyumbani.

34. Wale wanatuchimbia,
Mkwara twawasikia,
Kwao wanaitumia,
Watukataza kwanini?

35. Ila cha kuangalia,
Mazingira zingatia,
Tusijetukajichulia,
Tuingie hatarini.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602


Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news