TANZANIA, BORA KUISHANGILIA-12: Ni Manyara, Ni nani utamwambia,Asitake kusikia?

NA LWAGA MWAMBANDE

HISTORIA inaonesha kuwa, Mkoa wa Manyara ulianzishwa kwa tangazo la Serikali Na. 367 lililotolewa Julai 27, 2002 na kuchapishwa katika gazeti la Serikali la Agosti 2, 2002 baada ya kugawanywa kwa Mkoa wa Arusha ambao kabla na wakati wa kipindi cha Uhuru ulijulikana kama Jimbo la Kaskazini (Northern Province).

Aidha, Mkoa wa Arusha ulianza kutumia rasmi jina hilo mwaka 1963.Miongoni mwa wilaya zilizounda mkoa huo ni Mbulu na Maasailand ambazo sehemu kubwa iko katika Mkoa wa Manyara sasa.

Wilaya hizo ziligawanywa kama ifuatavyo,Wilaya ya Mbulu ilianzisha Wilaya ya Hanang' mwaka 1969 na Hanang' ikianzisha Babati mwaka 1985, wakati Wilaya ya Maasailand iligawanywa kwenye Wilaya ya Kiteto mwaka 1974 ambayo pia iligawanywa na kuanzisha Wilaya ya Simanjiro mwaka 1993.

Aidha, baada ya kugawanywa kwa Mkoa wa Arusha, Wilaya za Mbulu, Hanang’, Babati, Kiteto na Simanjiro ziliuunda Mkoa wa Manyara.

Mkoa wa Manyara ni kati ya mikoa mikoa 26 ya Tanzania na mikoa 31 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ukiwa unapakana na mikoa ya Singida na Shinyanga upande wa Magharibi, Mkoa wa Dodoma upande wa Kusini, Mkoa wa Tanga upande wa Mashariki na mikoa ya Arusha na Kilimanjaro upande wa Kaskazini.

Makao makuu ya mkoa wa Manyara yapo Babati Mjini. Manyara inapata wastani wa mvua kati ya mm 450 na mm1200 kwa mwaka.

Kuna misimu miwili ya mvua. Mvua za muda mfupi ambazo hunyesha kati ya Oktoba na Desemba katika baadhi ya maeneo ya wilaya za Kiteto, Hanang’, Babati na Mbulu.

Mvua za muda mrefu hunyesha kati ya mwezi Februari na Juni. Hali ya hewa ni nyuzi joto 130C wakati wa masika na nyuzi 330C wakati wa kiangazi kutegemeana na msimu na mwinuko wa ardhi. Mkoa upo katika mwinuko kati ya mita 1000-2000 juu ya usawa wa bahari.Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema, Manyara kuna jambo. Endelea;


1. Mkoa Manyara pia,
Upo hapa Tanzania,
Huo tunajivunia,
Watalii unawini.

2. Ni nani utamwambia,
Asitake kusikia,
Vile tunajivunia,
Ngorongoro hifadhini.

3. Mbuga tunajivunia,
Kuwa kwetu Tanzania,
Na pia tunatambia,
Kwa kuvutia wageni.

4. Ukifika nakwambia,
Kule bondeni sawia,
Kila tachoangalia,
Takuingia moyoni.

5. Simba na pundamilia,
Eneo wanachangia,
Chui wafugaji pia,
Wote hao wamo ndani.

6. Ila ndege nakwambia,
Tonge ukishikilia,
Waweza kukuibia,
Kwa hiyo uwe makini.

7. Wamasai twatambia,
Manyara, Arusha pia,
Uchumi wanachangia,
Kwa kulinda tamaduni.

8. Nguo zao asilia,
Na maisha asilia,
Hivyo kweli vyavutia,
Wenyeji hata wageni.

9. Sote tunatamania,
Hamasa kuwapatia,
Mila wasije achia,
Kufuata ya mjini.

10. Huko ninakuambia,
Lugha zetu zaishia,
Na mila twazisagia,
Makabila huyaoni.

11. Kiswahili twasifia,
Umoja kimechangia,
Lugha zetu zaishia,
Kikitamba duniani.

12. Kwa Wamasai sikia,
Na wengine nakwambia,
Mila kufuatilia,
Ibaki yao nishani.

13. Vitunguu twatumia,
Kwa vyakula kuungia,
Licha ya kwingine pia,
Manyara vingi shambani.

14. Ziwa Babati sikia,
Samaki twajivulia,
Vile ninalisifia,
Latoa maji nyumbani.

15. Magadi ninakwambia,
Manyara tajipatia,
Kama ukipafikia,
Mandhari taitamani.

16. Tanzanite sikia,
Fahari ya Tanzania,
Madini yanavutia,
Yako pale ardhini.

17. Utajiri twakalia,
Udhibiti nasifia,
Saniniu twatambia,
Kuvuna mabilioni.

18. Hapa sio tamatia,
Manyara kuisifia,
Nayo ilitupatia,
Waziri Mkuu nchini.

19. Kwa sasa ashikilia,
Rekodi ya kusalia,
Kitini kitumikia,
Muda wa madarakani.

20. Sumaye nakutajia,
Frederick sikia,
Ukuu alikalia,
Miaka kumi nchini.

21. Miaka alosalia,
Kwa Mkapa aminia,
Yale alitufanyia,
Rais alisaini.

22. Mkapa kimsifia,
Yale alitufanyia,
Ni vema kukumbukia,
Sumaye ndiye mpini.

23. Yale anaaminia,
Hayaachi kutitia,
Hayo ayasimamia,
Hadi yafike mwishoni.

24.Huyu ndiye lianzia,
Upinzani kuingia,
Mengi liwasaidia,
Sasa karudi nyumbani.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602


Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news