ZHC yasikia hitaji la makazi kwa wenye kipato cha chini Zanzibar

NA DIRAMAKINI

SHIRIKA la Nyumba Zanzibar (ZHC) limesema lina mpango wa kujenga nyumba za kuwapangisha watu wenye kipato cha chini katika maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba. 
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Mwanaisha Ali Said wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa shirika hilo Darajani, Unguja. 

Amesema, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imetenga ardhi ya akiba kwa ajili ya maendeleo hivyo shirika litatumia fursa hiyo kujenga nyumba za kupangisha na kuuza kwa wananchi mbalimbali kwa ajili ya kuleta makaazi bora. 

Mkurugenzi Mwanaisha amesema, ZHC kwa sasa imeanza kujenga nyumba za kuuza katika eneo la Mombasa kwa Mchina, lakini hata mwananchi mwenyewe kipato cha chini anaweza kununua kutokana na utaratibu mzuri ambao ZHC imepanga kuziuza nyumba hizo. 

Alieleza kwamba, nyumba hizo zitauzwa kwa Wazanzibari waliyopo ndani na nje ya nchi, muhimu mtu afuate taratibu za manunuzi zilizowekwa na shirika hilo. Nyumba zinazojengwa na Shirika la Nyumba Zanzibar (ZHC) eneo la Mombasa kwa Mchina Unguja.

Pia amesema, ZHC itauza nyumba hizo kwa njia tatu, aidha njia kulipa pesa zote kwa pamoja, au njia ya kulipa pesa kwa awamu nne au kwa njia ya benki.

"Mortgage House ni njia ambayo mtu anazungumza na benki, hivyo sisi shirika tunapokea pesa kutoka benki,lakini mteja yeye atafunga mkataba na benki kwa ajili ya kukatwa pesa za nyumba hiyo,"amesema Mwanaisha.

Aliezea kwamba, ZHC iko tayari kupokea pesa za nyumba zinazojengwa Mombasa kwa Mchina kwani ujenzi umeshaanza tangu Machi 2023 na utamalizika baada ya miezi 15 kuanzia mwezi huo. 

Amesema, nyumba hizo zitauzwa bei tofauti kutokana na idadi ya vyumba kwani kuna nyumba za vyumba viwili zitauzwa sh.milioni 136 na nyumba ya vyumba vitatu zitauzwa milioni 153, bei hizo bila vati (VAT). 

Aidha, Mkurugenzi Mwanaisha alizungumzia suala la mazingira ya usafi katika eneo la nyumba hizo, amesema dhamana ya usafi, ZHC itamkabidhi Bodi ya Kondominia ambayo ni taasisi moja wapo ya Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi ndio itakayobeba dhamana ya kuweka mazingira safi katika maeneo ya nyumba hizo. 

Mwisho Mkurugenzi Mwanaisha amemshukuru Rais wa Zanzibar, Dkt.Hussein Ali Mwinyi kwa kuwaunga mkono katika gharama za ujenzi wa nyumba hizo kwani bila ya kupata msaada kutoka Serikali Kuu,shirika lisingeweza. Ujenzi wa Nyumba za Mombasa kwa Mchina utagharimu shilingi Bilioni 9.8 ambapo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imetoa shilingi bilioni 6.8 na Shirika la Nyumba Zanzibar ( ZHC) limetoa shilingi bilioni tatu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news