Watumishi OUT wabisha hodi Dr.Edmund Rice Sinon Secondary School

NA DKT.MOHAMED OMARY MAGUO

CHUO Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) kimepata fursa ya kutembelea Shule ya Sekondari Dr. Edmund Rice Sinon iliyopo jijini Arusha leo tarehe 18/05/2023.

Tumepata mapokezi na ukarimu mzuri kutoka kwa uongozi wa shule hii ambapo mkuu wetu wa msafara Dkt.Nangware Msofe ambaye ni Mkurugenzi wa Kituo cha OUT cha Mkoa wa Arusha, Mwalimu. Rosemary Makiya na mimi tumefarijika sana kufika kwenye shule hii.

Tukiwa shuleni hapo tumepata nafasi ya kuzungumza na walimu peke yao na baadae wanafunzi wa kidato cha tano ambao hivi karibuni wanaingia kidato cha sita baada ya watangulizi wao kuhitimu mwezi huu wa Mei 2023. Masuala ya tuliyozungumza ni haya:

Mosi; Tumewaeleza walimu na wanafunzi hao historia na chimbuko la OUT, kwamba ni wazo la Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Nyerere ambalo lilitimia mwaka 1992 kwa sheria ya Bunge namba 17 ya mwaka huo na kuanza kutoa mafunzo mwaka 1994.

Pili: Tumewaeleza walimu na wanafunzi kwamba OUT ni Chuo Kikuu ambacho kinawafuata wanafunzi huko walipo na siyo wanafunzi kukifuata chuo.

Hii inajihidhirisha kupitia kuwepo kwa vituo vya OUT katika mikoa yote ya Tanzania Bara, vituo vya uratibu Unguja, Pemba, Kahama na Tunduru. Lengo ni kufika katika kila wilaya na baadae kwenye kata. Hii ndiyo azma ya waasisi wa taifa na dira ya OUT katika miaka michache ijayo.

Tatu: Tumezungumzia masuala ya mikopo ya Elimu ya Juu kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ya Tanzania na mikopo kutoka Benki ya NMB.

Hapa tumeeleza kwamba, mikopo inatolewa kwa wote wenye sifa na kukidhi vigezo kama vilivyoainishwa na Bodi ya Mikopo. Kwa ambao watakuwa tayari kukopa NMB wakitimiza masharti na vigezo watapewa mikopo kwa riba nafuu ya Asilimia 9. Maelekezo ya kina na huduma zinatolewa kwenye matawi yote ya NMB nchi nzima.

Nne: Wanafunzi wa Kidato cha Sita watarajiwa, wamepata maelezo ya kina kuhusiana na foundation program ya OUT kwa wale ambao watapata ufaulu wa Division Three ya alama 14 na kuendelea.

Tano: Tumewaeleza walimu na wanafunzi kwamba OUT inatoa elimu katika ngazi za Astashahada, Stashahada, Shahada za Kwanza, Shahada za Umahiri na Uzamivu katika fani za Sayansi, Teknolojia, Mazingira, Elimu, Biashara, Uongozi, Sanaa, Sayansi za jamii na Sheria. Fursa za kujiendeleza kupitia OUT ni pana na kila mwenye nia ya kujiendeleza anaweza kufanya hivyo akiwa mahali popote pale Tanzania au nje ya nchi.

Sita: Tumewaeleza walimu na wanafunzi kuhusu mifumo ya kisasa ya ufundishaji na ujifunzaji ya OUT.

Mifumo hiyo ni MOODLE Platform, mihadhara mbashara kwa ZOOM, What's App Kimbwette, Telegram Kimbwette, ZOOM Kimbwette, mihadhara katika YouTube, mafunzo ya ana kwa ana, mafunzo kwa vitendo na utaratibu wa mitihani.

Mwisho

Tunatoa shukurani za dhati kwa uongozi wa shule ya Sekondari Dr. Edmund Rice Sinon kwa mapokezi, ukaribisho na ukarimu waliotupatia tukiwa shuleni hapo. Hakika ilikuwa ni fursa nzuri kwetu na kwa walimu na wanafunzi kujifunza masuala mbalimbali yanayohusiana na OUT.

WENU

Dkt. Mohamed Omary Maguo
Mhadhiri Mwandamizi
Mkurugenzi wa Mawasiliano na Masoko
Chuo Kikuu Huria cha Tanzania
Arusha
18/05/2023

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news