Ziara ya Rais Dkt.Mwinyi nchini Qatar yazifikia fursa kabambe

NA MWANDISHI WETU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi akiwa katika siku ya mwisho ya ziara yake ya Qatar akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan, alikutana na Waziri anayeshughulikia masuala ya Nishati wa Qatar, Mhe.Mhandisi Saad bin Sherida Al Kaabi.
Katika mazungumzo hayo walijadili juu ya ushirikiano kati ya Zanzibar na Qatar kuhusiana na uchimbaji wa mafuta na gesi Zanzibar. Mkutano huo ulilenga namna ambavyo nchi hizo mbili zinaweza kufanya kazi pamoja katika eneo hilo.

Rais Dkt Mwinyi alimfahamisha Waziri huyo wa Qatar kuhusu Sera ya Zanzibar ya Uchumi wa Buluu na jinsi Qatar inawezakuwa msaada katika suala la uchimbaji wa rasilimali hiyo. 

Dkt.Mwinyi alimwambia Waziri wa Nishati wa Qatar kutuma wataalamu wake Zanzibar ili kufanya kazi kwa pamoja na wataalamu wa Zanzibar kuchunguza uwezekano wa kuanza haraka uchimbaji wa rasilimali hizo. 

Alisisitiza kuwa, ushirikiano wa pamoja na ujuzi wa kitaalam kutoka Qatar unaweza kuchochea maendeleo na utekelezaji wa uchimbaji huo kwa ufanisi na kwa kasi.

Waziri wa Nishati wa Qatar, Mhandisi Saad bin Sherida Al Kaabi, alimjibu Mhe.Dkt.Mwinyi akielezea kuwa nchi yake tayari ina uzoefu wa kufanya kazi na mataifa ya Afrika katika uchimbaji wa mafuta na gesi. 

Alikuwa wazi kuwa Qatar imekuwa ikisaidia nchi nyingi barani Afrika katika sekta hii na iko tayari kuendelea kufanya hivyo na Zanzibar.
Baadae, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi, alikutana na Waziri wa Uchukuzi wa Qatar, Mhe.Jassin bin Saif Ahmed. 

Katika mkutano huo, Dkt.Mwinyi alimuelezea Waziri wa Uchukuzi wa Qatar kuhusu mipango ya Zanzibar kuhusu mradi mkubwa wa ujenzi wa Bandari ya Mangapwani, ambayo itakuwa kituo kikuu cha kupakia na kupakua mizigo. Dk. Mwinyi alipendekeza kuwa Serikali ya Qatar inaweza kutoa msaada katika ujenzi wa bandari hiyo.

Waziri wa Uchukuzi wa Qatar, Mhe. Jassin bin Saif Ahmed, alionyesha shauku kubwa kuhusu mradi huo, hasa baada ya kupewa taarifa kuwa eneo la ujenzi wa Bandari ya Mangapwani lina kina cha mita 18, ambacho ni kina kinachofaa kwa meli kubwa za mizigo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news