Awoke International Sports Tourist Conference and Expo wapewa baraka Mara

NA FRESHA KINASA

SERIKALI mkoani Mara imesema inaunga mkono juhudi na kutoa baraka zote kwa Kampuni ya Utalii ya Awoke International Sports Tourist Conference and Expo iliyokusudia kuvitangaza vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo mkoani humo katika kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan kukuza sekta hiyo.

Lengo ni kuwavuta watalii wengi kutoka mataifa mbalimbali waje kutalii na kuwekeza katika nyanja mbalimbali ili kuchangia kuleta mageuzi chanya ya kiuchumi kwa wakazi wa mkoa huo na taifa kwa ujumla. 
Kauli hiyo imetolewa leo Juni 27, 2023 na Katibu Tawala Mkoa wa Mara, Robert Msalika Makungu wakati akifungua mkutano wa wadau wa utalii uliofanyika Mjini Musoma mkoani humo na kuwakutanisha wadau mbalimbali na viongozi wa Serikali. 

Amesema, Serikali ya mkoa ipo tayari kupokea wazo lolote, ushauri na kutoa ushirikiano kwa wadau wote wanaokuja na mikakati ya kuwaletea maendeleo wananchi. 
"Rais wetu Samia Suluhu Hassan amekuwa mstari wa mbele kuifungua nchi, niseme kwamba Serikali ya mkoa inaunga mkono juhudi na kutoa baraka zote kwa Buche Buche ambaye anataka kuvitangaza vivutio vya utalii katika Mkoa wetu. 

"Na pia wazo lake linakibali kutoka TAMISEMI na sisi Ofisi ya Mkuu wa Mkoa tumempa ushirikiano na kibali katika kusukuma mbele juhudi za kuleta maendeleo,"amesema Robert. 

Pia, amesema kuwa juhudi za Rais Dkt.Samia zinazofanywa ikiwemo kujenga mahusiano na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashiriki zinafaida kubwa katika kuimarisha mahusiano ya kiuchumi, kitalii na kibiashara hivyo kuna umuhimu mkubwa wa kutangaza fursa za Mkoa wa Mara ziweze kuwanufaisha wananchi kwa kuongeza wawekezaji wengi wa ndani na nje ya nchi. 

Kwa upande wake Mratibu wa kampuni hiyo, Buche Buche Enosy amesema, vivutio mbalimbali vya utalii vinavyopatikana Mkoa wa Mara vinatarajiwa kutangazwa kwa wageni zaidi ya 350 kutoka mataifa mbalimbali ili viweze kufahamika zaidi duniani mwezi Septemba, mwaka huu. 
Amesema, nia ni kuhakikisha Mkoa wa Mara ambao pia umebeba heshima ya kumtoa Mwasisi wa taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere unakuwa kitovu cha utalii duniani. 

Ameongeza kuwa, Ppogramu ya kuvitangaza vivutio vya utalii vya mkoa huo itafanyika mwezi Septemba, ambapo itahusisha maonesho ya biashara kuanzia Septemba 20, 2023 hadi Septemba 30, 2023 ambayo yatafanyika Mjini Musoma. 

Pia amesema, utafanyika Mkutano wa kimataifa utakaohudhuriwa na wageni 350 ambao utafanyika ndani ya mwezi huo na wageni kutoka mataifa ya Rwanda, Burundi, DRC Congo, Kenya, Uganda Burundi watashiriki kuangazia fursa na mchango wa utalii katika kuleta maendeleo ya wananchi. 
Aidha, wageni hao amesema wataambatana na waandishi wa habari 24 wa kimataifa kutoka mataifa mbalimbali ambao pia watashiriki kutembelea vivutio vya utalii vya Mkoa wa Mara kwa siku mbili ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Serengeti. 

Amevitaja baadhi ya vivutio vya Utalii vinavyopatikana mkoani Mara kuwa ni pamoja na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Maporomoko ya Nyamihare, Maporomoko ya Mogabiri, mtazamo wa bonde la ufa, maji ya moto Ngoreme, Kijiji cha Robanda, Fort Ikoma.

Vivutio vingine ni mawe ya Makongoro, mawe ya Chitafubha, bustani ya Malkia Elizabeth iliyopo Manispaa ya Musoma, Uvuvi wa samaki, Utalii wa madini na makumbusho ya Mwalimu Nyerere Butiama ambavyo amesema vina manufaa makubwa vikitangazwa kwa uhakika. 
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Mkoa wa Mara, Joseph Nyiraha amesema kuwa, ajenda ya kutangaza vivutio vya Mkoa wa Mara inapaswa iungwe mkono na Serikali na mazingira wezeshi yawekwe ili kuleta tija katika maendeleo. 

Martine Korogo ambaye ni mdau wa utalii mkoani humo ameuomba uongozi wa Mkoa wa Mara kuhakikisha unasimama pamoja na wadau wote na kuwapa ushirikiano kufanikisha malengo yao kwa kuweka mazingira wezeshi na kusimamia utekelezaji wa mipango yao kwa manufaa ya wananchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news