DC Dkt.Haule atoa maagizo muhimu Musoma

NA FRESHA KINASA

MKUU wa Wilaya ya Musoma, Dkt. Halfan Haule amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Musoma mkoani Mara, Bosco Ndunguru kufanya usimamizi madhubuti katika Kituo cha Afya cha Nyasho kilichopo katika manispaa hiyo, kwani kuna malalamiko mengi kutoka kwa wananchi.
Amesema,malalamiko hayo ni kuhusu ubovu wa huduma wanapofika kituoni hapo kutibiwa na pia kutozwa gharama za vipimo ambazo haziendani na uhalisia.

Pia, Dkt.Haule amemtaka kuboresha mazingira ya Kituo cha Afya cha Bweri ambacho pia amesema mazingira ya kituo hicho ni machafu na majengo yake yamechakaa hayaendani na kuonesha heshima ya serikali na kama kuna mpango wa kuboresha majengo ya kituo hicho juhudi za haraka zifanyike. 

Dkt.Haule ametoa maagizo hayo Juni 7, 2023 wakati akitoa salamu za serikali katika kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Musoma.

"Mkurugenzi mkifuatilie kwa ukaribu Kituo cha Afya cha Nyasho kuna malalamiko mengi sana kutoka kwa wananchi. Wagonjwa wanaolazwa mfano kama mgonjwa kaandikiwa dawa saa nne watoa huduma hawapiti kwa wakati kutoa huduma jambo hilo halipendezi kabisa.

"Pia bili wanazo chaji kwa wagonjwa wanaofika kutibiwa haziendani na uhalisia mfano Ultra Sound ni elfu 15,000. Wanatoza elfu 25,000 hadi 30,000. Na pia hakuna bango linaloonesha gharama za huduma hii si sahihi, Mkurugenzi naomba kituo hiki kisimamiwe vizuri kukidhi haja na huduma bora ambazo wananchi wanapaswa kuzipata.

"Pia Kituo cha Afya cha Bweri mazingira yake ni machafu na majengo yamechakaa hayaoneshi heshima na hadhi ya kituo cha serikali na kama kuna mpango wa kufanya ukarabati mipango hiyo ifanyike mapema vituo hivi visimamieni vyema," amesema Dkt. Haule.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Musoma, Bosco Ndunguru amesema kwamba amepokea maelekezo hayo na atafanya ufuatiliaji kuhakikisha huduma zinatolewa kwa kufuata sheria taratibu na kanuni. 

"Kwa bahati nzuri tulikaa na Mheshimiwa Mbunge wa Musoma Mjini, Meya, Mkurugenzi na Waganga wakuu wa Vituo vya Afya hapa Manispaa ya Musoma. Tukawapa maelekezo ya utoaji huduma hasa kwa makundi maalumu wajawazito, watoto chini ya miaka mitano wazee na tunafanya ufuatiliaji kuona huduma zinatolewa kwa ubora kwa kuzingatia matakwa katika vituo vyote na kuhakikisha gharama zinazotozwa ndizo ambazo zinatakiwa,"amesema Bosco Ndunguru.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Nyasho, Haji Mtete amesema kuwa, dhamira ya Serikali ni kutoa huduma bora za afya kwa wananchi. Hivyo, watumishi wa kituo hicho cha afya wanapaswa kutimiza majukumu yao kwa kuzingatia sheria na taratibu za kazi yao i ili kuwapa huduma bora Wananchi wanaofika kupata huduma. 

Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Musoma, William Patrick Gumbo amewataka madiwani katika maeneo yao kufuatilia miradi inayotekelezwa kwa karibu katika maeneo yao sambamba na kuwa watatuzi wa migogoro badala ya kuikuza kwa masilahi mapana ya wananchi ambao wamewachagua kuwatumikia. 
Pia, Gumbo amewataka madiwani na watumishi wa halmashauri hiyo kuendelea kufanya kazi kwa pamoja na kwa ushirikiano ili kuhakikisha maendeleo ya Wananchi yanasonga mbele kwa ufanisi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news