Huzuni wanamichezo wanawake

NA ADELADIUS MAKWEGA 

MEI 2, 2023 Mwanakwetu alisoma taarifa katika vyombo kadhaa vya Habari vya Kimataifa juu ya kifo cha mwanariadha mweusi wa Marekani, Tori Bowie.
Kumbukumbu za Mwanakwetu zilikumbuka kuwa mwanamke huyu aliwahi kulipatia sifa kadhaa taifa la Marekani, huku bendera ya taifa hilo kubwa ikipanda juu na wimbo wa taifa hilo ukichezwa mara kadhaa katika mashindano ya kimataifa, Marekani ikinyakua medali ya fedha, shaba na dhahabu. 

Nayo magazeti, runinga na mitandao ya kijamii ikipambwe na picha za mwanariadha huyu akivishwa medali iwe yeye mwenyewe au katika timu ya riadha aliyoshiriki nayo kushinda medali hizo. 

Kifo hicho cha mwanariadha huyu kilimkumbusha Mwanakwetu uhodari wa mwanariadha huyu, 

“Tori Bowie au Frentorish alikuwa mkimbiaji wa mbio kama vile kukimbia na kuruka vihunzi mita 100 na 200, akishinda medali ya shaba na fedha mita 200 mwaka 2016, huko katika mashindano ya Olimpiki ya Rio de Janero. 

"Awali alishinda medali za fedha na dhahabu mita 100 mwaka 2015 na 2017 akawa mshindi wa dunia wa umbali huo. Pia alishinda medali ya dhahabu mita 100 kwa wanawake wanne wanne relai mara mbili mwaka 2016 na 2017 katika mashindano ya Olimpiki.” 

Taarifa ya kifo cha Tori Bowie ikisema mara baada ya watu wakaribu kutomuona kwa siku kadhaa karibu juma moja waliamua kwenda kwake, ndipo walibaini kuwa alikuwa amefariki dunia bila ya kutaja chanzo cha kifo hicho. Kwa hakika wanahabari walifanya kazi yao na siku chache baadaye vyombo vya Habari vya Kimataifa viliripoti, 

“Tori Bowie wakati anafariki alikuwa na ujauzito wa kati ya miezi saba au nane, huku akifariki akiwa na umri wa miaka 32 akizaliwa Agosti 27, 1990 na kufariki Aprili 23, 2023. “ 

Mwanakwetu alijiuliza, je mwanariadha Tori Bowie alifariki dunia kutokana na sababu za ujauzito ? Kulingana na medali alizoshinda Tori Bowie akiwa hai inaonekana wazi hakuwa mtu fukara angeweza hata kuwa msaidizi wa kumuhudumia katika hali hiyo ya ujauzito. Huku ikiaminika kuwa hakuwahi kuonekana na mwanamme yoyote yule kwa vipindi tofauti. Hoja ya kutokuwa na mume ikiibuka.

Kwa kuwa Tori Bowie alifariki akiwa na ujauzito huo wa miezi kati ya saba na nane na mara ya mwisho alishiriki mchezo huo mwaka 2019 huko London, Mwanakwetu alipata maswali ya kujiuliza hasa juu ya ushiriki wa wanawake katika michezo na afya zao za uzazi. 
“Je mwanamke anapokuwa katikaa siku zake, je anaweza kushiriki vizuri michezo kama alivyo katika hali yake ya kawaida katika mwezi?” 

Kwa kipindi cha mwezi mmoja tangu taarifa ya Tori Bowie ya Mei 2, 2023 hadi Juni 3, 2023 Mwanakwetu alijaribu kupita huku na kule kupata majibu katika hili kutoka kwa wanamichezo, matabibu na wajuzi wa lishe za wanamichezo. 

“Mwanamke anapokuwa katika hedhi anaweza kushiriki michezo kwa kiasi kidogo na mazoezi ya kawaida, japokuwa wapo akina mama ambao wanaweza kushiriki michezo kama wako katika hedhi wakiwa kama katika hali zao za kawaida kabisa.” 

Haya yalielezwa na Mtaalamu wa Lishe kwa wachezaji ambaye Mwanakwetu alimfikia huku akilifafanua hilo na kwa umbali zaidi, 

“Baadhi ya wanamichezo wa kike wakiwa katika hali hiyo huwa wanatumia vidonge vya kuzuia hedhi ili washiriki katika mashindano yaliyo jirani au yale mashindano ambayo yapo katika siku hizo ili kulinda medali zao na heshima za timu, makampuni walio na mikataba nao na mataifa wanaocheze na mara nyingi wanafanya hivyo kulinda nafasi zao katika timu hizo vibarua vyao visiote nyasi.” 

Mwanakwetu ndani ya mwezi huo alikuwa kigulu na njia na kupiga simu hapa na pale na aliwasiliana na daktari mmoja ambaye kwa kipindi kirefu tangu ahitimu utabibu wake amekuwa akiwatibu wachezaji. 

“Afya ya mchezaji kwa sehemu kubwa katika michezo ni mali ya kocha na yeye lazima afahamu kupitia tabibu wa timu ili aweze kumpangia mazoezi sahihi au kushiriki vizuri mashindano, kinyume chake mchezaji anaweza asifanye vizuri na hata akaumia maana afya yake haifahamiki kwa kocha wake .” 

Michezo mingi imeweka nafasi ya kumtoa mchezaji na kumuingiza mchezaji mwingine kutokana na dharura mbalimbali ikiwamo majeraha na ugonjwa. Kwa mfano katika Mpira wa Kikapu timu moja ina wachezaji watano ndani ya uwanja, huku wachezaji saba wakiwa benchi, ruhusa ya kubadilisha wachezaji wote watano. Katika Mpira wa Miguu timu inakuwa na wachezaji kumi na mmoja ndani ya uwanja huku wanaoweza kubadilishwa mchezoni ni watano. 

Kwa Mpira wa Wavu timu inakuwa na wachezaji sita ndani kiwanja kwa timu moja kumbadilisha mchezaji kunategemea mahitaji ya timu na wote sita wanaweza kubadilishwa. Kwa Netiboli uwanjani timu inakuwa na wachezaji saba na wanaweza kubadilsihwa wote, hoja lazima wawe katika orodha ya wachezaji katika mchezo huo. 

Kwa mchezo wa Mpira Kengele(Goal Ball) timu uwanjani inacheza wachezaji wa tatu lakini wanaoweza kubadilishwa mara nne, sharti katika nusu ya kwanza ya dakika 12 uwe umebadilisha mchezaji mmoja hiyo itakupa haki ya kufanya mabadiliko hayo matatu yaliyosalia. 

Wakurufunzi wa Michezo wanasema kuwa ipo michezo kadhaa ambayo haina nafasi ya mabadiliko kama vile ngumi, kuogelea, mieleka ya mtu mmoja mmoja na riadha ambayo ndiyo Tori Bowie alikuwa akikimbia. 

”Fikiria mchezaji wa riadha yupo katika orodha ya timu ya taifa, hapo analiwakilisha taifa lake, dharura inamkuta katika ya mchezo, hilo linashawishi kutumika mbinu zingine hata za kuzuia dharura hizo, usipomchezesha mchezaji huyo taifa, jamii na mashabiki wa timu/taifa hawawezi kukuelewa, wao wanataka ushindi tu. Hilo si kwa michezo ambayo haina nafasi ya kumbadilisha mcheza tu bali hata katika Mpira wa Miguu, Netiboli na mingineyo.” 

Timu za mataifa mbalimbali zinapokwenda kushiriki mashindano wapo wachezaji wengi ambao wanashiriki michezo mingi, hilo linasaidia hata kupunguza gharama za kifedha, mathalani Tori Bowie alikuwa anakimbia mbio hizo katika urefu mbalimbali na huko kote akilipatia taifa lake la Marekani medali kadhaa. 

Hilo ni zaidi kwa mataifa masikini, katika mshindano ya ndani ambapo mchezaji mmoja anaweza kucheza Mpira wa Miguu wa Wanawake, anacheza Netiboli, anakimbia riadha anacheza Mpira wa Kikapu na anacheza Mpira wa Wavu na hata Mpira wa Mikono. 

Mtu mmoja anayecheza michezo zaidi ya sita ni muhimu kusafiri naye katika mashindano kuliko kusafiri na wachezaji hao sita kila mmoja akicheza mchezo wake. Haya unaweza kuyaona katika mashindano mengi ya shule ziwe za msingi na hata sekondari. 

Mwanakwetu siku ya leo anasema nini? 

“Ni vizuri mabinti zetu kuanza kucheza michezo mapema na wakifikisha miaka 23, 24 wajiuzulu ili wawe labda walimu wa michezo na wakufunzi hilo linatatoa muda wa kufanya mazoezi mepesi na hilo linatoa muda wa kuweza kuingia katika mambo ya kifamilia ikiwamo kutafuta watoto, kinyume chake inaweza kuleta shida.” 

Daktari aliyezungumza na Mwanakwetu alisisitiza hilo, huku akitolewa mifano kadhaa ya wachezaji wa kike waliopata changamoto hizo. Jamii inafahamu mno wachezaji wao wa kiume na wanaonekana kuwa na familia zao, vipi kwa wachezaji wetu wa wanawake? 
Mwanakwetu anaweka chini kalamu yake akisema kuwa sasa ni wakati sahihi wa mashabiki wa michezo kuutazama ulimwengu wa mustakabali wa wanamichezo wetu wa kike wapo wapi baada ya kutupatia mafanikio na furaha tele, wao wamebaki na furaha au huzuni milele. 

Mwanakwetu upo? Nakutakia siku njema. 
makwadeladius @gmail.com 
0717649257

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news