Kwa hili, Uzanzibar na Utanganyika hapana!

NA MWALIMU MEIJO LAIZER

NI dhahiri kuwa, mjadala wa uwekezaji wa Bandari yetu ya Dar es Salaam umechukua nafasi kubwa katika jamii, katika vyombo vya habari na katika kada mbalimbali ndani na nje ya nchi yetu.
Katika mchango wangu wa awali juu ya uwekezaji wa bandari yetu ya Dar es Salaam nimeungana na Serikali yetu kupongeza kwa hatua nzuri ya kubuni uwekezaji mkubwa katika Bandari yetu ya Dar es Salaam.

Hata hivyo, pamoja na kufanya hivyo nimeungana na Watanzania wote wazalendo wanaotoa maoni yao na ushauri wa namna ya kuwekeza bandari yetu bila kuwapa wawekezaji kwa asilimia 100 na kuweka muda wa mkataba, lengo nchi yetu ibaki katika umiliki wake wa bandari yetu ya Dar es Salaam.

Suala la Uzanzibari na Utanganyika kuingizwa katika Mjadala wa Uwekezaji wa Bandari Yetu ni Siasa zilizopitwa na wakati jambo ambalo kwa Wachambuzi wa Masuala ya Siasa na Kijamii inaonesha kuwa, ni upotoshaji mkubwa inayoondoa Watanzania kujadili mambo ya msingi katika uwekezaji wa bandari yetu kwa lengo la kulinda rasilimali za nchi yao.

Wapo baadhi yetu na wengine ni wapinzani wanatumia dhana ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa kuwa wao ni Wazanzibar na suala la Bandari ya Dar es Salaam kupatiwa wawekezaji wa kigeni eti kwa sababu siyo Watanganyika haikustahili.

Jambo hili siyo jema kwa masilahi mapana ya Muungano wetu uliyoasisi na viongozi wetu wakuu wa Taifa letu Hayati Baba wa Taifa Mwlaimu Julius Kambarage Nyerere na Amani Abeid Karume.

Maswali yangu ya msingi kuhusu Uzanzibari na Utanganyika unaosemwa kwa uwekezaji wa bandari yetu ya Dar es Salaam ni haya yafuatayo:-

Mosi,Je? Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyepitia mkataba kuhusiana na uwekezaji wa bandari yetu ya Dar es Salaam ni Mzanzibari?.

Pili,Je? Watalaamu wetu wa sheria waliopo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kupata nafasi ya kushiriki katika suala zima la Uwekezaji wa Bandari yetu ya Dar es Salaam ni Wazanzibari wote?.

Tatu, Je? Baraza letu la Mawaziri ambalo jambo hili la Uwekezaji wa Bandari yetu limepita kwao na kufikia hatua ya kupelekwa bungeni ni Wazanzibari wote?.

Nne,Je? Wabunge wetu waliopata fursa ya kwenda Dubai kushiriki mazungumzo ya uwekezaji wa bandari yetu ni Wazanzibari Wote?.

Hapa tunaona Mbunge Dkt.Msukuma akijinazua katika tuhuhuma za kupatiwa rushwa na kuonesha mali zake alizojiwekezea kabla ya kupata ubunge, huyu kwake ni Mkoa wa Geita.

Tano,Je? Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Mwigulu Nchemba ni Mzanzibari? Sote tunamjua huyu ndio kinara wa kusimamia masuala ya kiuchumi kupitia Wizara ya Fedha, sote tunajua.

Sita,Je? Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lililopitisha na kuridhia azimio la uwekezaji na uendelezaji wa bandari ya Dar es Salaam kupitia DP World ni Wazanzibari?.

Mijadala hii inayoendelea kuhusiana na suala zima la uwekezaji wa Bandari ya Dar es Salaam iweze kutuweka pamoja kama Taifa.

Pia,iweze kutuweka kama Watanzania kwa taswira ya Muungano wetu, iweze kutufanya kutoa maoni mbadala kwa uwekezaji wa Bandari ya Dar es Salaam ili iwe na tija kama nchi.

Binafsi, bado naona kuna fursa nzuri ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan kuendelea kusikiliza ushauri na maoni ya Watanzania bila kujali mtazamo hasi inayotolewa na baadhi yetu katika uwekezaji wa Bandari ya Dar es Salaam, kwani kwa mujibu wa sheria za nchi yetu kila mtu ana uhuru wa kutoa maoni yake bila kuvunja sheria za nchi kulingana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Sote tunajua kuwa Watanzania wanataka maendeleo ya haraka kwa masilahi mapana ya Taifa letu na ni dhahiri kuwa Watanzania wanajua umuhimu mkubwa wa uwekezaji katika Bandari ya Dar es Salaam.

Pamoja na maoni na ushauri unaoendelea ni dhamira njema ya kila mmoja wetu kutaka uwepo wa uwekezaji wenye tija na kulinda rasilimali za nchi yetu na kuepuka kukabidhi wawekezaji kumiliki rasilimali zetu kwa asilimia 100 na kwa muda mrefu bila kuwekwa na kubainishwa kikomo kuhusu uendeshaji wa bandari yetu kwa wageni.

Jambo ambalo ni vema Serikali yetu ya Awamu ya Sita iweze kulitazama kwa kina kabla ya kufanya maamuzi ya uwekezaji huu mkubwa na wenye tija kwa masilahi mapana ya Taifa letu.

Rais wetu, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan ni muumini na kinara namba moja katika suala la kudumisha uhuru na amani katika nchi yetu ikiwemo kuulinda Muungano kwa ustawi bora wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kama ilivyoasisiwa na waasisi wa Taifa letu, hivyo dhana ya *Uzanzibari na Utanganyika* katika Mjadala wa Uwekezaji wa Bandari ya Dar es Salaam ninachelea kukubaliana na kauli hizo zinasotolewa na baadhi yetu kwa Sasa kwani Haina Tija kwa Taifa Letu.

Sote kama Watanzania tuungane kwa pamoja tukatae mijadala ya Uzanzibari na Utanganyika katika mjadala huu unaoendelea kuhusu Uwekezaji wa Bandari ya Dar es Salaam na Serikali ya Dubai kwa kutoa maoni na ushauri wetu wenye tija kwa Taifa letu.

Lengo, nchi iweze kupata maendeleo ya haraka na endelevu na kuweza kuwa na uchumi imara kwa masilahi ya wananchi na kwa vizazi vijavyo.

Kuzungumzia habari ya Uzanzibari na Utanganyika katika Mjadala wa Uwekezaji wa Bandari ya Dar es Salaam ni kutaka kujenga Ufa na Mgawanyiko ndani ya Watanzania kwa Masilahi ya Wanasiasa jambo ambalo halina tija kwetu kama Taifa.

Inaripotiwa na:-

Mwalimu Meijo Laizer
MNEC Mstaafu
Wilaya ya Siha
Mkoani Kilimanjaro

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news