Mtandao watoa tamko utumikishwaji watoto nchini

NA GODFREY NNKO

MTANDAO wa Kupinga Utumikishaji Watoto nchini (Tanzania Coalition Against Child Labour-TCACL) umeitaka jamii ya Watanzania kuendelea kuheshimu mikataba mbalimbali ya Kimataifa ambayo Tanzania imeridhia,
Sambamba na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 zikiwemo sheria, sera na mipango mbalimbali inayolinda haki za mtoto nchini.

Rai hiyo imetolewa leo Juni 12, 2023 jijini Dar es Salaam kupitia tamko la mtandao huo wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Kupinga Utumikishaji wa Watoto Duniani. Huku kauli mbiu ya mwaka huu ikiwa ni 'Haki ya Kijamii kwa Wote:Tokomeza Utumikishwaji Watoto'.

Mtoto hapa nchini anatafsiriwa kuwa ni mtu yeyote aliye chini ya umri wa miaka 18 kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto Na.21 ya mwaka 2009.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Child Welfare (TCW),Bi.Eddna Chandeu ambao ni wanachama wa mtandao huo amesema kuwa, kuna jitihada kubwa zinazoendelea kufanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi za kuhakikisha vitendo vya unyanyasaji na ukatili dhidi ya watoto vinadhibitiwa.

Amesema, licha ya jitihada hizo, bado jamii inayo nafasi kubwa ya kuhakikisha inashiriki kikamilifu ili kuwezesha kudhibiti vitendo vya utumikishwaji wa watoto ambapo matukio hayo yamekuwa yakifanyika ndani ya jamii mbalimbali nchini.

""Tunapoadhimisha siku hii, Tanzania Coaliation Against Child Labour (TCACL) inaungana na wadau mbalimbali wa haki za mtoto duniani katika kupinga utumikishwaji watoto, sambamba na kuelimisha jamii juu ya madhara ya ajira hizo.
"Mtandao unatambua na kuunga mkono juhudi mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali katika kutokomeza ajira kwa watoto ikiwa ni pamoja na kutunga Sheria ya Mtoto Sura ya 13 ambapo kupitia kifungu cha 12 kinaelekeza kuwa, mtoto hatahusishwa katika kazi yoyote ambayo inaweza kumsababishia madhara kiafya, kielimu, kiakili, kimwili na katika ukuaji wake,"amefafanua Bi.Chandeu.

Wito huo unakuja ikiwa Juni 12 ya kila mwaka huwa ni Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ajira kwa Watoto Duniani (World Day Against Child Labour). Siku hii ilianzishwa na Shirika la Kazi Duniani (ILO) mwaka 2002 kwa lengo la kutoa elimu ili kuzuia ajira kwa watoto. 

Aidha, ILO kupitia Mkataba wa Kimataifa Na.138 liliweka umri wa ajira kuwa miaka 15 na kuendelea, na katika Mkataba Na.182 liliorodhesha ajira zisizokubalika kwa watoto na ambazo zinatakiwa kuzuiwa.

Sheria ya Mtoto Na.21 ya mwaka 2009 nchini kifungu cha 81 kimetoa fursa na haki ya malipo kwa mtoto anayefanya kazi kwa mujibu wa sheria kulingana na uzito na ukubwa wa kazi husika.

Pia katika kifungu cha 85 (1) cha Sheria ya Mtoto Na.21 ya mwaka 2008 mwajiri anatakiwa kuwa na rejesta ya watoto wanaofanya kazi kwake au kupata mafunzo ya kazi kwake.
Rejesta hiyo pamoja na mambo mengine inatakiwa kuwa na kumbukumbu muhimu za umri wa mtoto na aina ya kazi anayofanya mtoto husika.

Kazi hatarishi

Miongoni mwa kazi hatarishi kwa mtoto ni unyunyiziaji wa madawa ya sumu na mbolea, uvunaji kwenye mashamba makubwa kama vile tumbaku, chai, kahawa, uendeshaji wa mashine za kilimo za aina zote, upaaji wa samaki, uvuaji wa samaki, ukaushaji wa samaki,kukaanga samaki, migodini, machimbo ya mchanga na kokoto, ujenzi na kazi za majumbani.

Kazi nyingine hatarishi ni kuhudumia kwenye sehemu za starehe kama baa,Casino,, nyumba za wageni, biashara ya ngono, biashara ndogondogo pembezoni mwa barabara, viwanda vidogo vidogo visivyo rasmi, usafirishaji, upakuaji mizigo na usafirishaji wa magari.

Aidha, kifungu cha 78, 79 na 80 cha Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 imekataza na kuzuia mtoto kufanyishwa kazi za kinyonyaji na majira ya usiku.

"Jumuiya ya Kimataifa iliwahi kuutangaza mwaka 2021 kuwa ni mwaka wa Kimataifa wa kutokomeza ajira kwa watoto, kwa sasa ni takribani miaka miwili imepita tangu uamuzi huo.

"Hatua hii ni muhimu sasa kutokana na tatizo la ajira kwa watoto kutishiwa kuvurugika kutokana na janga la UVIKO-19 lililoikumba Dunia kuanzia mwaka 2020,"amefafanua.

TCACL

Kwa upande wake, Mjumbe wa Bodi wa Mtandao wa Tanzania Coalition Against Child Labour (TCACL), Bw.Ibrahim Samata amesema kuwa, kwa mujibu wa kifungu cha 102 (2) cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ni kosa kisheria kumtumikisha mtoto.
"Hivyo, mtu atakayepatikana na hatia kwa kosa la kumtumikisha mtoto atakabiliwa na adhabu ya faini isiyozidi shilingi za Tanzania milioni tano au kifungo jela kwa mwaka mmoja, au vyote kwa pamoja kutegemeana na ukosaji wenyewe.

"Sheria hizi zinazomlinda mtoto zinasomeka sambamaba na kanuni za Sheria ya Mtoto zilizochapishwa katika Gazeti la Serikali namba 196/2012. Kati ya mambo ambayo mashirika haya yanayoendelea kufanya ni pamoja na kuongeza nguvu na kufanya kampeni na uelewa kwa wananchi juu ya ajira hatarishi kwa watoto,"amefafanua Bw.Samata.

Mambo mengine ambayo amesema wanaendelea kuyafanya ni pamoja na kuendelea kufanya kampeni shirikishi ya makundi mbalimbali ya jamii ili nao wapate uelewa na kuweza kusambaza elimu hiyo kwa wahanga na walengwa wengine.

"Tunaishauri jamii na wadau kujitahidi kukabiliana na ukatili wa ajira hatarishi kwa watoto katika ngazi ya kaya, kuhakikisha elimu inatolewa kwa jamii ili kuwajengea uelewa wa maana halisi ya utumikishwaji wa mtoto na namna ya kumlinda mtoto na ukatili huo,"amesema Samata.

Kwa mujibu wa Bw.Samata, mtandao huo unatoa wito kwa umma, Serikali wakiwemo wadau wa haki za watoto kuunganisha nguvu kupinga utumikishwaji watoto mahali popote nchini.

"Aidha, tunapendekeza, Serikali iendelee kuwasaidia watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani kurejea shuleni kwa kujenga mifumo bora itakayowawezesha kupata mahitaji yao ya kila siku.Na, Serikali iandae mkakati kabambe wa kuwabaini wanaowaajiri watoto na iwawajibishe kisheria,"amefafanua Samata.

Pendekezo lingine ni kwa jamii kuendelea kutoa ushirikiano kwa kuwafichua watu wote wanaowaajiri watoto huku wazazi wakitakiwa kuwatunza, kuwalinda na kuwapatia watoto mahitaji yao ya msingi.

Mwanasheria

Kwa upande wake mwanasheria, Davis Komba amesema, ili kuweza kukabiliana na changamoto ya utumikishaji wa watoto wameendelea kuwa mstari wa mbele kutoa elimu ya kisheria.

"Kupitia kesi au masuala yoyote ambayo yanahusika na ajira za utotoni hususani pia katika masuala ya usafirishaji, sisi kama taasisi na mashirika ambayo siyo ya kiserikali, kwanza kabisa tunaweka msisitizo katika jamii kwa kujua sheria ambayo inahusika na haya masuala.
"Sheria ya Watoto inazungumza kwamba, tatizo lolote au haki yoyote ya mtoto inapokuwa inakosewa mtu stahiki anayepaswa kulisimamia hilo suala ni Serikali, Serikali ndiyo pekee inaweza kusimamia hizo haki za mtoto.

"Na, ngazi ya kwanza kabisa ni kupitia kwenye Serikali za mitaa ambapo kuna maafisa ustawi wa jamii, ambao wapo na jukumu la kuhakikisha ustawi mzima wa mtoto unakwenda sawasawa, kwa hiyo msisitizo mkubwa kupitia mashirika yetu ni watu kuweza kufahamu huu utaratibu unakuwaje.

"Kwa hiyo sisi ushiriki wetu mkubwa ni kuhakikisha kwamba, wananchi wanakuwa na haki ya kuweza kutoa taarifa katika Serikali za mitaa endapo wataona kuna huo ukiukaji wowote wa haki ya mtoto na pia dawati la afisa ustawi wa jamii linakwenda polisi na baadae ile kesi inakuwa ni baina ya Serikali na yule ambaye amevunja haki ya mtoto,"amefafanua Bw.Komba. 

KIWOHEDE

Naye, Joseph Mugyabuso kutoka Shirika la Kiota Women Health and Development (KIWOHEDE) amesema, "Sisi kama KIWOHEDE ambao ni wanachama wa mtandao tumeweza kutambua watoto watano ambao wote walichukuliwa na kwenda kukaa Bunju.
"Kwa sasa wanapatiwa huduma mbalimbali katika kituo cha KIWOHEDE Bunju ambapo kuna shule ya sekondari na chuo cha ufundi, huku wakiendelea kupata msaada wa kisaikolojia ili kuweza kutengamaa baada ya kutumikishwa.

"Na kazi nyingi ambazo walikuwa wakitumikishwa ni kazi za ndani ambapo walikuwa hawalipwi chochote na walikuwa wameletwa huku Dar es Salaam kwa minajili ya kuja kusoma.

"Lakini, baada ya kufika Dar es Salaam ndiyo wakakutana na kadhia hiyo, kwa hiyo takribani tuna kesi tano ambazo mwaka jana tuliweza kuzishughulikia na hivi sasa zipo mahakamani na wengine tayari kesi zao zimeisha wamesharudishwa nyumbani kwao.

"Baada ya kupata elimu ya sekondari na elimu ya ufundi katika kituo chetu kilichopo Bunju ambao ni mwanachama wa Tanzania Coalition Against Child Labour,"amefafanua Joseph.

Ustawi wa Jamii

Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Jamii kutoka jijini Dar es Salaam, Joyce Agustino amesema, "Kwa upande wa Ustawi wa Jamii, sisi tumekuwa tukipokea kama sehemu ya usimamizi wa haki za watoto, lakini jambo hili tunalifanya kama utaratibu unavyotupasa kulifanya.

"Kwamba kupokea watoto ambao wamefanyishwa kazi, aidha majumbani au kwenye biashara au wale ambao wanaletwa kwa ajili ya kuuza kahawa, karanga, maji hao wote tunawapokea.
"Lakini, hata kwenye maduka, kuna maduka mjini ukienda Kariakoo unakuta kuna watoto wadogo, pia nao ni kundi hilo hilo ambao tumekuwa tukiwapokea, aidha wanakuja wakiwa na changamoto ya malalamiko au watu wamewaleta baada ya kuonekana wanateseka.

"Kwa hiyo kiujumla wake tumekuwa tukipokea haya mashauri na baada ya kuyapokea tumekuwa tukishirikiana na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali hata KIWOHEDE tumefanya nao kazi sana, tumekuwa tukiwapeleka kule kwenye hifadhi au maeneo mengine.

"Lakini, pia kufanya majadiliano na wale ambao tumewakuta nao ikiwemo kupelekwa kwenye vyombo vya kisheria kama polisi kwa ajili ya kuhakikisha kwamba watoto haki zao zinapatikana.

"Lakini pia tumeweza kuhusisha familia wanazotoka, kwa sababu baada ya kuwapata tunaanza kufanya uchunguzi kule wanakotoka ni wapi na maafisa ustawi wa wilaya ambazo wametoka, kwa hiyo kwa ujumla wake ndiyo namna ambavyo tunawahudumia watoto mara baada ya kuwagundua,"amefafanua Afisa Ustawi huyo. 

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news