Mwinjilisti Temba: Hata watumishi wa Mungu twendeni tukawekeze Kwala

NA DIRAMAKINI

MWINJILISTI wa Kimataifa, Alphonce Temba ametoa wito kwa Watanzania mbalimbali wakiwemo watumishi wa Mungu kwenda kuwekeza miradi mbalimbali ya maendeleo katika jiji la kibiashara na uwekezaji lililopo Kwala mkoani Pwani.

Temba ameyabainisha hayo ikiwa hivi karibuni Serikali imelieleza Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa, inatekeleza mpango wa kuanzisha, kupanga na kuendeleza jiji la kibiashara na uwekezaji Kwala mkoani Pwani.

Hayo yalibainishwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa Dkt.Angeline Mabula bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2023/24.

Mheshimiwa Waziri Dkt.Mabula alifafanua kuwa, katika kufanikisha mpango huo wizara hiyo kwa kushirikiana na wizara zingine za kisekta imeshiriki katika kuandaa mpango kabambe wa jiji hilo.

Alifafanua kuwa, mpango huo unahusisha eneo lenye ukubwa wa hekta 181,130 linalojumuisha vijiji 30 vya halmashauri za wilaya za Kibaha yenye vijiji 16, Kisarawe vijiji vitano na Chalinze vijiji tisa.

"Uanzishwaji wa jiji hilo unalenga kupata eneo kubwa zaidi la uwekezaji wa viwanda na shughuli nyingine za kiuchumi na pia kupunguza msongamano wa shughuli mbalimbali za kiuchumi katika Jiji la Dar es Salaam ikiwemo Bandari ya Dar es Salaam,"alifafanua Waziri Dkt.Mabula.

Kufuatia hatua hiyo, Mwinjilisti Temba ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kukamilisha ujenzi wa Bandari Kavu ya Kwala ambayo ni sehemu ya utekelezaji wa mipango ya jiji la kibiashara na uwekezaji Kwala.

Temba ametoa pongezi hizo baada ya kufika ilipo bandari hiyo na kushuhudia mafanikio makubwa ambayo amesema, uwekezaji huo ni hatua njema na ustawi bora kwa Taifa na jamii kwa ujumla.

"Nimefika katika Bandari ya Kwala ambayo itahudumia mataifa mbalimbali. Serikali imefanya kazi kubwa, chini ya uongozi mahiri wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan, ndiyo maana unaona sasa hivi uchumi unaenda kukuwa.

"Hivi karibuni, Katibu Mkuu wa Uchukuzi ametuambia kwamba,zaidi ya makontena 75,000 hadi 100,000 yatapatikana kwa mwaka, mizigo inaingia bandarini, itakuja mahali hapa.Mama umefanya kazi kubwa, tunakupongeza sana, Watanzania ni wakati wa kuhamka sasa, fursa zipo Kwala.

"Vigwaza, Chalinze, Kibaha na Pwani kwa ujumla. Zaidi ya ajira milioni moja za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja zinaweza kupatikana, tunakupongeza mama kwa kazi kubwa unayoifanya. Kwa kweli nimeshuhudia mambo makubwa sana ambayo yanafanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan.

"Mama anafanya kazi kubwa, kwa ustawi bora wa Taifa letu, jamii na wanananchi kwa ujumla, hivyo tutaendelea kumuunga mkono ili kuhakikisha maono yake ya kuliwezesha Taifa kuwa na maendeleo endelevu na kutekeleza kikamilifu Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inatimia kwa wakati,"amefafanua Mwinjilisti Temba.

Amesema, Rais Dkt.Samia amekuwa akipambambania na kutoa fedha nyingi kuhakikisha miradi ya kimkakati inatekelezeka kwa wakati ili iweze kutoa huduma kwa wananchi na kuhudumia mataifa ya nje.

"Bandari ya Kwala imetumia mabilioni ya fedha kwa ajili ya kuwatengenezea Watanzania fursa na kuweza kuhudumia mataifa zaidi ya saba Afrika yanayoizunguka Tanzania. Hivyo, ninakupongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt.Samia kwa hatua hii njema,"amefafanua Mwinjilisti Temba.

Burundi

Aidha, miongoni mwa mataifa yatakayonufaika na huduma za Bandari Kavu ya Kwala ni Burundi ambapo Oktoba, mwaka juzi Rais wa Jamhuri ya Burundi, Mhe. Evariste Ndayishimiye alitembelea bandari hiyo mkoani Pwani.
Mhe.Ndayishimiye alisema kuwa, eneo la bandari kavu (Kwala) litakuza biashara kati ya Tanzania na Burundi na litawasaidia kupunguza gharama za usafiri na fedha zitakazookolewa zitaenda kwenye miradi mingine.

“Mradi huu pia utapunguza gharama za bidhaa mbalimbali nchini Burundi, kwetu sisi Burundi, mtu akikupa eneo amekuthamini sawa na kukuunga undugu kwenye familia yake,”alisema Mhe.Ndayishimie.

Temba tena

Wakati huo huo, Mwinjilisti Temba amewataka Watanzania na watumishi mbalimbali wa Mungu kuchangamkia fursa na kuangalia maeneo yanayowafaa kwa ajili ya kuwekeza miradi yao huko Kwala.

Amesema, jiji la kibiashara na uwekezaji Kwala litakuwa na manufaa makubwa na litakuwa sehemu kubwa ya kuchochea kasi ya ukuaji uchumi kwa jamii, wawekezaji na Taifa kwa ujumla.

"Hivyo,yafaa kila mmoja wetu kushiriki kikamilifu kuunga mkono juhudi hizi njema za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania za kuwasogezea wananchi huduma na miradi ya maendeleo karibu kama ilivyo Kwala ambapo kwa sasa mji umebadilika na unakwenda kuwa wa kisasa zaidi,"amefafanua Mwinjilisti Temba.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news