NMB yakabidhi gawio Bilioni 45.5/- Serikalini, Rais Dkt.Samia aagiza

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan ameyataka mashirika yote ya umma kujiendesha kwa ufanisi, tija na ushindani ili yaweze kuwa endelevu.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akipokea mfano wa Hundi ya Shilingi Bilioni 45.5 (Gawio la Serikali) kutoka kwa Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB Bi. Ruth Zaipuna kwenye maadhimisho ya miaka 25 ya Benki ya NMB yaliyofanyika Mlimani City Jijini Dar es Salaam tarehe 17 Juni, 2023. Wengine katika picha ni Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba, Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya NMB Dkt. Edwin Mhede pamoja na Msajili wa Hazina Nehemia Mchechu wakishuhudia.(Picha na Ikulu).

Ametoa tamko hilo leo Juni 17, 2023 wakati wa hafla ya Benki ya NMB ya kukabidhi gawio kwa Serikali na kusherehekea miaka 25 ya safari ya mafanikio ya benki hiyo,iliyofanyika katika ukumbi wa Mlimani City.

Aidha, Rais Dkt.Samia amesema Serikali inaendelea kufanya tathmini ya utendaji wa mashirika yote ya umma na yale ambayo Serikali ina hisa kubwa ili kubaini mashirika yasiyo na faida yanayoshindwa kujiendesha na kuitia hasara Serikali.

Rais Dkt.Samia pia amesema, tathmini hiyo inafanywa na Msajili wa Hazina ambapo Serikali itayachukulia hatua na kuyafuta mashirika ambayo hayafanyi vizuri, kuyasaidia na kuyapa miongozo ya namna ya kujiendesha ili yapate faida.

Rais Dkt.Samia amewataka wajasiriamali, wakulima na wananchi wote wanaohudumiwa na benki ya NMB kuendelea kuwa waaminifu wanapochukua mikopo bila dhamana ili benki hiyo iendelee kuwa na ustawi.

Benki ya NMB imekabidhi gawio la shilingi bilioni 45.5 ambapo Serikali inamiliki asilimia 31.8 ya hisa katika benki hiyo huku asilimia zingine zikiwa zinamilikiwa na wadau kutoka sekta binafsi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news