OUT na VETA waja na Stashahada ya Uzamili katika Ualimu wa Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi

NA MWANDISHI WETU

KOZI ya Stashahada ya Uzamili katika Ualimu wa Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi inayotolewa na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) kwa kushikiana na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), imeanzishwa wakati muafaka kabisa.
Hayo yamesemwa leo Juni 27, 2023 na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dkt. Wilson Mahera kwa niaba ya Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI, wakati akizindua Programu Maalum ya Stashahada ya Uzamili katika Ualimu wa Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi kwa wanafunzi wanaodhaminiwa na Ofisi ya Rais-TAMISEMI katika Ukumbi wa Chuo cha Ualimu wa VETA kilichopo mjini Morogoro.
Akizungumza katika ufunguzi huo, Dkt.Mahera ametoa pongezi nyingi kwa taasisi hizo mbili kwa kuanzisha ushirikiano unaoonekana kuwa ni wa kipekee kwa kuanzisha kozi ambayo OUT wanatoa zaidi mafunzo huku VETA wakitumia karakana zao kuhakikisha wanafunzi wanaiva ipasavyo.

“Ili nchi ifikie malengo yake ya kimaendeleo ni lazima uwekezaji kwa upande wa sayansi na teknolojia upewe kipaumbele na uwekezaji mkubwa ambapo walimu hawa wanapopata mafunzo haya watakuwa na umahiri mkubwa zaidi katika kutoa elimu hizi za sayansi na teknolojia ili kuendana na utekelezaji wa dira ya maendeleo ya nchi ya mwaka 2025, ambayo inataka wananchi ambao wakitoka kwenye elimu waweze kukabiliana na changamoto za kimaisha na kuzishinda,”amesema Dkt.Mahera.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Prof. Elifas Bisanda amesema, mafunzo haya yanaendeshwa kwa kutumia zaidi Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kumfanya mwanafunzi aweze kumaliza mafunzo yake kwa muda mfupi, lakini pia anasoma huku akiwa kazini anaendelea kutimiza majukumu yake ya kikazi.
“Mafunzo haya tunaamini yatakuwa ufunguo wa kuhakikisha kuwa wataalam wa fani mbalimbali za ufundi wanaboreshwa na kuwezeshwa kufundisha kwa ustadi ili kwenda kuzalisha watu ambao watakuwa na nguvukazi ya kutosha katika ufundi,”amesema Prof.Bisanda.
Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, amesema lengo kuu la muunganiko huu wa OUT na VETA kushirikiana katika kutoa elimu hii pamoja na kuhakikisha kuwa serikali inafikia malengo yake ya kuwa na walimu wa kutosha na nguvu kazi itakayoshiriki katika utoaji wa elimu ya ufundi na ufundi stadi ambayo ipo mahiri na ina uwezo wa kutosha.

“Ushirikiano huu umeweza kutujenga zaidi katika kuimarisha uzoefu tunaobadilishana kupitia utoaji wa haya mafunzo na matunda yameanza kuonekana. Sote tunajenga nyumba moja hivyo tunatarajia kujiimarisha zaidi ili kuhakikisha kuwa wigo wa upatikanaji wa walimu nchini ambao wanakuwa na ujuzi na uelewa katika elimu ya ufundi na ufundi stadi nchini unaongezeka,"amebainisha CPA Kasore.
Kozi ya Stashahada ya Uzamili katika Mafunzo ya Ufundi na Ufundi Stadi ambayo ilipata ithibati yake mwaka 2020, inatolewa kwa pamoja kwa kushirikiana baina ya OUT na VETA ili kutoa taaluma ya ualimu kwa walimu wa Ufundi na Ufundi Stadi ili kuwapa umahiri katika ufundishaji. 
Halikadhalika, hii programu maalum ya stashahada ya Uzamili katika Ufundi na Ufundi stadi iliyozinduliwa leo imekuja baada ya Ofisi ya Rais-TAMISEMI kutoa udhamini kwa takribani walimu 87 wa fani mbalimbali za ufundi kusoma stashahada ya uzamili katika ualimu wa ufundi na mafunzo ya ufundi stadi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news