RC SENYAMULE AAGIZA CHEMBA KUJIPANGA UPYA

NA MWANDISHI WETU

MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule amesema hajaridhishwa na kasi ya ujenzi wa Shule Mpya ya Msingi katika Kijiji cha Magungu, Kata ya Mpendo, Wilaya ya Chemba na kukemea vikali uongozi wa Kijiji kukusanya fedha kwa wananchi bila kufuata utaratibu.
Senyamule ameyasema hayo leo Juni 13,2023 mara baada ya kufanya ziara yakukagua utekelezaji wa miradi ya boost katika Wilaya ya Chemba.

"Sijaona dhamira ya dhati katika ukamilishaji wa mradi huu kwa muda tuliokubaliana wa tarehe 30/6/2023, tumekubaliana sote kuwa miradi hii ikamilike kwa wakati lakini leo nimesikitishwa sana hatua hii ya ujenzi ambao uko katika hatua za awali," Senyamule amefafanua.

Amesema hayuko tayari kuona dhamira njema ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwaletea wananchi maendeleo hususan katika nyanja ya elimu haifikiwi kutokana na watu wachache kutotimiza wajibu wao.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe.Rosemary Senyamule akiongea na Wananchi waliojitokeza kushiriki na kusaidia kazi mbalimbali katika Utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa vyumba vinne (4) vya madarasa ya Shule ya Msingi Birise leo tarehe 13/06/2023 alipofanya ziara ya kikazi ya kukagua miradi inayoyotekelezwa kupitia fedha za Mradi wa Boost.

"Katika mradi huu Chemba hamjafika hata asilimia 20 na mna siku 18 zimesalia, fedha zilitolewa kwa wakati mmoja nchi nzima, Wilaya nyingine za Mkoa wa Dodoma wako katika hatua za upauji, siko tayati kumuangusha Mhe. Rais, ujenzi ufanyike mchana na usiku," Senyamule ameagiza.

Katika hatua nyingine Mhe. Senyamule amekemea vikali utaratibu unaotumiwa na Mwenyekiti wa Kijiji cha Magungu Bw. Bernard Kapaya kuchangisha fedha wananchi bila kibali cha Mkuu wa Wilaya.
"Naomba kuwakumbusha kuwa Serikali imetoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Shule mpya, vyumba vya madarasa ya awali na msingi, nyumba za walimu na ujenzi wa Vyoo. Wananchi wasishurutishwe kuchangia fedha, wachangie kwa hiari yao wenyewe na utaratibu ufuatwe ikiwa ni pamoja na kuambatanisha muhtasari wa mkutano wa Serikali ya Kijiji na barua iliyopitishwa kwa Mkurugenzi kwenda kwa Mkuu wa Wilaya. Ni kinyume kuchangisha fedha bila kufuata utaratibu huo,” Senyamule ameonya.

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Chemba Bw. Gerald Mongella amesema kumekuwa na ucheweshaji kutokana na kusuasua kwa mchango wa nguvu za wananchi hali iliyopelekea ucheleweshaji wa upatikanaji wa madini.
Maendeleo ya ujenzi wa Madarasa ya Shule ya Msingi Magungu, Shule ya Msingi Birise, Shule ya Msingi Lahoda na Shule ya Msingi Handa ‘B’ yanayoyojengwa wilayani Chemba kupitia fedha za mradi wa Boost.
Mkoa wa Dodoma kupitia mradi wa Boost umepokea kiasi cha Shilingi Bilioni 10.6 kwa ajili ujenzi wa Shule mpya 16, vyumba vya madarasa ya msingi 163, madarasa ya awali 16, ujenzi wa vyoo 106, nyumba za walimu 03 na darasa 01 la elimu maalumu. Wilaya ya Chemba imepokea kiasi cha shilingi Bilioni 1.3.

Katika ziara yake Mhe. Senyamule amekagua maendeleo ya ujenzi wa Shule mpya ya Magungu, Ujenzi madarasa katika Shule ya Msingi Birise, ujenzi wa madarasa Lahoda na Ujenzi wa shule mpya Handa ‘B’.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news