Serikali yawauma sikio maofisa biashara nchini

NA FRESHA KINASA

SERIKALI imewataka maofisa biashara nchini kutoa huduma bora kwa wafanyabiashara katika halmashauri zao na kuwa na mahusiano bora na kundi hilo hatua ambayo itasaidia kuongeza ukusanywaji wa mapato ya Serikali katika kutekeleza miradi ya maendeleo kwa wananchi. 
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Mara, Robert Msalika Makungu leo Juni 28, 2023 Mjini Musoma wakati akihitimisha mafunzo kwa Maofisa Biashara 138 kutoka mikoa 10 ya Tanzania Bara ambayo yamefanyika katika ukumbi wa Uwekezaji uliopo ofisi ya Mkuu wa mkoa huo kwa siku tatu kuanzia Juni 26, 2023 hadi Juni 28, 2028. 

Makungu amesema, maofisa biashara wanalo jukumu la kuhakikisha wanakuwa walezi wazuri wa wafanyabiashara kwa kuwapa ushauri, mbinu na wahusike kikamilifu kuweka mazingira wezeshi ya uanzishwaji wa viwanda na biashara mpya zitakazozalisha ajira na kuchochea maendeleo ya kiuchumi. 

Pia, amewataka wajiepushe na rushwa katika utoaji wa leseni kwa wafanyabiashara Sambamba na kuwa waadilifu kwa kuweka mbele maslahi ya nchi kwani dhamana waliyopewa ni muhimu katika kuifanya sekta hiyo iwe na mchango mkubwa katika kuongeza mapato ya serikali. 
"Kazingatieni weledi katika utekelezaji wa majukumu yenu, Serikali inahitaji Kodi iweze kujiendesha na kodi hizo zitapatikana kwa wingi iwapo mtajenga Mahusiano mema na wafanyabiashara ili biashara zao zikue lakini pia katoeni elimu kwa wafanyabiashara. wengine wanaanzisha biashara lakini wanashindwa kuziendeleza badala yake zinakufa wao wanarudi nyuma na Serikali inakosa kodi," amesema Makungu. 

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa sehemu ya Leseni za Biashara kutoka BRELA Tawi Kilumile amesema kuwa, mafunzo hayo yatakuwa endelevu kwani yapo kwenye sehemu ya utekelezaji wa mpango mkakati wa brela yakilenga kuwajengea Maafisa biashara uwezo wa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi. 

Amesema kuwa, mpaka sasa mafunzo hayo yamekwisha tolewa kwa Maofisa Biashara wapatao 569 kati ya Maafisa biashara 682 waliopo nchini katika kuhakikisha kwamba wanaendana na malengo ya serikaki. 
Amewahimiza kuyafanyia kazi mafunzo hayo kwa vitendo na kwa tija katika maeneo yao kusudi kuiwezesha Serikali kufikia adhma ya kuwa na biashara zenye tija katika kuchochea maendeleo katika nyanja mbalimbali. 

Naye Rose Tungu Ofisa Biashara wa Mkoa wa Shinyanga amepongeza Brela kwa kutoa mafunzo hayo ambapo amesema amejifunza mambo muhimu ikiwemo mabadiliko ya sheria za leseni za vileo na hivyo ataweza kutoa huduma bora kwa Wafanyabiashara. 

Kwa mujibu wa sheria Brela inahusika na utoaji wa leseni za kundi A ambazo ni leseni za biashara za kitaifa na kimataifa ikiwemo viwanda huku Tamisemi ikihusika na utoaji wa leseni za kundi B ambazo ni biashara ambazo hazina sura ya kitaifa na kimataifa.

Mafunzo hayo ya siku tatu yenye lengo la kuwajengea uwezo Maofisa Biashara kuhusu sheria ya leseni na biashara ya mwaka 1972 walitoka katika halmashauri za mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Tabora, Kigoma, Geita, Shinyanga, Mwanza, Kagera na Mara ambao wamepewa mafunzo hayo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news