SIMULIZI YA KUTISHA KATIKA MAISHA-31

NA WILLIAM BOMBOM

Ilipoishia...mchawi huyo alikuwa aneshika ziwa bichi la mwanamke alilokuwa akiling'ata na kutafuna mithili wa mbuzi.
Ziwa hilo lilikuwa limeoza tena lilikuwa likinuka kuliko maelezo, lakini mchawi huyo hakujali hata kidogo. Alipowasogelea abiria hao walionekana kutetemeka zaidi, aling'ata kidogo ziwa lile kisha aka...

Endelea

Akamkabidhi miongoni mwao wale abiria titi hilo, harufu yake ilikuwa kali kuliko maelezo. Yule abiria alilipokea titi hilo huku mikono yake ikiwa inatetemeka mithili ya mawimbi ya bahari.

Wakati huo alikuwa akisubiri maelekezo toka kwa mchawi huyo, asingewe kufanya jambo lolote. Mapigo ya moyo yalikuwa yakimuenda mbiyo mithili ya mwizi wa bata anayefukuzwa na wananchi wenye hasira kali.

Wakati huo yule mchawi alikuwa anamuangalia kwa hasira, macho hayo hayakuonesha chembe ya mzaha hata kidogo.

Kwa upande mwingine yule abiria aliyekuwa kakabidhiwa kibuyu cha damu, naye alikuwa akisubiria maelekezo toka kwa mchawi aliyempatia kibuyu hicho.

Wakati huo gari lilikuwa limefika kituo kikuu cha MAGARI NYAMHONGOLO,lilisimama kwa ajili ya kumpandisha mchawi mmoja kituoni hapo.

Kabla hajapanda mchawi huyo yule abiria aliyekuwa amepewa kibuyu cha damu, aliutumia mwanya huo kucheza karata yake ya mwisho.

Kwa kuwa alikuwa karibu na mlango, aliruka na kumkanyaga teke mchawi aliyekuwa akipanda ndani ya gari.

Bahati ikawa upande wa abiria huyo, lile teke lilimpata sawia yule mchawi tumboni mwake akadondoka chini ya gari mfano wa furushi la mchanga.

Pale chini alibaki anagaragara mfano wa punda anayecheza kwenye majivu. Kile kibuyu cha damu kilidondoka lami, damu ikasambaa chini mithili ya mbuzi aliyechinjwa.

Yule abiria hakuwa na muda wa kusubiria, alisimama na kuanza mbio mithili ya wakimbiza mwenge wa Taifa.

Alifuata barabara ya kurudi mji wa Igoma, lakini kabla hajafika darajani ghafla lilitokea fuso ambalo lilimgonga mgongoni akadondoka chini.

Lilipita juu yake na kumsagasaga mithili ya nyama za sambusa, yote haya yalikuwa yakitendeka machoni mwa wale abiria wengine.

Mbaya zaidi wale wachawi hawakuwa wakijishughulisha na yote yaliyokuwa yakiendelea, mlango wa gari ulifungwa baada ya yule mchawi aliyekanyagwa teke kupanda.

Huo ukawa mwisho wa maisha ya abiria huyo, biashara ya matunda, mbogamboga za majani ikawa ni chanzo cha kukatisha uhai wake.

Mtoto THE BOMBOM na kundi lake walikuwa wametulia ndani ya gari hilo, hawakutaka kuingilia kesi isiyowahusu waliamua kuwaachia abiria hao kesi yao.

Yule mchawi aliyemkabidhi titi yule abiria, alimuonesha ishara ya kung'ata na kutafuna ziwa hilo, yule abiria mikono yake ikawa anatetemeka mfano wa uji ndani ya sinia.

Alinyanyua mikono yake kulipeleka kinywani mwake, kutetemeka kukazidi zaidi. Harufu nzito ya uvundo ilihanikiza eneo zima, hali haikuwa nzuri hata kidogo kwa upande wa abiria huyo.

Alitamani angalau ardhi ipasuke ajichimbie ndani yake ili ayakimbie madhira hayo, lakini haikuwezekana.

Kabla titi hilo hajaling'ata abiria huyo, alihisi likivutwa na mtu aliyekuwa hamuoni machoni mwake. Wale wachawi wakabaki wakishangaa kitu kilichokuwa kikifanyika mbele yao, lile titi lilipotea kimiujiaza miujiza mbele ya upeo wa macho yao.

Ilileta taharuki kwa wachawi waliokuwa ndani ya gari, jambo hilo lilikuwa geni machoni mwao. Toka wajiunge na kambi hiyo hili lilikuwa tukio la kwanza katika maisha yao.

Hapa niseme kidogo, ndugu msomaji baada ya mtoto THE BOMBOM kuchoshwa na uonevu uliokuwa ukifanywa ndani ya gari hilo aliingilia kati.

Kwa kuwa hakuwa akionekana machoni mwa wachawi wa gari hilo, alimtuma mchawi mwenzake kumnyakuwa abiria huyo nyama ya titi.

Mchawi huyo alipomnyang'anya ziwa hilo yule abiria, wachawi ndani ya gari walitahamaki. Wakagundua hawakuwa salama hata kidogo ndani ya gari lao, waliamini kuwa hawakuwa peke yao tu bali kulikuwa na kambi nyingine ya kichawi.

Walianza kuhaha wakimwaga madawa kadha wa kadha ya uoni, lakini wapi mambo yaliendelea kuwa kimya.

Wakiwa wanawaza na kuwazua wachawi hao ndani ya gari, ghafla gari lao lilisimama kukatokea kimbunga ndani ya gari hilo.

Kimbunga hicho kilisukasuka gari hilo kwa muda wa dakika kadhaa, wachawi hao hawakuwa wakionana tena.

Mtoto THE BOMBOM na kundi lake waliutumia muda huo kuwashusha wale abiria waliokuwa wamepanda gari hilo.

Baada ya dakika tano upepo ulitulia kukawa shwari kabisa, kitendo hicho kiliwashangaza sana wachawi wa gari hilo.

Walivyotahamaki wakiwa wamebakia wenyewe, hakukuwa na wale abiria ndani ya gari. Kitendo hicho kiliwaongezea hasira, wakajihapiza kufikisha taarifa hizi kwa viongozi wao ili hatua kali zichukuliwe.

Wale abiria walibaki wakishangaa namna walivyookoka mikononi mwa wachawi hao. Waliyoyashuhudia ndani ya gari hilo yalikuwa mazito, kila mmoja alikuwa na gagasiko kuu ndani ya mtima wake.

Hapa niseme kidogo, ndugu msomaji kwa watu mnaosafiri usiku mnapaswa kuwa makini sana na aina ya usafiri mnaotaka kupanda.

Kwa usafiri wa barabarani yaani kwa upande wa magari, wachawi huwa na magari yao ambayo hufanya kazi usiku.

Magari hayo ya kichawi yanaweza kufanana sana na yale tuliyoyazoea, kufanana huko huwa ni picha ya gari halisi huchukuliwa na kuwekwa kwenye gari la kichawi kwa malengo maalumu.

Muda mwingine ni vigumu sana kwa mtu wa kawaida kuyatofautisha magari hayo ya kichawi na yale halisi.

Unapoona gari linakuja usiku likiwa linatoa muungurumo wa kubembeleza sana, kuwa makini sana na aina hiyo ya gari.

Gari hilo likifika kituoni halafu usisikie kondakta akizungumza chochote kama ilivyo kawaida ya makondakta, kaa pembeni usipande gari hilo kwa kuwa ni la kichawi.

Mara nyingi magari ya namna hii huanzia saa tano za usiku hadi saa tisa, watu wengi wamewahi kupotea ndani ya jamii kwa uzembe wa aina hii.

Mara nyingi ukipanda gari hilo ni vigumu kurudi, unakuwa umechukuliwa msukule maishani mwako. Kwa upande wa wasafiri wa majini napo zipo meli, vivuko au mitumbwi ya kichawi.

Meli au vivuko vya kichawi hufanana kwa kila kitu na meli mlizozoea maeneo yenu, hata ukiiona ni ngumu kushituka mpaka uwe umeelezwa.

Mambo yanayoweza kukusaidia ni uwakaji wake wa taa huwa mkali kuliko kawaida, pia kipenga chake wakati inafika na kuondoka huwa kikali sana na hufanya fujo sana.

Ukiona mambo hayo usipande meli au kivuko hicho, kwa kawaida usafiri huo hufanyika wakati wa usiku.

Baada ya mtoto THE BOMBOM na kundi lake kuwasaidia abiria wale, nao walishuka ndani ya gari hilo na kutembea kwa miguu.

Kitendo cha gari la kichawi kusimama ghafla kisha kutokea kimbunga hakikuwa cha bahati mbaya, ilikuwa ni mipango thabiti ya mtoto huyo na kundi lake.

Eneo ilipopatia hitilafu gari hiyo ilikuwa ni mji wa Kanyama, mji ambao mtoto huyo alikuwa kakabidhiwa eneo kwa ajili ya kujenga KANISA LA KICHAWI.

Hii ilibaki kuwa siri yake na kundi lake, japo kwa nje watu wengi walikuwa wakiamini eneo hilo kutajengwa kanisa juu ya Mlima Makamelwa.

Mtoto huyo aliongozana na kundi lile la wachawi na yule mateka mmoja aliyeachwa na wale Wazungu kule makaburini Igoma.

Walipanda mlimani hapo kulikagua eneo hilo na kushauriana mambo kadha wa kadha. Wakiwa mlimani hapo walijadili mambo mbalimbali, hatimaye wakakubaliana usiku unaofuata walipaswa kuja kulizindika eneo hilo.

Mipango ya ujenzi wa kanisa hilo haikuwa mbali, hivyo walipaswa kulizindika eneo hilo kabla ya ujenzi, wakati wa ujenzi na baada ya ujenzi. Eneo hilo lilihitaji mazindiko mazito maana ni eneo ambalo waamini wake dunia nzima watakuja kuhiji.

Wakiwa bado eneo hilo ghafla kitu mfano wa nyota kilishuka kutoka mbinguni kwa kasi ya ajabu. Nyota hiyo iliyokuwa na pembe tano ilikuwa kubwa zaidi ya dunia, kadri ilivyokuwa ikishuka ndivyo ilizidi kuwa ndogo.

Wale wachawi wakawa wanasemezana juu ya tukio hilo, lakini mtoto THE BOMBOM aliwaondoa wasiwasi ikabidi watulie.

Mwanzoni walitaka kuamini kuwa siku hiyo ilikuwa ya kiama, namna ya nyota hiyo ilivyoanza kushuka ilionesha ingeisambaratisha dunia nzima.

Lakini kitendo cha kupungua umbo kadri ilivyokuwa ikishuka, iliwapunguzia wasiwasi wachawi hao wa kundi la mtoto THE BOMBOM.

Nyota hiyo ilikuwa iking'ara mfano wa nyota ya jaha, iliendelea kushuka kwa kasi ya ajabu. Hatimaye nyota hiyo iliangaza eneo lote la mlima Makamelwa, ilikuwa imefika eneo la juu la mlima huo huku ikiwa juu ya usawa alipokuwa kasimama mtoto huyo.

Ghafla ile nyota iliendelea kuwapungua na kufikia umbi la punje ya mahindi, mwanga wake uliendelea kutamalaki eneo zima la mlima.

Hatimaye nyota hiyo ilishuka kichwani mwa mtoto huyo kisha ikazama kichwani mwake, yote hayo yalifanyika machoni mwa wachawi wote waliokuwepo eneo hilo.

Mwili wa mtoto THE BOMBOM ulibadilika na kungara kama mbalamwezi changa, macho yake yakawa yanametameta mfano wa mchanga wa baharini.

Kikasikika kikohozi toka mbinguni "Kho! Khoo! Khooooo!" Kikifuatwa na sauti kuu iliyokuwa ikisema *Ntemi wamabala! Ntemi wamabala! Ntemi wamabala. Ikiwa na maana kiongozi wa dunia.

Kisha sauti hiyo ikatoweka, mfano wa upepo wa kisulisuli. Wale wachawi walibaki wakimtazama mtoto huyo kwa macho ya kushangaza.

Mwili wa mtoto THE BOMBOM uliendelea kung'ara kwa muda wa dakika tano kisha ukarudi katika hali ya kawaida.

Wale wachawi wakabaki wakisema "Hakika huyu ni mwana wa mungu" wakapiga kelele juu ya mlima Makamelwa wakilitukuza jina la mungu wao kisha wakarudi kambini kwao.

Ndugu msomaji mambo yanazidi kunoga katika simulizi yetu ya KANISA LA KICHAWI. Vita ya mtoto huyo na Wazungu itakuwaje? Unadhani kwa nini nyota hiyo imeingia mwilini mwa mtoto THE BOMBOM? Endelea kufuatilia kisa hiki cha kusisimua sehemu inayofuata.

IKELESIA

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news