TANAPA yavunja rekodi ya mapato, Waziri Mchengerwa asema yajayo ni makubwa zaidi

NA BRIGITHA KIMARIO

HIFADHI za Taifa Tanzania (TANAPA) zimeendelea kuonesha ufanisi wa hali ya juu ambapo kwa miezi 10 tu ya mwaka huu wa fedha, zimeshakusanya shilingi Bilioni 291. 

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mheshimiwa, Mohamed Mchengerwa amesema mafanikio hayo yametokana na kuongezeka kwa idadi ya watalii kitaifa katika Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA). 
Ameyasema hayo wakati akiwasilisha Bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii katika Bunge la 12, mkutano wa 11 kikao cha 39 jijini Dodoma leo Juni 2,2023.

“Taasisi za utalii nchini zimevunja rekodi ya mapato katika maeneo yao mfano TANAPA kwa mwaka mzima wa 2021/22 walikusanya shilingi bilioni 174, kwa miezi 10 tu ya mwaka huu wa fedha, wameshakusanya shilingi Bilioni 291 mapato haya kwa taasisi ni makubwa kuliko yoyote yaliyowahi kukusanywa tangu zianzishwe.”
Aidha, mapato hayo amesema yametokana na juhudi zilizofanyika za pamoja kutangaza vivutio vya utalii na kuimarika kwa miundombinu ya utalii ndani ya hifadhi.

Aliongeza kuwa,shirika litaendelea na juhudi zote kuimarisha shughuli zake za ulinzi, ikolojia, kutangaza utalii, kukusanya maduhuli na kuimarisha miundombinu ili waendelee kuvunja rekodi na watalii kufurika zaidi katika hifadhi zetu.
"Shirika litaendelea kuboresha miundombinu ya huduma za utalii kwa kujenga barabara mpya zenye urefu wa kilomita 500 na kukarabati kilometa 10,500. Vilevile shirika litakarabati kilomita 300 za njia ya miguu za kupanda milimani; kujenga mifumo ya usambazaji wa maji safi na malango 10 ya kukusanya mapato katika hifadhi za Taifa Ibanda-Kyerwa (1), Serengeti (2), Kilimanjaro (1), Tarangire (1), Ruaha (1), Katavi (1), Nyerere (1), na Mikumi (2). 
"Pia, Shirika litajenga studio ya kurusha vivutio vya utalii mubashara utakaowezesha vivutio kurushwa moja kwa moja kwenye mitandao na chaneli za kimataifa.”
Wizara ya Maliasili na Utalii leo imewasilisha makadirio ya Bajeti ya jumla ya Shilingi 654,668,208,000 kwa mwaka wa fedha 2023/2024 matumizi ya fungu 69 kwa mwaka wa fedha. Kati ya fedha hizo shilingi 486,501,449,000 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi 168,166,759,000 ni za miradi ya maendeleo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news