SIMULIZI YA KUTISHA KATIKA MAISHA-34

NA WILLIAM BOMBOM

Alitoka nje akiwa kwenye umbo lile la paka, akaelekea kwenye ungo alipouficha kisha akafanya taratibu za kupaa. Punde si punde alionekana hewani akielekea kambini kwao.

Endelea

Ndugu msomaji hapa niseme kidogo, kwa kawaida usafiri wa ungo huendeshwa na dereva mmoja. Usafiri huu unaweza kubeba abiria zaidi ya mmoja na kuendelea, kutegemea na ukubwa wa ungo wenyewe.

Kuna ungo ambao unaweza kubeba abiria watano, sita, kumi, kumi na tano hadi ishirini kwa mpigo. Itambulike kuwa usafiri huo siyo ungo, isipokuwa sehemu yake ya juu imekaa katika umbo la ungo ndiyo maana unaitwa ungo.

Umbo halisi la kifaa hicho huwa hauzidi kiganja cha mtu mzima, isipokuwa kuna maneno ambayo dereva huyasema ndipo hupanuka wenyewe.

Dereva husika huwa anajua ukubwa wa kifaa chake, endapo wanaosafiri ni watano dereva huzungumza maneno fulani kifaa hicho kinatanuka nafasi ya kutosha watu watano.

Yapo masharti mengi ambayo abiria wa chombo hicho ni lazima ayazingatie, miongoni mwake ni kuwa uchi wa mnyama pamoja na kufumba macho mpaka mwisho wa safari.

Ni dereva pekee ambaye huwa amefumbua macho, abiria wote ni sharti wafumbe macho mpaka dereva atakapowataarifu mwisho wa safari yao.

Endapo mchawi atakaidi akafumbua macho ndiyo hao hupata ajali, huanguka vibaya na kukutwa na watu wa kawaida maana anapoanguka lazima akili iyumbe kidogo.

Si kila mchawi anamiliki ungo, wengine hawana uwezo wa kumiliki chombo hicho hivyo wanapokuwa na safari hukodi.

Ungo unaweza kutua maeneo yeyote, lakini kwa usalama zaidi hutua kwenye viwanjwa vya shule, makanisa, misikiti na sehemu zingine za wazi.

Maeneo hayo huwa salama zaidi kwa kuwa huwa hayajazindikwa, pia wachawi mara nyingi shughuli zao kuu hufanyika maeneo hayo.

Kwa kuwa alikuwa peke yake ndani ya ungo huo mtoto THE BOMBOM, hakuwa na haja ya kufumba macho aliendesha kwa kasi ya ajabu ungo huo akielekea kambini kwao.

Kadri unavyokwenda mbali ndivyo utakwenda juu zaidi, mfano mtu anayetoka Mwanza kwenda Dodoma umbali wa juu ya uso wa dunia atatofautiana na yule anayekwenda Morogoro au Dar es Saalam.

Kadri unavyokwenda mbali ndivyo urefu wa kwenda juu uongezeka. Kwa kifupi usafiri huo hautofautiani sana na usafiri wa ndege za kawaida, japo usafiri wa ungo una kasi kubwa zaidi ya ndege za abiria.

Taa za ungo huwaka zaidi maana hutumia viganja vya binadamu, mafuta yake hutokana na mwili wa binadamu.

Mtoto huyo akiwa nyuma ya usukani wa ungo, alikuwa akipangua gia na kuongeza kasi ili kuwahi kambini kwake.

Siku hiyo walikuwa wamepanga kwenda kuzindika eneo lote la kanisa lao pale Mlima Makamilwa kwenye mji wa Kanyama, akiwa hewani ghafla aliona miale ya mwangu mingi iliyokuwa ikija upande aliokuwa akielekea.

Miale hiyo ilizidi kusogea karibu kadri alivyokuwa akisonga mbele, akaamua kubadili uelekeo ili kuepuka madhira aliyoanza kuyahisi mbele ya safari yake.

Alipochepuka kidogo kuiacha njia aliyokuwa akipita, alishangaa kuona gogo kubwa likipita kwa kasi ya ajabu kwenye njia aliyokuwa akipita.

Lilikuwa gogo kubwa mfano wa miti ya nguzo za umeme, alipogeuka kutazama vyema alishangaa kuwaona wazungu watatu waliokuwa wamepanda gogo hilo wakiendelea na safari zao.

Endapo angeng'ang'ania kubaki kwenye njia hiyo maisha yake yangekuwa historia, kwa ukubwa wa gogo hilo hakika ule ungo ungegongwa na kusambaa kabisa.

Akiwa bado kwenye hekaheka ya kuweka sawa ungo wake, alishangaa kuona gogo jingine likiwa karibu yake.

Safari hii alikishusha kidogo chombo chake na kuhama kwenye njia aliyokuwa awali, gogo hilo lilipita kwa kasi ya ajabu mithili ya makombora ya Korea Kaskazini.

Alibahatika kuwaona tena abiria wawili ndani ya gogo hilo pamoja na dereva wakawa watatu, wote walikuwa na ngozi nyeupe.

Machale yalimcheza mtoto huyo akabaini uhai wake ulikuwa mashakani, hiyo haikuwa ajali ya bahati mbaya bali wazungu hao walikuwa wamedhamiria kuchukua uhai wake.

Akili yake ilicheza haraka akaona njia bora ya kuwakwepa Wazungu hao ilikuwa ni kurudi nyumbani kwao.

Ghafla alibadili uelekeo wa ungo kisha akaongeza kasi chombo kikapepea kwa kasi ya ajabu. Kabla hajafika mbele zaidi alishangaa kuona wingu jeusi tii uelekeo aliokuwa akielekea.

Alipoangalia vyema wingu hilo alibaini halikuwa wingu bali, walikuwa ni popo waliokuwa wakimfuata yeye.

Akaamua kukishusha zaidi chombo hicho ili kuwakwepa popo hao, lilikuwa ni swala la haraka sana pasipo kufikiri mara mbili mbili.

Kwa kuwa hakuwa juu sana alikuwa kimo cha chini zaidi, ungo huo ulijigonga kwenye mkaratusi. Mtoto THE BOMBOM alijogonga kwenye mti huo, akadondoka mpaka chini.

Bahati nzuri alidondokea kwenye bwawa lililochimbwa wakati wa ujenzi wa barabara, alikuwa uchi wa mnyama.

Ghafla maeneo hayo walishuka wale popo, kila walipofika chini waligeuka na kuwa binadamu. Walikuwa ni Waafrika zaidi ya thelathini na wazungu kumi na moja, walikuwa wameungana kuhakikisha wanampoteza Mtoto Nabii THE BOMBOM.

Walishuka eneo hilo na kilizunguka bwawa lote, walikuwa wameshuhudia namna mtoto huyo alivyodondokea bwawani humo.

Mara baada ya kudondokea bwawani humo mtoto huyo alijibadili na kuchukua umbo la chura. Bahati mbaya wale Wazungu na swahiba zao hawakuweza kumbaini mtoto huyo katika umbo la chura.

Mtoto huyo alitoka bwawani akiwa anarukaruka mithili ya chura halisi, wale Wazungu walikuwa wamezunguka bwawa zima wakimtafuta mtoto huyo.

Hata walivyomuona chura huyo akitoka bwawani hawakujishughulisha naye, lengo lao ilikuwa ni kukamilisha kazi iliyowaleta.

Hakika kazi waliyokuwa wametumwa Wazungu hao walikuwa wameitekeleza zaidi ya asilimia sitini, hivyo asilimia arobaini iliyokuwa imesalia ilikuwa mbiyoni kukamilika.

Yule chura alikwenda chini ya mkaratusi uliokuwa karibu na bwawa hilo, mkaratusi uliokuwa umesababisha ajali. wakati huo wale wachawi waliendelea na shughuli zao za kumasaka mtoto huyo bwawani. Mtoto huyo alifanikiwa kuuona ungo wake bado akiwa kwenya umbo la chura, bahati ikawa upande wake kwani ule ungo ulikuwa haujapata hitirafu yeyote.

Kwa kuwa walikuwa hawajambaini aliamua kukaa chini ya mti huo ili awachunguze vyema wale Wazungu.

Bahati ikazidi kumuangukia zaidi, wale wachawi wa kizungu walichukua dawa fulani na kuimwaga kwenye bwawa hilo.

Walisubiria kwa muda wa dakika kadhaa, lakini hakukutokea kitu. Mzungu mmoja alipiga magoti karibu na bwawa kisha akapiga makofi mawili ardhini harafu akasimama.

Dakika tatu mbele walitua wachawi wawili wa kizungu wakiwa na mateka wao Kiafrika, Wazungu hao walishuka eneo hilo wakiwa na usafiri wa ungo.

Walisaidiana na wale Wazungu wengine kumsogeza mateka huyo karibu na bwawa. Mtoto huyo alikodoa macho yake kwa nguvu ili kumbaini mateka huyo, sura ya mateka huyo haikuwa ngeni.

Alikuwa ni jamaa mweusi tii mithili ya lami ya barabara, macho yake yalikuwa makubwa mithili ya komba mzee.

Alikuwa ni pandikizi la jibaba mwenye rangi nyeusi isiyo na vikwatuzi, akiwa chini ya himaya ya Wazungu hao.

Mtoto Nabii THE BOMBOM, alikuwa akifahamu kwa kina jambo lililokuwa likienda kumtokea mateka huyo.

Kadri alivyokuwa akimuangalia mateka huyo, alibaini kuwa alishawahi kumuona maeneo fulani. Hata hivyo hakuwa na uhakika wa eneo alilowahi kumuona mateka huyo, unde si punde aling'amua eneo alilowahi kumuona.

Macho ya mtoto THE BOMBOM yalichanua kwa mshangao, alikuwa ameshakumbuka eneo alilowahi kukutana naye.

Mateka huyo ni miongoni mwa wafanyabiashara wa viungo vya binadamu aliowaona jana kule makaburini.

Mtoto huyo alibaki akijiuliza maswali yasiyo na majibu, maana mateka huyo walimuacha kule makaburini akiwa mzima wa bukheri.

Tena mtoto huyo na kundi lake la wachawi walimuacha mtu huyo akiwa anakatakata viungo vya maiti aliyekuwa kazikwa siku hiyo.

Wakati akiwa kwenye lindi la mawazo wale Wazungu walimchukua mateka wao na kumsogeza zaidi karibu na bwawa.

Alikuwa kafungwa mikono kwa nyuma huku mdomo wake ukiwa umejazwa nguo, hakuwa na uwezo wa kuzungumza zaidi ya kukodoa macho yake makubwa mithili ya mbilimbi.

Mzungu mmoja alitoa kisu kiunoni mwake, kisha akamsogelea yule mateka halafu akakiweka kisu hicho shingoni mwake.

Aliinua macho yake juu kisha akamuomba mungu wake kabula ya kumchinja mateka huyo. Baada ya sekunde chache mzungu huyo alimchinja mateka shingoni mwake, damu zikimiminika mfano wa mwanakondoo.

Maji ya bwawa hilo yaligeuka kuwa damu tupu, hali haikuwa nzuri hata kidogo maeneo hayo. Yule mateka alifanyika sadaka kwa ajili ya upatanisho wa mungu wa Wazungu hao kumpata mtoto Nabii THE BOMBOM.

Mbali ya kumchinja mateka huyo hakuna kilichopatikana, wazungu hao rangi zao zilibadilika na kuwa nyekundu ndi.

Hii ilionesha ni kwa jinsi gani wazungu hao walikuwa wamekasirika sana. Walikuwa na uhakika kuwa mtoto huyo alidondokea maeneo hayo, kwa namna moja au nyingine hakuwa amefanikiwa kutoroka.

Alitakiwa kupatikana kwa njia yeyote, hii ingekamilisha kwa urahisi kazi waliyokuwa wametumwa. Baada ya kutumia muda mrefu kumtafuta bwawani hapo, waliamua kwenda chini ya mti wa mkaratusi kuutafuta ule ungo ili waufanyie kazi.

Mbaya zaidi ungo huo ulikuwa karibu zaidi ya mtoto huyo alipokuwa kajificha, Wazungu watatu walionekana kukaza miguu yao chapu kuelekea mahali ilipokuwa ungo.

Ndugu msomaji, unadhani nini kitampata mtoto huyo baada ya Wazungu hao kuusogelea ungo huo? Tafadhali endelea kufuatilia kisa hiki cha kusisimua sehemu inayofuata.

SHILOGILE GETE

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news