TANZANIA, BORA KUISHANGILIA-25: HAPA SONGWE, KUNA MENGI SANA

NA LWAGA MWAMBANDE

HISTORIA inaonesha kuwa, Mkoa wa Songwe uliundwa kutoka mkoani Mbeya, baada ya Serikali ya Awamu ya Nne chini ya aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete kutangaza kuanza mchakato wa uanzishaji wa mkoa na wilaya Oktoba 18, 2015.

Baada ya hapo mrithi wake Rais Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Jonh Pombe Joseph Magufuli alitangaza kuanzishwa kwa Mkoa wa Songwe kwenye Gazeti la Serikali (GN) namba 461 la Januari 29, 2016.

Ndani ya Mkoa wa Songwe kuna wilaya nne ambazo ni Mbozi, Momba, Ileje na Songwe. Pia kuna halmashauri nne za wilaya za Mbozi, Momba, Ileje, Songwe na Halmashauri ya Mji mmoja wa Tunduma.

Katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, Songwe ipo katika Latitudo 7o na 9o 36' Kusini mwa Ikweta na 32o na 33o 41' Mashariki mwa Greenwich.

Aidha,kwa upande wa Kusini, Songwe unapakana na Malawi na Zambia, mikoa ya Rukwa na Katavi upande wa Magharibi, Tabora upande wa Kaskazini na Mbeya upande wa Mashariki.

Ziwa Rukwa upande wa Magharibi ndilo chanzo kikubwa cha maji katika ukanda huo. Tunduma inaingia Zambia na nchi nyingine za Kusini na Kati mwa Afrika huku Isongole ikitengeneza lango la kuingia Malawi.

Mkoa wa Songwe una eneo la takribani kilomita za mraba 27,598.9.Chini ya bonde la ufa, watu hupitia msimu wa joto kutoka mapema Septemba hadi mwishoni mwa Aprili na msimu wa baridi kutoka Mei hadi mwishoni mwa Agosti.

Joto la juu zaidi hufikia 25o C katika nyanda za chini kuzunguka Ziwa Rukwa, Songwe na Momba na 16o C katika miinuko ya Mbozi, Tunduma na Ileje.

Idadi kubwa ya watu wanajihusisha na kilimo, ufugaji na uvuvi. Wachache wao ni wafanyabiashara na wafugaji kutoka wakiwemo Wasukuma na Wamasai.Mazao yanayolimwa ni mpunga, mahindi, kahawa,ufuta, alizeti, maharage na mtama.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa na mkewe Mary Majaliwa (kulia kwake) wakitazama Kimondo wakati walipotembelea Kituo cha Mambo ya Kale cha Mbozi mkoani Songwe Julai 23, 2017.(Picha na Maktaba).

Miongoni mwa vivutio vya kipekee vya utalii mkoani Songwe ni Kimondo cha Mbozi ambacho kinakadiriwa kuwa na uzito wa tani 12 na ni cha nane kwa ukubwa duniani.

Pia, ni kimondo cha pili Afrika baada ya kimondo cha Hoba chenye tani 60. Kimondo cha Hoba kilichopo nchini Namibia ndicho kikubwa zaidi Afrika na duniani.

Haijulikani ni lini hasa kimondo hicho cha Mbozi kilianguka, ila mtu wa kwanza kukiona katika miaka ya 1930 alijulikana kwa jina la Halele Simbaya, ambaye alikuwa mhunzi.

Halele alipogundua kimondo hicho alitoa taarifa kijijini kwao, ndipo wenyeji wakaanza kuabudu katika shimo ambalo huwa linahifadhi maji ambayo wenyeji hunawa kupata baraka na wakaliita tukio hilo kuwa ni kusafisha nyota.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema, mkoani Songwe mbali na vivutio vya utalii pia kuna fursa mbalimbali za uwekezaji. Endelea;


1. Mbeya meshajizalia,
Mkoa Songwe sikia,
Japo mpya nakwambia,
Unakwenda kileleni.

2.Mahindi watulimia,
Hata maharage pia,
Chakula kimetimia,
Ni kazi kwenda jikoni.

3. Biashara wafanyia,
Nchini hadi Zambia,
Wako bize nakwambia,
Kawaone mpakani.

4.Kimondo likisikia,
Mdude umetulia,
Ni chuma kinavyolia,
Maajabu duniani.

5.Wale waliosikia,
Huko wanakimbilia,
Kwa macho kushuhudia,
Dude kutoka angani.

6.Ileje meisikia?
Mpakani yaishia,
Huko mtindi pitia,
Tafurahika kooni.

7.Chunya twajifagilia,
Dhahabu twajichimbia,
Huko wote wanukia,
Utajiri mifukoni.

8.Na kimataifa pia,
Songwe haujasinzia,
Ndege zatua sawia,
Songwe Uwanja wa shani.

9.Kifika Mbeya tulia,
Ni karibu zungukia,
Uwanja taangalia,
Walojenga hongereni.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news