TANZANIA, BORA KUISHANGILIA-29: ZANZIBAR, SI UTALII TU PIA KILIMO

NA LWAGA MWAMBANDE

NI wazi kuwa, Zanzibar ina fursa muhumu kwa maendeleo ya jamii na ukuaji uchumi, zikiwemo sekta za kilimo cha baharini na utalii.

Aidha,kilimo cha mwani visiwani Zanzibar kimepewa msukumo mkubwa na Serikali, hali ambayo inaongeza motisha na hamasa kwa wakulima wengi kujihusisha nacho.

Ni kutokana na juhudi ambazo zimekuwa zikifanywa na uongozi wa Serikali ya Awamu ya Nane chini ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi ambapo Serikali, imeweka vifaa na fedha maalumu kwa ajili ya wakulima wa zao hilo.

Zanzibar inatajwa kuwa ni nchi ya nne duniani kati ya nchi zinazozalisha mwani mwekundu ikiongozwa na Indonesia, Ufilipino na Malaysia ambapo mwaka 2021 Zanzibar imezalisha takribani tani 12,000.

Kilimo cha mwani ni moja kati ya shughuli za uchumi wa buluu, kabla ya dhana hiyo hadi wakati huu watu wanaoishi pembezoni mwa bahari wamejiajiri na wengi wao ni wanawake.

Mwani hutegemea maji ya bahari kama ukulima wa mpunga unavyotegemea mashamba ya ardhi, wanawake hutumia fursa hiyo kujiajiri baada ya kutambua fursa za uchumi zilizopo baharini.
Wanawake wakiendelea na kilimo cha mwani Zanzibar hivi karibuni. (Picha na BBC).

Aidha, mwani huwa unalimwa na kuvunwa siku 45 hadi 60, kulingana na mabadiliko ya hali ya hewa, Zanzibar huendelezwa shughuli hiyo kwa kiasi kikubwa ambapo maelfu ya wananchi wanalima mwani katika vijiji 86, vijiji 50 Unguja, na vivi 33 huko Pemba.

Mwani hutumika kama chakula na kutengeneza bidhaa mbalimbali ikiwemo sabuni, juisi, mafuta, kashata, vileja, keki, jamu na bidhaa nyengine ambazo zinatumiwa ndani na nje ya nchi. Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza mbali na Mwani pia ndani ya Zanzibar kuna mengi mazuri. Endelea;

1. Karafuu watambia,
Nyingi wanajilimia,
Kipato yawapatia,
Chawafaa maishani.

2. Utalii zungukia,
Kote unakopitia,
Pemba utashuhudia,
Kwapendeza mashambani.

3. Baharini chungulia,
Hoteli imetulia,
Maji yaizungukia,
Ni raha iso kifani.

4. Samaki waangalia,
Vile wanajipitia,
Raha sana nakwambia,
Tadhani uko peponi.

5.Unguja namalizia,
Mikoa mitatu pia,
Huko utazungukia,
Utalii huu ndani.

6. Kati Kusini sikia,
Koani unafikia,
Kaskazini pitia,
Kituo Mkokotoni.

7.Forodhani kufikia,
Mimi nakutamania,
Piza nikijipatia,
Huko Unguja mjini.

8.Uvuvi mtawalia,
Kote wanajifanyia,
Chakula wajipatia,
Na kuuza nje ndani.

9.Hoteli nyingi sikia,
Kiwengwa ushasikia?
Raha wanavyojilia?
Wewe wapitwa kwa nini?

10. Kilimo mwani sikia,
Uchumi kinachangia,
Faidaze kama mia
Mashamba ni baharini.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news