Wajane watoa ombi serikalini, Waziri Dkt.Gwajima asisitiza

NA MWANDISHI WETU
WMJJWM, MBEYA

WAJANE nchini wameiomba Serikali kuwapatia msaada wa kisheria ili kupata haki zao na kusaidiwa huduma ya afya ya akili ili kudhibiti msongo wa mawazo.
Hayo yamebainishwa na Katibu wa Chama Cha Wanawake Wajane Tanzania (CCWWT) Taifa, Sabrina Tenganamba alipokuwa akiwasilisha risala mbele ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Wajane Duniani, jijini Mbeya leo Juni 23, 2023.
Sabrina ameeleza changamoto wanazokumbana nazo wajane kuwa ni pamoja na kusingiziwa kuwauwa waume zao na kunyang'anywa haki zao za mirathi hivyo, wengi kukabiliwa na umaskini mkubwa na kupelekea msongo wa mawazo hata wengine kujiua.
"Lakini pia tunaomba Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) ahakiki kumbukumbu za ndoa kwani changamoto nyingine zinaletwa na wanaume kuwa na ndoa zilizosajiliwa zaidi ya moja hivyo kuleta shida wakati wa mirathi,"amesema Sabrina.
Aidha, wajane wameomba waunganishwe na mifumo ya benki ili wanufaike na fursa za kiuchumi na kufanya uzalishaji.

Akijibu changamoto hizo, Waziri Mhe.Dkt.Gwajima amesema Serikali itaimarisha zaidi uratibu wa masuala ya wajane na kusimamia Sheria ya Msaada wa Kisheria Na. 1 ya mwaka 2017 kuhakikisha wajane wanapata haki zao.
"Taasisi 125 za kutoa huduma za msaada wa kisheria zimetambuliwa na Wasaidizi wa Kisheria 3,721 wamesajiliwa kote nchini ambapo, mwaka 2021/22 kesi 277 za mirathi ya wajane zilitolewa hukumu ya ushindi,"amesema Waziri Dkt.Gwajima.
Katika kuwaelimisha wajane juu ya fursa za kiuchumi, Dkt.Gwajima ameelekeza uandaliwe mkutano wa Chama cha Wajane na Watendaji wote kupitia mtandao wa kidigitali ili kujadili changamoto zote na kuziwekea mkakati mapema Julai, mwaka huu.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Juma Homera amesema, katika kutatua changanoto za wajane, mkoa huo unahakikisha Kamati za MTAKUWWA zinafanya kazi yake ya kupinga ukatili kwa wanawake na watoto.
Naye Naibu Katibu Mkuu, Amon Mpanju ameabinisha kuwa wajane wanakumbana na changamoto nyingi za kijamii, hivyo wizara inasimamia Sera, mikakati, miongozo na sheria kuhakikisha zinatatuliwa ili wanawake Wajane wazifikie na kujikwamua kiuchumi.
"Maadhimisho ya mwaka huu wanawake wajane wamepata nafasi ya mafunzo ya ujasiriamali, mirathi, afya ya akili na msaada wa kisheria,"amesema Mpanju.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news