BoT yatunukiwa cheti kwa kuandaa Mkataba wa Huduma kwa Mteja

NA MWANDISHI WETU

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imetunukiwa cheti kwa kuandaa Mkataba wa Huduma kwa Mteja na kuwa mfano kwa taasisi ambazo bado hazijafanikiwa kukamilisha mkataba huo.

Pia, cheti kimetolewa kwa Chuo cha BoT kilichopo jijini Mwanza ambacho pia kimeandaa Mkataba wake wa Huduma kwa Mteja kutokana na upekee wa shughuli zake.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti, Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene, alikabidhi vyeti hivyo kwa Naibu Gavana wa Benki Kuu, Dkt. Yamungu Kayandabila, pamoja na kwa viongozi wa taasisi nyingine ambazo pia zimeandaa Mkataba wa Huduma kwa Mteja katika hafla iliyofanyika Nyerere Square jijini Dodoma.

Mkataba huo wa Huduma kwa Mteja unaelezea huduma ambazo BoT itatoa na muda wa utekelezaji wa huduma hizo kwa wananchi na wadau wake.

Waziri Simbachawene ameziagiza taasisi zote nchini kuandaa na kuhuisha Mikataba ya Huduma kwa Mteja na kuitumia katika utekelezaji wa majukumu yao ili kutoa huduma bora kwa wananchi.

Akizungumza katika kilele cha wiki ya Utumishi wa Umma Simbachawene amezipongeza taasisi zote zilizokamilisha uandaaji wa Mkataba wa Huduma kwa Mteja kwa kuwa mkataba huo utaongeza chachu katika utendaji wa kazi na kuleta ufanisi na tija katika taasisi na hivyo wananchi kupata huduma bora kama wanavyotarajia.
Aidha, amezitaka taasisi zote nchini kutumia mfumo wa e-mrejesho ambao unaonyesha mwanzo wa mwananchi kupata huduma na namna tatizo lake lilivyoshughulikiwa na kupata mrejesho kwa wakati

Akizungumzia maadili katika utumishi wa umma Waziri Simbachawene amesisitiza kila mtumishi kuvaa kitambulisho chenye jina na cheo chake muda wote awapo katika maeneo ya kazi huku akisema kuwa uzalendo ni kutoa huduma bora kwa wananchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news