Waziri Prof.Mkenda atoa maagizo kwa Taasisi ya Elimu Tanzania

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda ameitaka Taasisi ya Elimu Tanzania kuweka mazingira endelevu ya kutambua walimu wanaomudu vizuri stadi za ufundishaji kwenye shule za umma na Binafsi.
Waziri Mkenda ametoa rai hiyo jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya utoaji Tuzo za Stadi za Ufundishaji kwa Walimu wa Elimu ya Awali na Msingi ambapo amesema Walimu wanahitaji motisha mbalimbali ikiwemo katika kutambua katika kazi wanayofanya 

Amesema ubora wa elimu hapa nchini pamoja na mageuzi ya elimu bila kuwa na walimu wenye hamasa itakuwa ni kazi bure.
“Ningependa kwenye hili la kutambua stadi za ufundishaji TET muweke mazingira endelevu, najua kwa sasa Mradi wa BOOST umewezesha na mmefika katika halmashauri 26 nataka muende kwenye halmashauri zote na Tuzo hizi ziwe endelevu na kazi hii mfanye pamoja na Wizara ili hata baada ya Mradi iweze kuendelea,”amesema Prof. Mkenda.

Prof. Mkenda amewaeleza walimu kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa walimu na kwamba Sera mpya ya elimu itaendeleza mafunzo kazini kwa walimu na itasisitiza fursa za walimu kusoma.
Waziri Mkenda ametumia fursa hiyo kuishukuri Benki ya dunia kwa namna inavyofadhili miradi mbalimbali ya elimu hapa nchini na pia kwa kuwezesha hafla ya utoaji wa Tuzo kwa washindi wa Stadi za Ufundishaji kwa Walimu wa Elimu ya Awali na Msingi kupitia Mradi wa BOOST.

Naye Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia Tanzania, Preeti Arora amesema Ushindani wa ujuzi wa kufundisha ni moja ya njia bora za maendeleo ya kitaaluma ya mwalimu na kwamba inaweza kuwa sehemu na sehemu ya mpango wa MEWAKA kwani Ushindani huwapa walimu fursa ya kuonyesha ujuzi wao na kujifunza kutoka kwa wenzao. 
“Kwa kushiriki katika ushindani, waalimu wanahamasishwa kuendelea kuboresha mbinu zao za kufundisha, kupanua maarifa yao, na kuendeleza mikakati mpya ya kushiriki na kuhamasisha wanafunzi wao kujifunza. Hii inasababisha ukuaji wao wa kitaaluma na huongeza ubora wa jumla wa elimu, hongera walimu wote mlioshinda,” amesema mkurugenzi huyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu Tanzania, Dkt. Aneth komba amesema utoaji wa tuzo hii ni ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa BOOST ambao unafadhiliwa na Benki ya Dunia na unalenga kuboresha uwezo wa walimu katika ufundishaji na ujifunzaji wa wanafunzi kupitia Mafunzo Endelelevu ya Walimu Kazini (MEWAKA).
“Shindano la Stadi za Ufundishaji kwa Walimu wa Elimu ya Awali na Msingi lilianza mwezi wa nne kwa kukusanya na kutathmini video za walimu zenye maudhui ya ufundishaji na ujifunzaji wa kuhesabu pamoja na Somo la Hisabati katika Halmashauri 26 zinazotekeleza Mradi wa BOOST,” amesema Dkt. Komba.
Amesema, pamoja na washindi kupata fedha, cheti na wengine ngao video zao zitarekodiwa upya katika studio za TET na kupakiwa katika mfumo wa ujifunzaji na ufundishaji wa LMS na hivyo kuzidi kuleta chachu ya ufundishaji unaozingatia ujenzi wa umahiri.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news