Buriani mwanamuziki Adolf Mbinga

NA ADELADIUS MAKWEGA 

REMEGIUS Mmavele ni mwanahabari wa Tanzania kwa miaka kadhaa sasa ambaye Mwanakwetu anamfahamu tangu wakiwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Ndanda mwaka 1996-1998 ambapo Mwanakwetu akisajiliwa kwa kidato cha tano /sita wakati Mmavele akiwa Kidato cha Pili/ Tatu na cha Nne. 
Kufahamiana kwa Mwanakwetu na Mmavele kulitokana na mwalimu Magreth Mmavele ambaye alikuwa ni akisomesha masomo ya Mapishi &Ushonaji shuleni hapo, akisimamia idara hiyo iliyokuwa na vifaa bora kuliko shule yoyote Tanzania baada yakupewa misaada kadhaa wa vifaa vya masomo hayo mawili kutoka Shirika la Wabedikitine la Ndanda ikisimamiwa na mama huyu. 

Mwanakwetu hakuwa mwanafunzi anayesoma masomo hayobali akisoma mchepuo wa HKL, Je alijuaje habari za Idara ya Ushonaji &Mapishi?. 

Mwalimu Mmavele alimpenda sana mwanafunzi aliyekuwa akifahamika kama Adeladius Francis Makwega tangu alipofika shuleni hapo kwani kila kulipokuwa na kazi ya upambaji aliagiza aitwe ashiriki zoezi hilo, huku akipewa kazi ya akitazama kama kazi hiyo imefanyika vizuri. Mwanakwetu hafahamu kigezo kilichotumiwa na mwalimu huyo kumpangia kazi hiyo lakini ilikuwa hivyo. Jambo hilo likasababisha hata siku mama Mmavele alipofundisha somo la Mapishi kwa vitendo, Mwanakwetu aliitwa kuchukua vyakula kadhaa kama vile maandazi na mboga , huku wanafunzi wengine hawakupata bahati hiyo, hiyo ikiwa bahati ya mtende kwa Mwanakwetu.
Mwanahabari Mmavele akiwa na Adolf Mbinga wakati wa ugonjwa.

Mambo yalikuwa matamu sana siku za mitihani ya mapishi kwa kidato cha nne, Mwanakwetu aliishi kwa raha mno shuleni hapo. Hapo ndipo Mwanakwetu akamfahamu Remigius Mmavele ambaye alikuwa ni mwanafunzi mrefu kuliko wote mtoto wa mwalimu Mavele. Remigius Mavele wakati huo akiwa na kaka yake aliyekuwa akisoma Chuo cha Ufundi Ndanda aliyekuwa pia mwanachuo mrefu kuliko wote chuoni hapo wakati huo.Hayo ni ya miaka hiyo Je sasa kuna nini? 

Juni 16, 2023 Mwanakwetu alipotembelea ukurasa wa mtandao wa kijamii wa mwanahabari Remigius Mmavele na akakutana maelezo haya, 

“Mungu akupokee na kukujalia pumziko la milele huko ulipotangulia ADOLF MBINGA, tulikuwa pamoja nyakati zote za furaha na mahangaiko, nyakati ya ugonjwa, sote njia yetu ni moja umetangulia ndugu, rafiki yangu Adolf Mbinga, mtaalamu wa kucharaza Solo gitaa uliyepata ujuzi huo Chuo cha Ufundi Ndanda.” 

Mwanakwetu baadaya ya kusoma ujumbe huu akamtafuta mwanahabari Mavele na kuzungumza naye, 

“Adolf Mbinga namfahamu sana, mpaka wakati anaumwa mimi na wenzangu tulifika nyumbani kwake na kumpeleka Hospitali hadi tukaamua arudi nyumbani, tangu amekwenda huko haijafika hata majuma matatu amefariki. Awali nilimtafuta nikafanya nae vipindi vya redio viwili. Anazikwa Kwao Kijiji cha Mpute Juni 17, 2023 saa 4 ya asubuhi lakini mimi sintoshiriki kutokana na majukumu ya kazi.” 

Mwanakwetu alimpa pole Remigius Mmavele kwa msiba wa rafiki yake, kaka yake na nduguye huyo akisema kwa hata kitendo cha kumchukue Adolf na kumpeleka Hospitali ni kitendo cha kiungwana sana huku Mwanakwetu alitamani kufahamu juu ya mambo aliyoongea naye mwanamuzi huyu akiwa hai ni yepi? 

“Adolf Mbinga katika vipindi vyangu vya redio aliungama wazi kuwa alitoka Bendi ya Twanga Pepeta na kumfuta Waziri wa zamani mhe. Mudhihiri Mudhihiri na kumshawisha anunue vifaa vya bendi ya muziki, mhe huyu alifanya hivyo , baadaye Adolf Mbinga aligeuka nyuma na kurudi Twanga Pepeta na hilo likamtia hasara mhe.Mudhhiri. Adolf Aliporudi Twanga Pepeta ndipo akapachikwa jina la MTUHUMIWA na wenzake kwa utani. Hata mimi(Mavele) nilipompigia simu mhe Mudhhiri alikata kusikiliza habari za Adolf Mbinga kwani alisema alimtia hasara kubwa.” 

Mwanakwetu katika suala la kutiana hasara anasema kuwa kila mmoja wetu anayo simulizi ya maisha yenye kupanda milima na mabonde, maana panda shuka panda shuka ndiyo maisha ya binadamu.Mwanakwetu alimuuza mwanahabari Mavele je alimuliza Adolf Mbinga je katika muziki aliwahi kutunga wimbo wowote na je wimbo upi ulikuwa wa kwanza? 

“Alitunga nyimbo nyingi na wimbo wa kwanza ulikuwa ni Neema wa Daimond Sound -wana Kibinda Nkoi miaka 1996 na baadaye zikaja zile nyimbo zake za Twanga pepeta kama Kisa cha Mpemba, Bwana Kijiko na Tabu za Maisha.”
Mwanahabri Mmavele akiwa studio na Adolf Mbinga baada ya kufanya nae kipindi cha redio. 

Mwanakwetu mara alipomaliza mazungumzo na mwanahabari Remigius Mmavele alimtafuta Mwanamuzi Mwinyijuma Muumini- Kocha wa Dunia, hayo yalikuwa majira ya saa 10.20 ya jioni ya Juni 16, 2023 mwanamuziki huyu alikuwa stendi ya Mabasi ya Mikoani ya Mbagala Zakhem akisubiri basi lililokuwa linatoka Dodoma kuelekea Nachingwea apande kuelekea Kijiji cha Mpute-Nachingwea kushiriki maziko ya Adolf Mbinga ya Juni 17, 2023, huku Kocha wa Dunia akisema haya, 

“Nilimfahamu akiwa Daimond Sound tangu mwaka 1996 na walikuwa wakifika Kenya, Mwaka 2000 nilipotoka Nairobi nikamkuta Twanga Pepeta na yeye alikuwa kiongozi wa bendi hiyo na baadaye tukaenda Mchinga Sound pamoja. Akiwa Twanga altunga wimbo wa Kidomo domo ambao tulipokwenda Mchinga tukaurekodi, Twanga Pepeta nilikuwa naimba kopi tu,lakini Mchinga Sound niliimba nyimbo nyingi na yeye kupiga gitaa.” 

Kocha wa Dunia akiwa anazungumza na Mwanakwetu kwa njia ya simu katika eneo lenye makelele sana alisema kuwa wakiwa Mchinga Sound. 

“Katika nyimbo zote za Mchinga Sound magitaa ya solo na rhythm wakati wa kurekodi kazi hizo zilifanywa na Adolf Mmbinga peke yake studio, baada ya kurekodi katika maonesho ya wazi alimuachia Godi kupiga gitaa la rhythm .” 

Mwanakwetu aliyakumbuka mno maneno hayo ya Mwinjuma Muumini, akisema kuwa Adolf Mbinga hakujitapa kwa kuifanya kazi hiyo peke yake wengine wakidhani kuwa Godi alishiriki kurekodi gitaa za nyimbo hizo na kupiga rhytihm. 

Mwanakwetu kwa heshima ya mchango wa mwanamuziki Adolf Mbinga katika muziki wa dansi wa Tanzania kwa karibu miaka 30 ya kazi anatoa pole kwa wanamuziki wote wa muziki wa dansi Tanzania kwa kumpoteza wanamuziki mwenzao, Pole kwa familia ya Adolf Mbinga , Pole kwa Kocha Dunia–Mwijuma Muumini na Pole kwa mwanahabari Remigius Mmavele. 

Buriani Mwanamuziki Adolf Mbinga. 
0717649257

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news