Dkt.Mabula atahadharisha wanaosubiri fidia Ngara

NA MUNIR SHEMWETA
WANMM

WAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Mheshimiwa Dkt.Angeline Mabula amewatahadharisha wananchi wanaosubiri kulipwa fidia kupisha mradi wa uchimbaji madini wa Tembo Nickel wilayani Ngara Mkoa wa Kagera kujiepusha na mikopo umiza.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt.Angeline Mabula (kushoto) na Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Kanali Mathias Kahabi wakipata maelezo ya mradi wa uchimbaji madini ya Nickel wilayani Ngara Mkoa wa Kagera tarehe 23 Julai 2023. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI).

Dkt.Mabula amesema hayo leo Julai 23, 2023 katika Kijiji cha Bugarama wilayani Ngara mara baada ya kutembelea mradi wa uchimbaji madini ya Tembo Nickel kwa lengo la kupata taarifa ya maendeleo ya ulipaji fidia kwa wananchi wanaopitiwa na mradi huo akiwa katika ziara yake ya siku moja mkoani Kagera.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula (wa pili kushoto) na Mkuu wa Wilaya ya Ngara Kanali Mathias Kahabi (wa kwanza kushoto) wakipata maelezo mara baada ya kuwasili katika mgodi wa uchimbaji madini ya Nickel wilayani Ngara mkoa wa Kagera tarehe 23 Julai 2023.

Amesema, anawasikitia wale wananchi wote walioingia katika mikopo umiza kwa kueleza kuwa watalazimika kulipa kiasi kikubwa cha fedha na hivyo kutoona faida ya fidia ya mali zao.

‘’Hela yako yote umeshaikopa unakwenda kulipa pesa nyingi kwa pesa ndogo uliyoichukua mwisho wa siku unarudi katika umasikini bila sababu, niwaombe msikimbilie kukopa pesa unayokwenda kulipa ni asilimia kubwa ya kile ulichochukua,"amesema Dkt.Mabula.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula akizungumza na wananchi wa Bugarama wilayani Ngara Mkoa wa Kagera wakati wa ziara ya siku moja mkoani humo leo Julai 23, 2023. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Kanali Mathias Kahabi.

Amesema, wanaowakopesha wameshajua muda mfupi ujao wananchi hao wanapata pesa, hivyo wanajaribu kuwawahi watoe pesa leo, lakini watakuja kulipa kiasi kikubwa cha fedha kuliko ilivyostahili jambo litakalowafanya kurejea kwenye umasikini.

Amewataka viongozi wa vijiji vyote vinavyopotiwa na mradi huo kutoa elimu ili wananchi wasije wakasikitika na kulia hapo baadaye kwa kuwa mara watakapopokea fedha za fidia basi waliowakopesha watakuja kudai fedha zao.
Wananchi wa Bugarama wilayani Ngara Mkoa wa Kagera wakimsikiliza Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula alipofanya ziara wilayani humo leo.

Aliwataka wananchi ambao hawajakopa kuacha kufanya hivyo kwa kuwa wanahitaji kuwa na maisha endelevu, kuwekeza ambapo alisema iwapo wanahitaji mikopo basi waende benki kwenye riba nafuu.

Awali Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula alipata taarifa ya maendeleo ya ulipaji fidia wananchi wanaopisha mradi katika eneo la mradi.

Akiwa katika eneo hilo, Waziri Dkt.Mabula alielezwa na kiongozi wa mahusiano ya jamii, Bernard Sefu wa Kampuni ya Tembo Nickel kuwa, mgodi huo uko ndani ya kata tatu zenye vijiji vitano vinavyopisha mradi wa uchimbaji madini ya Nickel ambapo jumla ya wananchi 1,339 wanatarajiwa kulipwa fidia huku 349 kati ya hao wakijengewa nyumba kutokana na kuwa na makazi kwenye eneo la mradi huo.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula akizungumza mara baada ya kupata taarifa ya maendeleo ya ulipaji fidia wananchi wanaopisha mradi wa uchimbaji madini ya Nickel wilayani Ngara mkoa wa Kagera tarehe 23 Julai 2023. Kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Ngara Kanali Mathias Khabi.

Sefu amesema kuwa, mgodi huo umechukua hatua mbalimbali kwa kushirikisha viongozi, wataalamu na wananchi wanaopitiwa na mradi huo lengo likiwa kuhakikisha kila mwananchi anayehamishwa kupisha mradi anapata fidia stahiki kwa kufuata sheria za Tanzania na Kanuni za Kimataifa (IFC).

‘’Katika mchakato mzima wa kufanya ukokotovu wa malipo kwa wafidiwa, tuliwaonesha wahusika jedwali kabla ya kupeleka kwa mthamani mkuu wa serikali,’’amesema Sefu.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula (kushoto) akizungumza na Mthamini Mkuu wa Serikali, Evelyne Mugasha (katikati) alipowasili katika mgodi wa uchimbaji madini ya Nickel wilayani Ngara mkoa wa Kagera tarehe 23 Julai 2023.

Kwa upande wake, Waziri Dkt.Mabula mbali na kuipongeza Kampuni ya Tembo Nickel kuandaa utaratibu mzuri wa kulipa fidia wananchi wanaopisha mradi pamoja na kusaidia huduma mbalimbali za jamii. Hata hivyo, aliitaka kampuni hiyo kuhakikisha wale wananchi wanaoenda kujengewa nyumba na kampuni hiyo wanawekewa mpango wa makazi utakaokuwa katika mpangilio wa kimji.

‘’Wale wananchi mtakaowajengea nyumba muangalie namna ya kuwapanga, tunahitaji upangaji wa kimji walau ufanane na mahali pale, mkiweza kuwasaidia mtawafanya wafanane kimji,"amesema Dkt.Mabula.
Mthamini Mkuu wa Serikali, Evelyne Mugasha (kulia) akifuatilia uwasilishwaji taarifa ya ulipaji fidia wananchi wanaopisha mradi wa uchimbaji madini ya Nickel wilayani Ngara mkoa wa Kagera wakati wa ziara ya Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula tarehe 23 Julai 2023.

Kampuni ya Tembo Nickel Corporation Limited inatarajia kuchimba madini ya Nickel katika eneo la Kabanga, wilayani Ngara Mkoa wa Kagera ambapo zaidi ya hekta 4,000 zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.

Januari 19, mwaka 2021 Serikali ya Tanzania na kampuni ya Lifezone Metals Nickel Limited zilisaini mikataba uliowezesha kuanzishwa Kampuni ya Tembo Nickel Corporation Limited ambayo ni ya ubia kati yake na Serikali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news