Karibu tena Urusi Mheshimiwa Kassim Majaliwa

DAR ES SALAAM-Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Shirikisho la Urusi zina mahusiano mema zaidi ya kidiplomasia ambayo yameendelea kuwa na manufaa bora zaidi kwa ustawi wa pande zote mbili.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisalimiana na Rais wa Shirikisho la Urusi, Vladimir Putin baada ya Ufunguzi wa Jukwaa la Kimataifa la Uchumi na kibinadamu uliofanywa na Rais Putin kwenye Kituo cha Mikutano na Maonesho Expo Forum, St. Petersburg nchini humo Julai 27, 2023. Kushoto ni Mkewe Mama Mary Majaliwa. Mheshimiwa Majaliwa alimuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye jukwaa hilo.

Pande hizo zimekuwa zikijikita zaidi katika kuendeleza na kufungua maeneo mapya ya ushirikiano katika sekta mbalimbali kwa maslahi mapana ya mataifa hayo.

Kupitia, Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uliopo jijini Moscow, Urusi umekuwa ukiwajibika kikamilifu kuhakikisha unashughulikia masuala yote ya uhusiano wa kidiplomasia na una jukumu la kukuza uhusiano wa urafiki na ushirikiano kati ya Serikali na watu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Urusi.

Sambamba na mataifa mengine ya jirani ikiwemo Georgia, Belarus, Armenia, Kazakhstan, Kyrgyzstan, Moldova, Tajikistan, Turkmenistan na Uzbekistan.

Ubalozi huo umekuwa unawakilisha maslahi ya Tanzania katika maeneo mbalimbali yakiwemo, biashara, fedha, uwekezaji, utalii, elimu, utalii na utamaduni.

Pia, unawafikia wawekezaji watarajiwa, wafanyabiashara, taasisi za kiserikali na zisizo za kiserikali, pamoja na mambo mengine, katika eneo la ithibati na kuwahimiza kufanya biashara na Tanzania, kutembelea vivutio vya utalii, au kufanya mambo mengine kama hayo kwa lengo la kuimarisha uhusiano na Tanzania.

Julai 27,2023 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amehudhuria Mkutano wa Pili wa Kilele baina ya Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka mataifa ya Afrika na Urusi uliofanyika St.Petersburg, Urusi akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwenye mkutano huo.

Mkutano huo ambao umefunguliwa na Rais wa Shirikisho la Urusi, Vladmir Putin na Rais wa Comoro, Azali Assoumani, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), Putin amesisitiza Serikali yake itaendelea kuliunga mkono Bara la Afrika katika nyanya mbalimbali.
 
Mara ya pili

Mheshimiwa, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa anashiriki mkutano huu kwa mara ya pili ambapo, kwa mara ya kwanza alimwakilisha Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mwaka 2019 huko Sochi nchini Urusi.

Aidha, baada ya mkutano huo, mwaka huo, Mheshimiwa Waziri Mkuu aliutaka Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Urusi kuratibu mipango ya wafanyabiashara wa Urusi wanaokusudia kuja nchini kuwekeza kwa kuwaunganisha na taasisi na wizara husika ili waweze kuwekeza mitaji yao kwa kuzingatia maslahi ya Taifa.

Mheshimiwa Waziri Mkuu alitoa agizo hilo baada ya kugundua uwepo wa wafanyabiashara wengi wa Urusi wanakusudia kuja Tanzania kwa ajili ya kuangalia maeneo ya uwekezaji pamoja na kutafuta wafanyabiashara wa Kitanzania watakaoungana nao katika uwekezaji wanaokusudia kuufanya.

“Tayari miradi imekwishawekwa ya kuwakaribiasha wawekezaji wa Urusi kuja Tanzania kwa ushawishi wa kwangu mwenyewe pamoja na ushawishi wa wafanyabiashara wa Tanzania, hivyo nisingependa wafanyabiashara hao wasumbuliwe au kukatishwa tamaa katika kutimiza nia yao hiyo,” Waziri Mkuu alisisitiza mwaka 2019.

Alisema,mkutano baina ya wakuu wa nchi na serikali kutoka mataifa ya Afrika na Urusi uliomalizika Oktoba 24, 2019 ulilenga kujenga uhusiano mzuri zaidi katika nyanja mbalimbali hususani za kiuchumi.

Pia, akizungumza wakati huo baada kumalizika mkutano huo kwenye Ukumbi wa Olympic Park wa Sochi nchini Urusi, Waziri Mkuu alisema, Urusi iliutumia mkutano huo kueleza bayana maeneo ambayo wako tayari kushirikiana na Afrika katika kuwekeza kwa faida ya pande zote mbili.

Waziri Mkuu aliyataja maeneo hayo kuwa ni pamoja na uuzaji wa zana za kilimo kama vile matrekta, sekta ya mafuta na gesi pamoja na madini, ujenzi wa miundombinu hasa reli, masuala ya elimu hasa utoaji wa nafasi za mafunzo nchini humo. 

Njooni Tanzania

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaalika wawekezaji waliobobea kwenye sekta ya mbolea ili waje kufungua viwanda vya mbolea nchini.

Ametoa mwaliko huo Julai 27, 2023 wakati akizungumza kwenye mjadala uliohusu Uimarishaji wa Soko la Mbolea kama njia ya kuondoa njaa barani Afrika uliofanyika kwenye kituo cha mikutano na maonesho cha Expo Forum, jijini St. Petersburg, Urusi.

Amesema, uamuzi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan wa kuongeza bajeti ya kilimo una nia ya kuifanya Tanzania iwe eneo la uzalishaji la kulisha Afrika Mashariki, SADC na bara zima la Afrika. “Bado tuna changamoto ya upatikanaji wa mbolea kwa sababu ikikosekana inaathiri uzalishaji wa chakula.

“Mbolea kwa sasa ndiyo msingi wa uzalishaji chakula. Uzalishaji wetu unatumia zaidi ya asilimia 80 na kwa maana hiyo tunalazimika kutumia fedha nyingi ili kuagiza mbolea kutoka nje na msisitizo wa sasa ni kuzalisha mbolea yetu.

“Tunatumia fursa hii kutafuta marafiki ambao wako tayari kuja kuwekeza kwenye mbolea. Mahitaji yetu ni zaidi ya tani 800,000 wakati uzalishaji wetu ni tani 200,000. Tumeshapata kiwanda ambacho kinazalisha mbolea na sasa wameshafikisha tani 400,000 na wanalenga kufikia tani 800,000 lakini hatuwezi kuetegemea kiwanda kimoja peke yake,” amesema Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Amesema, Tanzania ina rasilmali ya gesi ambayo inaweza kutumika kutengeneza mbolea ukiacha zile za kawaida za wanyama.

“Tukifanikiwa kuongeza uzalishaji wa mbolea, tutakuwa na nafasi ya kuzalisha chakula zaidi. Jukwaa hili ni nafasi pekee ya kualika wawekezaji waliobobea kwenye maeneo kama haya,” amesisitiza.

Mapema, Waziri Mkuu alishiriki Jukwaa la Kimataifa la Uchumi na Kibinadamu lililofunguliwa na Rais wa Urusi, Vladimir Putin kwenye kituo cha mikutano na maonesho cha Expo Forum, jijini St. Petersburg, Urusi.

Jukwaa hilo ambalo limehudhuriwa na Wakuu wa Nchi na Serikali wa nchi za Umoja wa Afrika wakiwemo wa Uganda, Msumbiji, Zimbabwe, Sudan, limehusisha pia Mawaziri, wakuu wa Mashirika ya Kikanda, Taasisi na Mashirika ya kiserikali kutoka Urusi na Afrika.

Jukwaa hilo linaenda sambamba na maonesho ya kimataifa ya bidhaa na huduma mbalimbali kutoka Urusi na Afrika pamoja na majukwaa ya majadiliano (side meetings) zaidi ya 30 ambayo yanahususu mada mbalimbali zikiwemo za masuala ya vijana, kilimo, afya, elimu, masuala ya kibinadamu.

Baadhi mawaziri na makatibu wakuu na wakuu wa taasisi kutoka Tanzania Bara na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wanashiriki majukwaa hayo ya majadiliano.

Maudhui makuu ya jukwaa hilo linalotarajiwa kutoa fursa kwa Tanzania na mataifa mengine ya Afrika kushirikiana na Urusi kukuza uchumi, kutafuta ushirikiano wa kibiashara na kushughulikia changamoto za kimaendeleo yanahusu Uchumi Mpya wa Dunia (the New Global Economy); Usalama Jumuishi (Integrated Security); Sayansi na Teknolojia (Science and Technology); na Masuala ya Kibinadamu na Kijamii (Humanitarian Issues).

Kesho Waziri Mkuu anatarajiwa kushiriki ufunguzi wa Mkutano wa Pili wa Kilele baina ya Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka mataifa ya Afrika na Urusi, kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news