Wanafunzi Bunda kuwafichua wanaowafanyia ukatili wa kijinsia

NA FRESHA KINASA

WANAFUNZI wanaosoma katika shule za msingi na sekondari katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda mkoani Mara wamehimizwa kutoa taarifa bila kuogopa wanapofanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia bila kujalisha wanaowafanyia vitendo hivyo ni ndugu zao wa karibu ili kuwezesha Serikali kuwachukulia hatua kali za kisheria wahusika wa vitendo hivyo. 
Wametakiwa kutoa taarifa hizo kwa walimu wao,viongozi wa serikali za mitaa,vituo vya polisi, Ofisi za Ustawi wa Jamii na katika Dawati la Ulinzi na Usalama zilizopo katika shule zao kwani pasipo kuripoti itakuwa vigumu kutokomeza vitendo hivyo ambavyo ni kinyume cha sheria za nchi na haki za binadamu. 

Hayo yamebainishwa Julai 27, 2023 na Afisa Ustawi wa Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Bunda,Maria Marco John wakati wa zoezi la utoaji wa elimu ya ukatili wa kijinsia katika shule za msingi Muungano, Busambara na Nakatuba zilizopo katika Halmashauri hiyo. 
Ambapo pia zoezi hilo la utoaji wa elimu limeendana sambamba na uzinduzi wa Mwongozo wa Kitaifa wa Dawati la Ulinzi na Usalama wa mtoto shuleni na nje ya shule katika shule hizo wakishirikiana na Shirika la VIFAFIO linalotekeleza mradi wa 'Funguka Paza Sauti kutokomeza vitendo vya ukatili katika Halmashauri ya Bunda chini ya ufadhili wa Shirika la Foundation for Civil Society. 

Maria amesema kuwa, watoto wengi wamekuwa wakikumbana na kadhia ya kufanyiwa vitendo mbalimbali vya ukatili ikiwemo kulawitiwa, kupigwa isivyotakiwa na kunyima haki zao hivyo wasiwafumbie macho wanaowafanyia vitendo hivyo bila kuogopa. 

"Mila na desturi ni sababu za ukatili wa kijinsia, mfano ukeketaji na ulawiti hizo zinatokana na mila. Sababu nyingine ni uelewa mdogo wa jamii, malezi yasiyofaa na umaskini. Sababu hizi zimekuwa zikichangia aina nne za ukatili ambao ni ukatili wa kingono, Kimwili, kisaikolojia na kiuchumi," amesema Maria. 
Pia, ameishauri Jamii kutowatenga na kuwanyima fursa ya elimu watu wenye ulemavu kwani kufanya hivyo ni kuwafanyia ukatili Jambo ambalo halitakiwi. 

Kwa upande wake Restuta Malima kutoka Ofisi ya Elimu Wilaya ya Bunda amesema kuwa, ukatili una madhara mengi ikiwemo kuchangia kuzalisha ajira za utotoni, magonjwa ya kuambukiza, ulemavu, kuathirika kisaikolojia, kifo na kurudisha nyuma maendeleo ya Jamii na familia pia. 

Naye Robnson Wangaso Mratibu wa mradi wa 'Funguka Paza Sauti kutokomeza ukatili wa Kijinsia kutoka Shirika la VIFAFIO lililopo Musoma mkoani Mara amesema, shirika hilo linatekeleza mradi huo kuhakikisha vitendo vya ukatili wa kijinsia vinatokomezwa na jamii yote inashiriki mapambano hayo kupitia elimu wanayoitoa. 
"Mradi huu ambao awamu ya kwanza uliisha ukiwa na thamani ya shilingi milioni 37 na awamu ya pili FCS wametoa shilingi milioni 22 na mradi huu utaisha mwezi Oktoba mwaka huu nia yetu kupambana na ukatili tunashirikiana na Halmashauri ya Bunda na Musoma ambako mradi huu tunautekeleza kutoa elimu na Kuzindua mwongozo wa kitaifa wa dawati la ulinzi na usalama wa mtoto shuleni na nje ya shule. tumekuwa tukitumia matamasha, mikutano na wadau kutoa elimu ya ukatili."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news