Serikali yatoa maagizo kwa taasisi zinazotekeleza Programu ya AFDP

DAR ES SALAAM-Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika na masuala ya Sera, Bunge na Uratibu, Mhe.Jenista Mhagama amezitaka taasisi zinazotekeleza Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) kufanya kazi kwa malengo na kwa wakati ili kutekeleza mpango kazi ambao umewekwa katika programu hiyo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Mhe.Jenista Mhagama akipewa maelezo ya awali na Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO), Bw.Dennis Simba alipofanya ziara yake ya kikazi.

Kauli hiyo ameitoa Julai 27, 2023 jijini Dar es Salaam alipokuwa katika ziara ya kikazi ya kutembelea Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO).

Amesema,TAFICO ni moja ya taasisi za Serikali iliyopewa majukumu katika programu ya kuendeleza kilimo na uvuvi, yenye lengo kubwa la kuongeza tija na faida katika mazao yatokanayo na kilimo na uvuvi ikiwa ni pamoja na ukuzaji wa mazao yatokanayo na viumbe maji kupitia teknolojia ya kisasa.

Akizitaja wizara na tasisi zinazotekeleza programu hizo chini ya Uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Mheshimiwa Waziri Mhagama amesema ni pamoja na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar kupitia TAFICO na ZAFICO.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Mhe. Jenista Mhagama akikagua eneo la gati katika Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) wakati wa ziara ya kikazi katika shirika hilo jijini Dar es Salaam.

Waziri Mhagama alitaka taasisi hizo kuzingatia ubora, na thamani ya fedha katika mradi mzima. “Natarajia kila senti itakayowekezwa katika mradi huu itaenda kujibu na kuleta matokeo halisi tena yakiwa chanya na yatakayosaidia nchi yetu kusonga mbele na kupata maendeleo endelevu kwa wananchi na Taifa kwa ujumla,"alisisita.

Akizungumza katika ziara hiyo, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Dkt.Jim Yonazi alisema, Serikali imeweka mkazo katika kuhakikisha kwamba nchi inanufaika na rasilimali maji hasa katika eneo la uvuvi, kupitia mradi wa AFDP.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Mhe. Jenista Mhagama akikagua eneo la gati katika Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) wakati wa ziara ya kikazi katika shirika hilo jijini Dar es Salaam.

“Sisi kama watendaji tupo tayari kuweka msisitizo na kuhahakisha kwamba haya yote yanakamilika kwa wakati na kuleta tija kwa Taifa letu,”alisisitiza Dkt.Yonazi.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa shirika hilo, Bw. Dennis Simba alisema kuwa, TAFICO imejipanga na ipo tayari katika kuhakikisha kwamba inafungua njia ya kwenda katika uvuvi wa bahari kuu na mnyororo mzima wa thamani, na kuongeza kuwa miradi 11 iliyopo katika programu hiyo itatekelezwa kwa wakati,kwani Serikali imeonesha nia ya dhati ya kufungua uchumi wa buluu.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Mhe.Jenista Mhagama akizungumza na watendaji (hawapo pichani) wakati wa ziara yake ya kikazi katika Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO).

Awali, Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Bodi ya TAFICO, Dkt.Eliamini Kasembe alisema, Serikali ya Awamu ya Sita imeamua kufufua shirika hilo, kwani lina manufaa makubwa kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.

“Nia hii thabiti inaweza kufikia malengo ya uanzishwaji wa shirika hili ikiwa ni pamoja na kutoa ajira na kuchangia katika kuinua uchumi wa Taifa hili,”alibainisha.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news