Mbaroni kwa kusafirisha mirungi Same-Korogwe

TANGA-Jeshi la Polisi mkoani Tanga limewatia mbaroni watuhumiwa watatu waliokuwa wakisafirisha dawa za kulevya aina ya mirungi mabunda 313.

Dawa hizo zinakadiriwa kuwa na uzito wa kilo 112.5 ambapo walikamatiwa katika barabara ya Same-Korogwe katika eneo la Chekelei lilipo Kata ya Mombo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, SACP Henry Mwaibambe amewataja kuwa ni Samiru Shemweta (39) ambaye ni dereva, Abdallah Mndumi (37) wote wakazi wa Sakina Arusha na Abdulazizi Bakari (34) mkazi wa Chamazi, Dar es salaam.

"Watuhumiwa wamekutwa eneo la Chekelei wakiwa kwenye gari yenye namba T 467 CJS aina ya Toyota Carina wakiwa na bunda 313 za mirungi yenye kilo zipatazo 112.5 na tunawashikilia, taratibu za kuwafikisha mahakamani zinafanyika,"amesema.

DCEA wanasemaje?

Hivi karibuni akiwa katika operesheni tokomeza mirungi wilayani Same mkoani Kilimanjaro,Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA), Aretas Lyimo alifafanua kuwa, operesheni ijayo haitamuacha mtu yeyote wakiwemo viongozi wa eneo husika.

"Yeyote tutakayemkuta ana shamba la mirungi, tunamkamata, na watu wamesema kwamba, wapo viongozi mbalimbali ambao wapo huku, kwa nini na wao wanaona hiyo mirungi hawachukui hatua? Kuanzia sasa hivi tutakapofanya operesheni hatutachagua.

"Tutakamata kuanzia mwenyekiti wa kitongoji na watu wake, tutakamata mwenyekiti wa kijiji na watu wake, tutakamata na mtendaji wa kijiji husika kwa sababu mtendaji wa kijiji ni mwakilishi wa Serikali katika eneo hili, anatakiwa ahakikishe wananchi wake wanaishi katika mazingira mazuri, wananchi wake wanapata huduma, Serikali kuna huduma mbalimbali inazitoa huko wananchi wake wanazipata.

"Lakini, pia na mtendaji husika na yeye ni mwakilishi wa Serikali katika eneo hili, kwa hiyo hao wote na afisa tarafa ambaye ndiye anatakiwa kusimamia watendaji wa vijiji na watendaji wa kata kuhakikisha kwamba wananchi waliopo katika eneo lao, hawafanyi uhalifu,"amefafanua Kamishna Jenerali Aretas Lyimo wa DCEA.

Awali hekari 535 za mashamba ya mirungi zimeteketezwa katika oparesheni maalum ‘Tokomeza Mirungi’, iliyoanzia kutekelezwa ndani ya Vijiji vya Rikweni, Heikondi, Tae na Mahande wilayani Same Mkoa wa Kilimanjaro kwa muda wa siku nane kuanzia Julai 2 hadi 9,2023.

Oparesheni hiyo imefanywa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) ikishirikiana na Vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama likiwemo Jeshi la Polisi Tanzania.

Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo alisema katika oparesheni hiyo jumla ya watuhumiwa saba wamekamatwa huku akisema mirungi ni moja ya dawa za kulevya zilizokatazwa nchini kwani ina athari nyingi kwa binadamu, kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiafya.

“Inasababisha saratani ya koo, utumbo na uraibu, mtindio wa ubongo, kiuchumi inasababisha nchi inakosa mapato kwa sababu wengi wanaolima mirungi kata hii na eneo hili la Same hawaingizii mapato yoyote Serikali.

“Nawashukuru wote ambao tunashirikiana nao katika oparesheni hii, tuwaombe wananchi wote kama alivyoagiza Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, viongozi wote wa Serikali, mkoa, wilaya, kata na vijiji tushirikiane kutokomeza dawa za kulevya.”

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news