Ni Singida Fountain Gate FC au As Vita SC?

SINGIDA-Timu ya Singida Fountain Gate inatarajiwa kuicheza mchezo wa kirafiki na As Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Agosti 2, mwaka huu.

Mtanange huo utapigwa katika Dimba la Liti lililopo mkoani Singida likiwa ni tamasha la kwanza la timu hiyo ambalo limepewa jina la Singida Big Day.

Hilo linakuwa ni tamasha la kwanza tangu klabu hiyo iuzwe na kubadilishwa kuwa,Singida Fountain Gate FC ambapo ina historia ndefu.

Timu hiyo ilianzishwa mwaka 2010 ikiwa ni timu ya wafanyakazi wa Benki ya DTB ikifahamika kwa jina la DTB Football Club kabla ya kubadilishwa jina.

DTB FC baadae ilipata hamasa kubwa baada ya kushiriki mabonanza ya mabenki nchini na kufanya vizuri, hivyo kupelekea uongozi wa DTB kuwekeza kwenye timu na kuipeleka kushiriki michuano ya mashindano hadi kushiriki Ligi Daraja la Kwanza (Championship).

Aidha, baada ya kufanya vizuri kwenye championship na kufanikiwa kupanda daraja kwenda Ligi Kuu mwaka 2022, Benki ya DTB iliamua kutoendelea kumiliki timu ya mpira ili kubaki katika kazi zake za msingi za kibenki.

Uamuzi huo ulitoa fursa kwa wadau kutoka mkoani Singida kuinunua timu hiyo na kuibadilisha jina kutoka DTB FC kwenda Singida Big Stars.

Mwaka 2022/2023,Singida Big Stars ilianza kushiriki Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara na kufanikiwa kufanya vizuri kutokana na mkakati wake wa kusajili wachezaji wa kimataifa wenye ubora wa hali ya juu na wale waliocheza vilabu vikubwa vya Tanzania vikiwemo Simba, Yanga, Azam, Mtibwa, Mbeya City na kadhalika.

Mafanikio ya klabu ya Singida Big Stars yalitokana na ubora wa wachezaji, benchi la ufundi na uongozi madhubuti. Baada ya kumalizika msimu wa 2022/23 kwa mafanikio makubwa,Singida Big Stars ilipata ofa nzuri kutoka kwa mwekezaji Fountain Gate Academy ambaye aliinunua kwa lengo la kuiboresha zaidi na kuiendesha kisasa.

Baada ya kununuliwa, Singida Big Stars ikatengeneza muunganiko na Fountain Gate Academy hatimaye kupata jina lake jipya la Singida Fountain Gate FC.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news