Rais Dkt.Mwinyi awashirikisha Wachina maeneo ya uwekezaji

ZANZIBAR-Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema utalii ni sekta kuu ya uchumi na maendeleo unaoingiza pekee asilimia 30 ya pato la uchumi wa Zanzibar.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akiwa katika mazungumzo na mgeni wake Meneja Mwendeshaji wa Kampuni ya China Railway Construction Investment Group, Bw. Haoping Dong (kulia kwa Rais) akiwa na ujumbe wake,mazungumzo hayo yameyofanyika katika Ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar leo Julai 25,2023.(Picha na Ikulu).

Akizungumza na ujumbe wa watu saba kutoka kampuni ya ujenzi wa reli na uwekezaji ya China, Ikulu jijini Zanzibar, waliofika leo Julai 25,2023 kumtembelea, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi aliwakaribisha wawekezaji hao kuangalia fursa mbalimbali za maendeleo zilizomo nchini.

Dkt.Mwinyi amewaeleza wageni hao sekta tatu muhimu za uchumi wa Zanzibar ikiwemo Utalii, Uvuvi na Kumbi za mikutano, hivyo aliwataka kuangalia namna ya kuwekeza kwenye maeneo hayo ili kutoa ushirikinao kwa ajili ya maendeleo ya Zanzibar na wazanzibari kwa ujumla.

Akiizungumzia Sekta ya Utalii, Rais Dkt.Mwinyi aliwaeleza wawekezaji hao kwamba Zanzibar ni kisiwa cha utalii chenye vivutio vingi vya Fukwe za bahari na Hifadhi ya Kimataifa ya Mji Mkongwe ambacho awali kilipokea watalii zaidi kutoka Italia na wawekezaji wengi walitumia fursa hiyo kuwekeza na baadae watu wa Ulaya Mashariki waliendelea kuingia Zanzibar.

Hivyo, Mheshimiwa Rais aliikaribisha Kampuni ya Ujenzi wa Reli na Uwekezaji kutoka China, kuangalia fursa ya Mji Mkongwe wenye majengo ya historia kwa kufanya uwekezaji wa hoteli za kisasa ili kuwavutia Wachina wengi kuingia Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Aidha, aliwaeleza pia kuangalia namna ya kuwekeza kwenye kumbi za mikutano ya kimataifa kwani Zanzibar ina maeneo mengi ya mapumziko kwa watalii na uwekezaji sambamba na kuwakaribisha kwenye uwekezaji wa visiwa vidogo ambavyo ni vivutio vizuri kwa watalii ili kutoa fursa kwa mataifa mbalimbali duniani kuja kuitembelea Zanzibar.

Dkt.Mwinyi pia aliizungumzia sekta ya uvuvi na kuwaeleza wageni hao kwamba uvuvi ni sekta kiongiozi inayosadifu dhana nzima ya Uchumi wa Buluu kutona na maumbile ya visiwa vya Unguja na Pemba kuzungukwa na Bahari ya Hindi.

Hivyo, aliwaeleza kuangalia zaidi uwekezaji wa uvuvi wa kina kirefu cha maji, kwani Zanzibar ina rasilimali ya samaki wengi watakaosafirishwa hadi mataifa mengine duniani.

Pia, aliwaeleza kuangalia namna ya kufanya kilimo cha samaki hai ambacho mazingira ya Zanzibar yanaruhusu ustawi wa kilimo hicho.

Sambamba na kuangalia uwekezaji kwenye sekta ya miundombinu ikiwemo ujenzi wa viwanja vya ndege vya kisasa, bandari na barabara zenye viwango vya hali ya juu kwa lengo la kuimarisha maendeleo ya uchumi wa Zanzibar.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Meneja mwendeshaji wa kampuni hiyo ya Ujenzi wa Reli na Uwekezaji ya China ambaye pia ni mkuu wa msafara, Hao Ping Dong alimueleza Dkt.Mwinyi, kampuni yao ina miradi mingi ya mandeleo na tayari imewekeza maeneo mengi duniani.

Alieleza sekta ya ujenzi ni sekta kuu inayojishulisha zaidi kwenye kamapuni yao, pia wamejikita kwenye ujenzi wa viwanja vya ndege, hoteli na majengo makubwa.

Bw. Ping alieleza kufurahishwa kwake na uwepo wao Zanzibar yeye na wenzake na kutoa shukrani zake kwa Rais Dkt. Mwinyi kwa kuwapokea Ikulu jijini Zanzibar.

Hata hivyo, alimuahidi Rais Dkt.Mwinyi kujenga ushirikiano mzuri baina ya kampuni yake na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news