Rais Dkt.Samia apongezwa usambazaji umeme vijijini

SIMIYU-Viongozi pamoja na wananchi wa vijiji vya Chugambuli, Iwelimo pamoja na Buhangija wamempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kufikisha umeme katika vijiji vyao hali iliyochochea maendeleo pamoja na kuboresha elimu.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti Julai Mosi, 2023, wakati wa zoezi linaloendelea la kutoa elimu na hamasa kwa wananchi vijijini kuunganisha umeme, linalotekelezwa na timu maalumu kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), mkoani Simiyu, wananchi hao wameahidi kutumia umeme kujiletea maendeleo.

“Kwa kweli tunamshkuru sana Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za ziada kwa ajili ya kuwezesha wananchi zaidi kunufaika na uwepo wa umeme vijijini.

"Kwa sisi hapa tumeona manufaa makubwa ya umeme kijijini kwetu. Mfano awali tulikuwa tunatumia mashine za kusaga unga zinazotumia mafuta, ila kwa sasa kijijini kwetu kuna mashine za umeme na hata bei ya kusaga unga imeshuka na hivyo kupunguza gharama za maisha kwa wanakijiji,” amesema Mwigulu Zimbi Mwenyekiti wa Kijiji cha Buhangija.

Mwenyekiti huyo pia amebainisha kuwa siyo tu kwamba kijiji chao kimenufaika kwa kupata mwanga wa taa za umeme usiku, bali pia vijana wamejiajiri kwa kufungua saluni za kunyolea na kufungua vibanda vya kuonyeshea mpira.

Kwa upande wake, Zabroni Salum ambaye ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Chugambuli amesema kuwa uwepo wa umeme kijijini kwao umesaidia kupunguza vitendo vya kihalifu kama wizi.

“Umeme ulipofika hapa kijijini kwetu umesaidia sana kupunguza vitendo vya kihalifu kama wizi maana muda wote kuna mwanga na mtu akijaribu kufanya wizi ni rahisi kuonekana na kujulikana. Hivyo niwahamasishe wananchi ambao hawajaunga nyumba zao na umeme na miundombinu ya nguzo imefika basi wafanye hivyo ili kufanya kijiji chetu kuendelea kuwa salama zaidi,” amesema Mwenyekiti huyo.

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Iwelimo, Lukala Mayunga amempongeza na kumshukuru Mhe. Rais kwa kuwafikishia umeme akieleza kuwa umewasaidia kuepukana na wanyama wakali kama fisi waliopo kijijini hapo ambapo kwa sasa ni rahisi kuonekana na wananchi kuchukua tahadhari za kujilinda au kuwafukuza.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news