Rais Dkt.Samia aunda wizara, awateua Prof.Mkumbo, Dkt.Mwigulu, Dkt.Kijaji, Mafuru na Mwandumbya

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan amefanya mabadiliko madogo ya miundo ya wizara na kufanya uteuzi wa viongozi wake.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Julai 5, 2023 na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Zuhura Yunus, Mheshimiwa Rais Dkt.Samia amefanya mabadiliko hayo kufuatia kutungwa kwa Sheria ya Mipango ya Taifa ya mwaka 2023 pamoja na uamuzi wa kuhamishia masuala ya uwekezaji Ofisi ya Rais.

Aidha, kwa mujibu wa taarifa hiyo, Mheshimiwa Rais Dkt.Samia ameunda Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji ambapo amemteua Prof.Kitila Alexander Mkumbo kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji. Mheshimiwa Prof.Mkumbo ni Mbunge wa Jimbo la Ubungo mkoani Dar es Saalam.

Pia, Mheshimiwa Rais Dkt.Samia ameunda Wizara ya Fedha ambapo amemteua Mheshimiwa Dkt.Mwigulu Lameck Nchemba kuwa Waziri wa Fedha. Kabla ya uteuzi huu, Mheshimiwa Dkt.Nchemba alikuwa Waziri wa Fedha na Mipango.

Aidha, Mheshimiwa Rais Dkt.Samia ameunda Wizara ya Viwanda na Biashara ambapo amemteua Mheshimiwa Dkt.Ashatu Kachwamba Kijaji kuwa Waziri wa wizara hiyo. Kabla ya uteuzi huu, Mheshimiwa Dkt.Kijaji alikuwa Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara.

Wakati huo huo, Mheshimiwa Rais Dkt.Samia amemteua Bw.Lawrence Nyasebwa Mafuru kuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango ya Taifa.

Kabla ya uteuzi huu, Bw.Mafuru alikuwa Naibu katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango (Usimamizi wa Uchumi).

Vile vile, Mheshimiwa Rais Dkt.Samia amemteua, Bw. Elijah Mwandumbya kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha (Usimamizi wa Uchumi). Kabla ya uteuzi huu kwa mujibu wa taarifa hiyo, Bw.Mwandumbya alikuwa Kamishna, Idara ya Uchambuzi wa Sera, Wizara ya Fedha na Mipango.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news