Waziri Kairuki amshukuru Rais Samia kwa kuwathamini walimu

NA DIRAMAKINI

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mheshimiwa Angellah Kairuki amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake za kuhakikisha wizara na taasisi zinazosimamia utumishi wa walimu zinaendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzipatia fedha.

Sambamba na vitendea kazi na watumishi wenye ujuzi na weledi wa kutosha kupitia ufadhili wa Miradi ya Maendeleo ikiwemo mradi wa BOOST na SEQUIP ili kuboresha Sekta ya Elimu nchini.

Ameyasema hayo Julai 4, 2023 kwenye ufunguzi wa kikao kazi cha mafunzo kuhusu Mfumo wa Taarifa za Watumishi (HCMIS) kwa maafisa wa Tume ya Utumishi wa Walimu katika Ukumbi wa PSSSF jijini Dodoma.

"Pia, naomba nichukue nafasi hii kuwashukuru sana Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, kwa kuandaa mfumo ambao unatoa dirisha kwa Maafisa wa Tume ya Utumishi wa Walimu kuwa sehemu ya watumiaji ili kuwawezesha kuwahudumia walimu kwa ufanisi na kukubali kutoa mafunzo haya."

Waziri Kairuki ametaka walimu waliostahili kupandishwa vyeo, lakini hawakupanda kwa sababu mbalimbali na kukaa kwenye cheo kimoja kwa muda mrefu, taarifa zao zikionesha utumishi wao tangu walipoajiriwa hadi ngazi waliyopo sasa ziwasilishwe kwenye mamlaka husika kama watakavyoelekezwa.

Pia, kuhakikisha madai ya malimbikizo ya mishahara ya walimu wote yanaingizwa kwenye Mfumo wa Watumishi (HCMIS) na orodha iwasilishwe OR-TAMISEMI kama watakavyoelekezwa.

"Kuhakikisha kuwa mnafuatilia madai ya walimu ya malipo ya likizo na uhamisho ili wapate stahiki zao kwa wakati."

Alisema, Tume ya Utumishi wa Walimu ni Mamlaka ya Ajira na Nidhamu kwa Walimu wa Shule za Msingi na Sekondari kwa mujibu wa Sheria ya Tume ya Utumishi wa Walimu Sura 488 na Kanuni zake za Mwaka 2016 pamoja na Taratibu za Uendeshaji za Walimu walio kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa za mwaka 2016.

Waziri Kairuki alisema,pamoja na majukumu mengine Kifungu cha 5(a) cha Sheria hiyo, kimeipa Tume jukumu la msingi la kusimamia na kuendeleza Utumishi wa Walimu.

"Mafunzo haya ni sehemu ya uwezeshaji kwenu ili muendelee kutekeleza majukumu mliyopewa kisheria. Nimeelezwa kuwa, Tume na OR-TAMISEMI kwa nyakati tofauti zimekuwa zikipokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya walimu ambapo, miongoni mwa malalamiko haya yanatokana na baadhi yao kutopandishwa vyeo na kutobadilishwa vyeo kwa wakati na wengine kuchelewa kulipwa mishahara mara baada ya kuanza kazi au kupanda vyeo kutokana na sababu mbalimbali.

"Katika kutafuta namna bora ya kushughulikia na kuyapatia ufumbuzi wa kudumu malalamiko hayo, tarehe 21 Juni, 2023 viongozi wa Ofisi ya Rais TAMISEMI, Ofisi ya Rais UTUMISHI na Tume ya Utumishi wa Walimu walifanya kikao cha pamoja ambacho matokeo yake ni mafunzo haya.

"Nawapongeza viongozi wote kwa kuja na uamuzi huu. Hii ndiyo dhamira njema ya kumsaidia Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamuhuri ya Muungano ya Tanzania katika kutatua kero za Walimu."

Mheshimiwa Waziri Kairuki alifafanua kuwa,yeye mwenyewe amekuwa akipokea malalamiko ya walimu kuhusu madaraja na stahiki zao mbalimbali.

Malalamiko makuu ya walimu yaliyowasilishwa kwake ni pamoja na walimu waliostahili kupandishwa vyeo, lakini hawakupanda kutokana na kukaa kwenye cheo kimoja kwa muda mrefu.

"Walimu waliostahili kupanda, lakini hawakupanda kwa sababu ya kubadilishiwa cheo (recategorization), walimu waliostahili kupandishwa vyeo, lakini wameachwa kwa sababu ya kutofautiana kwa tarehe za kuidhinisha cheo cha awali."

Aidha, alisema wengine ni walimu waliokaa kwenye cheo kimoja kwa muda mrefu na hivyo kuwa nyuma cheo kwenye kundi rika lao,walimu kutolipwa malimbikizo ya mishahara na kutolipwa malipo ya likizo na uhamisho.

"Mhe.Majaliwa Kasimu Majaliwa, Waziri Mkuu amesisitiza juu ya wasimamizi wa walimu kwenda kuonana na watumishi katika maeneo yao ya kazi badala ya wao kuwafuata ofisini jambo ambalo halipendezi.

"Anapenda kuona kuwa walimu wanatumia muda wa kazi kutekeleza majukumu yao kuwahudumia watoto wa Tanzania kwa uadilifu na uzalendo wa hali ya juu ili kuleta tija na kuwa na matokeo chanya katika elimu yetu ambayo itaiwezesha nchi yetu kupiga hatua kimaendeleo.

"Niwaombe wote tushirikiane vyema katika kuwahudumia walimu ili kuleta ufanisi uliokusudiwa katika sekta ya elimu."

Waziri Kairuki alitoa wito kwa taasisi zote zinazoshiriki kutekeleza mafunzo hayo, kuwa na ushirikiano wakati wa utekelezaji ili kuhakikisha hakuna kitakachokwamisha lengo lililo kusudiwa la kuwafanya TSC kuwa sehemu ya watumiaji wa mfumo na kuongeza ufanisi katika kuwahudumia walimu.

"Hivyo, tunatakiwa kuunga mkono jitihada za Rais wetu kwa kuhakikisha kuwa, tunazingatia sheria, kanuni na miongozo iliyowekwa katika usimamizi wa masuala ya utumishi nchini."

Katika hatua nyingine, aliipongeza OR-UTUMISHI, OR-TAMISEMI na TSC kwa kuamua kufanya mkutano wa pamoja Juni 21, 2023 na kuona namna bora ya kufanya ili kutatua kero hizo za walimu.

Alisema, ni matumaini yake kuwa mafunzo hayo yatawawezesha kwenda kutekeleza majukumu na wajibu wao kuondoa kero zote za walimu zinazolalamikiwa,

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news