Sabasaba siku njema, kutukuza Kiswahili

NA LWAGA MWAMBANDE

LEO Julai 7, 2023 Watanzania na Dunia kwa ujumla inaadhimisha Maadhimisho ya Pili ya Lugha ya Kiswahili Duniani.

Maadhimisho haya yanafanyika kwa mara ya pili,kutokana na uamuzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) wa Novemba 2021 kuwa tarehe saba ya kila mwezi Julai kuwe na Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani.

Aidha, maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani mwaka huu (MASIKIDU 2023) ambayo Kitaifa yanaadhimishwa jijini Zanzibar kwa mara ya kwanza yalifanyika mwaka jana.

Ni wazi, Kiswahili ni lugha ya umoja na mawasiliano kwa watu wengi barani Afrika na nje ya Afrika na ndiyo maana shauku ya Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) na Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA) ni kuona Kiswahili kinaendelea kuzungumzwa duniani kote kama zilivyo lugha nyingine.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema, licha ya kuwatakia Watanzania Sabasaba njema pia ameendelea kuhimiza kila mmoja kutukuza Kiswahili. Endelea;

1.Kiswahili tiki pata, jinsi unatamanika,
Kwetu ulianza pita, mashariki ya Afrika,
Wengine wakakupata, Kusini mwa Afrika,
Sabasaba siku njema, kutukuza Kiswahili.

2.Mhuri kutoka nje, kwa lugha ya Afrika,
Sifa ziko nje nje, Kiswahili chatukuka,
Wengi waja wakionje, ladha ya kueleweka,
Sabasaba siku njema, kutukuza Kiswahili.

3.Na Umoja wa Afrika, Addis kukutanika,
Ukaona ni mwafaka, lugha ikatambulika,
Sasa inahutubika, hata pia kutamka,
Sabasaba siku njema, kutukuza Kiswahili.

4.Umoja wa Mataifa, UNESCO kasikika,
Kutenga siku ya sifa, Kiswahili kutukuka,
Sabasaba maarifa, imekuwa ni tukuka,
Sabasaba siku njema, kutukuza Kiswahili.

5.Kiswahili ni umoja, Tanzania chatumika,
Tumeshakuwa wamoja, makabila yatoweka,
Wenye ndoa na waseja, kwa wote kinatumika,
Sabasaba siku njema, kutukuza Kiswahili.

6.Lugha ni maendeleo kwa hamasa chasikika,
Hotuba zenye upeo, ndicho hicho chatumika,
Toka Nyerere na leo, kote kinatawanyika,
Sabasaba siku njema, kutukuza Kiswahili.

7.Kiswahili ni ajira, wananchi changamka,
Kujifunza hicho bora, kote kinahitajika,
Tunga vitabu kinara, dunia vitasomeka,
Sabasaba siku njema, kutukuza Kiswahili.

8.Diaspora sikia, fanya kikatangazika,
Mtaleta Tanzania, pesa mtazozishika,
Huku tutafurahia, uchumi ukijengeka,
Sabasaba siku njema, kutukuza Kiswahili.

9.Bakita zidi amka, misamiati kusuka,
Ifanye kutangazika, lugha izidi inuka,
Jinsi inatawanyika, fursa zaongezeka,
Sabasaba siku njema, kutukuza Kiswahili.

10.Sasa lugha ya dunia, jinsi inaongeleka,
Matangazo ya dunia, kote kote yasikika,
Nchi kubwa kitajia, huko kinaongeleka,
Sabasaba siku njema, kutukuza Kiswahili.

11.Tuipende lugha yetu, yafanya kutambulika,
Tuienzi lugha yetu, wageni wengi tafika,
Rahisi na mila zetu, wengine wakaziteka,
Sabasaba siku njema, kutukuza Kiswahili.

12.Hongera kwa Kiswahili, hebu zidi kutukuka,
Ulimwengu kikabili, jinsi unavyotumika,
Wa karibu na wa mbali, pamoja tuzidi cheka,
Sabasaba siku njema, kutukuza Kiswahili.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602


Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news