Serikali kujenga masoko matano ya mazao Songea

RUVUMA-Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu), Mhe.Jenista Mhagama ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Peramiho mkoani Ruvuma awaomba wananchi kuchangamkia fursa za uchumi zitakazochochewa na ujenzi wa masoko ya mazao yanayotarajiwa kujengwa na Halmashauri ya Wilaya ya Songea.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu), Mhe. Jenista Mhagama ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Peramiho akinunua mahitaji ya nyumbani katika Soko la Kijiji cha Peramiho “A” lilopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea.

Juhudi hizo za Serikali zinalenga kukuza uchumi kwa wananchi na kuongeza wigo wa ukusanyaji wa mapato kwa Serikali.

Wito huo umetolewa Julai 18,2023 katika ziara yake ya kutembelea na kujionea miradi ya maendeleo katika Jimbo la Peramiho lililopo Halmashauri ya Wilaya ya Songea wakati akizungumza na wananchi katika matukio tofauti katika kata mbili za Mbingamwalule na Peramiho.
“Tumepata fedha kwa ajili ya ujenzi wa masoko ya mazao, tutajenga soko kubwa Peramiho, tutajenga Mpitimbi, tutajenga Matimila, tutajenga Mbingamwalule, na tutajenga katika Kijiji cha Muhukuru,”amesisitiza Mhe.Mhagama.

Amefafanua kwamba, ujenzi wa miundo mbinu ya barabara ya lami kuanzia Kata ya Mbingamwalule inayoenda mpaka Kizuka ni ufunguzi wa uchumi kutoka mpaka wa Tanzania na Msumbiji na utasaidia kutoa mazao shambani kwenda kwenye masoko ya mazao.

Waziri Mhagama amesema,Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Songea imepanga kuunganisha kituo cha mabasi kitakachojengwa Kata ya Mbingamwalule ili kusaidia wageni kupata urahisi wa kufika kwenye soko la mazao lilopo kwenye kata hiyo, na hivyo kufungua fursa mbalimbali za uchumi.

Akizungumzia kuhusu mradi wa soko la kisasa kwa ajili ya uchuuzi wa mahitaji madogo madogo ya nyumbani lilojengwa Kijiji cha Peremiho “A” ambao uliotekelezwa na Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) amesema, "nimefurahi kuona wafanyabiashara wanafanya shughuli zao katika eneo zuri na bora la kibiashara."
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Mhe.Menas Komba amesema ujenzi wa soko la mazao katika Kijiji cha Matomondo kata Mbingamwalule halmashauri ilipokea jumla ya shilingi milioni 198 ambayo inatekeleza mradi na ujenzi unaoendelea.

“Tunataka kukamilisha ujenzi wa vyoo ili tuwalete wachuuzi waliopo mtaani kwenye soko, waanze kuzoea kutumia soko jipya la mazao wakati tukimalizia ujenzi kwenye baadhi ya maeneo ya soko,”amesema Mhe.Menas.

Amefafanua kuwa, ujenzi wa masoko hayo utasaidia kupunguza gharama za usafirshaji kutoka shambani mpaka kwenye eneo la soko.

“Tunafanya kazi kimkakati, hakuna mradi utakaoanzishwa usikamilike kila mradi utakaoletewa fedha lazima ukamilike kwa sababu sisi tunasimamia,”amesema Mhe.Menas.

Katika hatua nyingine, Mhe.Menas ametoa ombi kwa Serikali kufikiria kufanya Mji wa Peramiho kupata hadhi ya mji mdogo.

Naye Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Peramiho “A” Sara Athumani amesema, soko la kujipatia mahitaji madogo madogo la Peramiho “A” limegharimu kiasi cha shilingi milioni 185 ambazo zilikuwa zikisimamiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kwa ajili ya kuendeleza soko hilo lenye ukubwa wa vizimba 82.
“Wananchi wametoka katika adha ya kupanga bidhaa kwenye vichanja na kuweka kwenye vizimba na kusaidia kuongeza mapato ya kijiji," amesema Sara.

Kwa upande wake, Bi.Modesta Melinga ambaye ni mfanyabiashara wa soko la Peramiho “A” amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuleta mradi wa soko zuri na kuwaweka sehemu sahihi ya kufanya biashara.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news