Wakulima wa mwani, wajasiriamali ongezeni juhudi-Rais Dkt.Mwinyi

ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi amewata wakulima wa mwani na wajasiriamali kuongeza juhudi zaidi ya ukulima mwani na usarifu wa zao hilo, ili kuongeza tija na faida ya zao hilo.

Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo Julai 23,2023 katika Ukumbi wa Golden Tulip, Uwanja wa Ndege Zanzibar, kwenye kilele cha Maadhimisho ya siku ya Mwani Duniani.

Amesema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeanzisha Kampuni ya Mwani ya Serikali (ZASCO) ili kuleta matumaini ya kumkomboa mkulima wa mwani, kuongeza bei bora kwa wakulima wa zao hilo.

Pia amesema, kilimo cha mwani ni utekelezaji wa mipango ya serikali katika kuleta mageuzi kwenye sekta ya mwani nchini, kupitia uchumi wa buluu, juhudi zaidi zimeongezeka na kueleza kuwa Serikali imevutiwa na jinsi ya wakulima wa zao hilo na wananchi kwa ujumla wanavyoendelea kuitikia wito wa kauli mbiu ya Serikali na kupata mwamko zaidi katika kuzichangamkia fursa za maendeleo na ajira zinazotokana na kilimo na usarifu wa zao la mwani.

“Ninawahakikishieni Serikali yenu ipo pamoja nanyi ili kuhakikisha zao la mwani linaendelea kuwa mkombozi wa kuleta ustawi kwa wakulima na kuchangia ukuaji wa uchumi nchini kama tulivyodhamiria,”ameahidi Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi.

Dkt.Mwinyi ameeleza, mafanikio makubwa yamepatikana kutokana na kilimo cha mwani kupitia Fedha za Mfuko wa Ahuweni ya UVIKO 19, Serikali imewasaidia wakulima wa mwani 5,000 kwa Unguja na Pemba kwa kuwapatia boti maalumu zenye uwezo wa kufika kina kirefu cha maji na kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi na ugonjwa wa ice-ice.

Alisema, licha ya mafanikio hayo ya utekelezaji wa Sera na mikakati ya Wizara ya Uchumi wa bluu na mikakati ya uzalishaji wa mazao ya baharini ukiwemo mwani, Serikali imewekeza fedha nyingi kuwasaidia wakulima na wajasiriamali wa Sekta ya Mwani.

Pia, aliwashukuru wakulima wa mwana na wananchi kwa kuifanya Zanzibar kuwa mzalishaji namba moja wa barani Afrika licha ya changamoto za UVIKO-19, mabadiliko ya tabia nchi, ugonjwa wa ice-ice, athari za kuporomoka kwa bei ya mwani duniani, bado Zanzibar ina mchango mkubwa wa uzalishaji mwani, kwa kushindana na wazalishaji wakubwa duniani kama China, Philippines, Indonesia na wengine.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mwenyekiti wa Kongano la Mwani, Zanzibar (ZaSCI), Dkt.Flower Msuya aliomba ushirikiano kutoka serikalini na taasisi zake ili kuzimaliza changamoto zinazozikabili zao la mwani nchini.

Alieleza, changamoto za tabianchi na bei ndogo ya zao hilo zimelisababisha kuanzishwa kwa Kongano la Mwani miaka nane iliyopita, ili kuleta ubunifu na usarifu wa mwani Zanzibar.

Dkt.Flower alieleza Zanzibar kwa mara ya kwanza ilitambua bidhaa zinazotokana na zao la mwani mwaka 2006 kwa kikundi cha kwanza wanawake na kinamama kutoka Kidoti, Mkoa wa Kaskazini Unguja kuwapa elimu ya kusarifu bidhaa za zao la mwani kwa matumizi mengine ya jamii.

Kwa muijibu wa takwimu za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, uzalishaji mwani umeongezeka kutoka tani 9,663 mwaka 2019/2020, na kufikia tani 12,594 mwaka 2021/2022.

Zao la mwani lina matumizi mengi kwa usatawi wa uchumi wa Zanzibar ikiwemo chakula, vipodozi, dawa, mbolea na chakula cha mifugo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news