Waziri Kairuki akabidhi magari 43 kwa TARURA na makatibu tawala

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI),Mheshimiwa Angellah Kairuki amekabidhi magari 43 kwa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) na kwa makatibu tawala wa mikoa nchini.

Makabidhiano hayo yamefanyika Julai 5, 2023 huku akisema ni jambo la faraja kukabidhi magari kwa watendaji wa TARURA katika ngazi ya makao makuu,mikoa na makatibu tawala wasaidizi wanaoshughulika na miuondombinu katika ngazi za mikoa.

"Sote tutambue kwamba, tumekutana hapa leo kwa ajili ya hafla hii muhimu ya kukabidhi magari 43, ambapo magari 30 ni kwa ajili ya matumizi ya Ofisi za Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) (makao makuu na mikoa),

"Na magari 13 ni kwa ajili ya ofisi za wakuu wa mikoa kwa ajili ya usimamizi wa kazi za miundombinu. Lengo kuu kukabidhi magari haya kwa TARURA na mikoa ni kuwawezesha kuboresha utendaji kazi, hususan katika utekelezaji wa majukumu ya usimamizi wa ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya barabara."

Waziri Kairuki amesema, Serikali ya Awamu ya Sita katika kuendelea kuhakikisha kuwa inatoa huduma bora kwa wananchi, imeendelea kuwezesha taasisi za umma, hususan Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini, kwa kuwapatia fedha kwa ajili ya ununuzi wa magari ili kuimarisha utendaji kazi na usimamizi wa miradi.

Amesema, hadi sasa wakala imefanya manunuzi ya magari 270, ambapo magari hayo yamekuwa yakiwasili kwa vipindi tofauti, na kukabidhiwa kwa wahusika.

"Aidha, tukumbuke kuwa hivi karibuni TARURA ilikabidhiwa magari mengine 54 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Dkt.Philip Isdory Mpango.

"Hivyo, katika kuendelea kupokea magari hayo, leo nitakabidhi magari mengine 43, na hivyo kufanya magari yaliyokabidhiwa kuwa 241, tangu wakala ulipoanza ununuzi wa magari Julai 2017 hadi Juni 2023."

Amesema,lengo la ununuzi wa magari hayo ni kuendelea kuimarisha usimamizi wa shughuli za Serikali katika Sekta ya Miundombinu kwa kutoa huduma bora kwa wananchi.

"Tutambue pia kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imedhamiria kuwezesha wananchi kuwa kitovu cha maendeleo na kuimarisha ubia baina ya wananchi na Serikali.

"Katika ngazi ya msingi kwa kuimarisha miundombinu ya barabara ikiwa ndio kiungo kati ya Serikali kupitia Ofisi za Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) na wananchi katika utoaji wa huduma.

"Hivyo,magari haya yatasaidia kurahisisha huduma ya usafiri kwa watendaji wa TARURA na makatibu tawala wasaidizi sehemu ya miundombinu katika kusimamia, kuratibu na kufuatilia shughuli ujenzi katika mikoa.

"Lengo ni kuhakikisha kuwa utendaji kazi unaimarishwa kwa kuwa na vyombo vya usafiri vya uhakika, vitendea kazi, ofisi na watumishi makini wanaotekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma."

Kutokana na majukumu yaliyopo,Waziri Kairuki amesema,magari hayo yatagawiwa kwenye Ofisi za TARURA na Ofisi za Sekretatieti za Mikoa zenye changamoto na uhitaji zaidi wa magari kwa sasa, na zenye maeneo makubwa ya kusimamia.

Sekretarieti za mikoa zitakazopata magari awamu hii, Mheshimiwa Kairuki amesema ni Mtwara, Ruvuma, Mbeya, Songwe, Rukwa, Katavi, Kigoma, Kagera, Mara, Lindi, Dodoma, Tabora na Tanga.

"Ieleweke kwamba kwa kuwa magari haya yanatolewa kwa awamu Ofisi za TARURA na Sekretarieti za mikoa ambazo hazijapata magari leo, zitapatiwa mara tu magari hayo yatakapopokelewa na GPSA.

"Aidha,magari haya yatumike kwa kuzingatia miongozo na taratibu za Serikali, ili yalete tija katika kuboresha huduma kwa wananchi ikiwemo kuongeza ushiriki wa wananchi katika shughuli za kijamii na kiuchumi, kutokana na kuwa na miundombinu bora, na sio kutumika katika matumizi binafsi kinyume na taratibu."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news