Fahamu kuhusu Vimbwette vya aina nne Chuo Kikuu Huria cha Tanzania

NA DKT.MOHAMED OMARY MAGUO

Usuli

Vimbwette ni msamiati unatumika sana katika muktadha wa elimu ya juu nchini Tanzania. Vimbwette ni viti na meza ambavyo aghalabu vimetengenezwa kwa zege na nondo.

Meza huwa katikati na viti au benchi la kukalia huwa pembezoni. Wanafunzi hukaa katika vimbwette kwa ajili ya kujisomea, kufanya mijadala kuhusu masomo na pia wapo ambao huzungumza mambo mbalimbali kuhusiana na maisha kwa jumla.

Etimolojia au chimbuko la jina "vimbwette" ni kutoka katika jina la mwasisi au mtoa wazo la kujengwa kwa viti na meza tulivyovieleza ambaye ni Profesa Tolly Mbwette wakati huo akiwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Baadae alikuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania. Kwa kuwa yeye ndiye mtoa wazo basi na jina lake likachukuliwa na kufanya viti na meza hizo kuitwa Vimbwette.

Leo hii vimbwette vinapatikana katika vyuo mbalimbali vikiwa vimejengwa au kutengenezwa kwa zege na nondo, mbao au chuma.\


Kiini cha Mada

Kimsingi, maendeleo ya Sayansi na Teknolojia yamekiwezesha Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kuwa na aina anuai za Vimbwete zinazotumiwa na wanafunzi. Aina hizo ni kama zifuatazo:


ZOOM Kimbwete

Hiki ni Kimbwete ambacho wanachuo huunganishwa kwa mtandao wa ZOOM kila mmoja akiwa katika eneo tofauti na wenzake.

Wanachuo huandaa kiunganishi (ZOOM Link) na kupeana miongoni mwao na kufanya mijadala ya kimasomo kama vile wanafunzi wa vyuo vya bweni wanavyotumia Vimbwete vya zege vilivyowekwa chini ya vivuli vya miti kwenye mazingira ya vyuo.

Faida kubwa ya Kimbwete cha ZOOM ni kwamba wanafunzi hukutana kila mmoja akiwa huko huko alipo.

Wanachuo wa ndani ya nchi wanaopatikana katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar wanaosoma kozi fulani wanaweza kukutana na kufanya mijadala wakiwa huko huko wakiendelea na kazi zao.

Vilevile wanafunzi waliopo nje ya nchi pia hupata fursa ya kuingia katika ZOOM Kimbwete na kushirikiana na wanafunzi wa ndani ya nchi.

Kwa kutumia ZOOM wanafunzi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania wanapata uwanja mpana wa kujifunza kutoka mazingira mbalimbali-waliopo nje ya nchi watachangia mjadala na kutoa mifano kutoka katika mazingira ya nchi zao huko walipo.

Watanzania wakichukuwa mifano hiyo pamoja na hali halisi hapa nyumbani wakiunganisha wanapata maarifa ya kutosha kabisa.


What'sApp Kimbwete ni aina ya pili ya Kimbwette kinachotumiwa na wanachuo wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.

Kupitia mtandao huu wanafunzi huunda kundi sogozi kulingana na masomo au kozi zao. Katika makundi hayo, wanafunzi hufanya mijadala kama katika Kimbwette cha muasisi Prof. Mbwette.

Tofauti ni kwamba katika Kimbwete hiki wanafunzi hawakutani ana kwa ana bali kila mmoja huwa kazini, nyumbani, kwenye biashara, kilimo, ufugaji nakadhalika na kukutana na wenzake kupitia What's App. Mtandao huu huruhusu kuchati kwa maandishi na pia kufanya mijadala kwa njia ya VIDEO CALL.


Telegram Kimbwette, hiki hakina tofauti kubwa na What's App Kimbwette bali Telegram huchukuwa washiriki wengi zaidi.

Kupitia Kimbwette hiki, wanafunzi hufanya mijadala yao kwa kuchati na pia kujirekodi na kutuma sauti ili wengine wasikie na wao kujibu.

Kimbwette hiki kinaruhusu kutuma picha na mafaili yenye MB na GB kubwa zaidi ambayo katika What's App hayawezi kuingia.

Hivyo wanafunzi hupata uwanja mpana zaidi wa kutuma zana za ujifunzaji na kujipatia maarifa ya kutosha katika masomo yao.


Kimbwete cha ana kwa ana, hiki ni kile cha siku zote hata Chuo Kikuu Huria cha Tanzania pia kipo katika vituo vya mikoa na hata makao makuu.

Wapo wanafunzi ambao hupenda kufika chuoni kwa ajili ya kujisomea na kufanya mijadala baada ya kutoka kazini.

Hawa hukutana ana kwa ana. Wapo pia, ambao wao kila siku kuanzia asubuhi hukaa kwenye Vimbwette na kufanya mijadala ya masomo yao na hata kupata usaidizi kutoka kwa walimu pale wanapokwama kupata majibu au katika kuelewa swali.

Kimbwette hiki cha ana kwa ana pia huweza kufanyika sambamba na ZOOM na WHAT'S App. Mwanafunzi ambaye kwa sababu flani ameshindwa kukutana na wenzake ana kwa ana basi huunganishwa kupitia ZOOM au What's App. Hii humwezesha kufuatilia na kushiriki katika mjadala vizuri kabisa.


Hitimisho

Aina nne za Vimbwette vya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania vimeelezwa vema katika kiini cha mada. Vimbwete hivyo ZOOM Kimbwete, What's App Kimbwette,

Telegram Kimbwete na Ana kwa Ana Kimbwette. Wanachuo wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania wanatumia mitandao hii kufanya mijadala na kupata maarifa na uzoefu kutoka kwa wanachuo wenzao wanaoishi katika mazingira mbalimbali.

Mifumo hii inawawezesha kusoma na kufanya mijadala wakiwa katika shughuli zao bila kuziacha. Ukijiunga na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania utapata fursa ya kuifahamu mifumo hii na kuitumia na bila shaka utaipenda sana.

Karibuni sana

MWANDISHI
Dkt. Mohamed Omary Maguo
Mhadhiri Mwandamizi Mkurugenzi wa Mawasiliano na Masoko
Chuo Kikuu Huria cha Tanzania

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news