Global Fund yaipa kongole Tanzania

GENEVA-Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu amekutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Rasilimali Fedha wa Global Fund, Bi.Ada Faye katika kikao kilichofanyika kwenye ofisi za Makao Makuu ya Mfuko huo zilizopo Geneva, Uswisi.

Lengo la mazungumzo hayo ni kutoa taarifa ya utekelezaji wa miradi inayofadhiliwa na Global Fund pamoja na mwenendo wa viashiria vya UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria nchini.

Waziri Ummy amemjulisha Bi. Faye kuwa Tanzania inatarajia kuzindua Programu Jumuishi ya Wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii inayotarajiwa kuharakisha utokomezaji wa magonjwa ya UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria nchini.

Kwa upande wake Bi.Faye ameipongeza Tanzania kwa kupunguza maambukizi mapya na vifo vitokanavyo na UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria na pia kwa kufikia malengo ya viashiria vya magonjwa hayo kwa wakati.

Sambamba na hilo, Bi.Faye amesema Global Fund inatarajia kuwa Tanzania itatumia vyema msaada wa kiasi cha shilingi trilioni 1.5 kipindi cha Mwaka 2024 hadi 2026 katika utekelezaji wa vipaumbele vya kimkakati na kutatua changamoto dhidi ya mapambano ya UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria.

Mazungumzo hayo yamezitaka nchi zinazopokea misaada kutoka Global Fund kuhakikisha fedha zinawafikia wananchi na kutumika kwa kuzingatia ufanisi wenye tija huku Bi. Faye akiahidi kuwa Mfuko huo uko tayari kushirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa Program Jumuishi ya watoa huduma wa Afya ngazi ya jamii.

Waziri Ummy amemhakikishia Bi.Faye kuwa, Tanzania itaendelea kushirikiana na jumuiya za kimataifa na wadau wote ili kufikia lengo la afya kwa wote.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news