Huyu achukuliwe hatua -Ndejembi

NA JAMES MWANAMYOTO
OR-TAMISEMI

NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe.Deogratius Ndejembi amemuelekeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Bw. Shadrack Mhagama kumchukulia hatua za kinidhamu Mhandisi wa Ujenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Bw. Daniel Kileo.
 
Mheshimiwa Ndejembi ametoa maagizo hayo baada ya kubaini kuwa, Mhandisi huyo  ameshindwa kusimamia kikamilifu utekelezaji wa miradi ya elimu ikiwemo ujenzi wa madarasa ya mradi wa BOOST kinyume na maelekezo ya Serikali yaliyotolewa na Ofisi ya Rais-TAMISEMI.

Mhe. Ndejembi ametoa maelekezo hayo, mara baada ya kutoridhishwa na ujenzi wa madarasa akiwa katika ziara yake ya kikazi ya kukagua Ujenzi wa Miundombinu ya Elimu katika Halmashauri ya Wilaya ya Moshi inayojengwa na Serikali kupitia mradi wa BOOST na SEQUIP.

Mhe. Ndejembi amesema, haiwezekani Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atafute fedha za kujenga miundombinu ya elimu halafu zisitumike vizuri kwa sababu ya Mhandisi wa Wilaya kushindwa kutafsiri ramani wakati yeye ndiye mtalaam na mwenye jukumu hilo.

“Mkurugenzi mchukulie hatua za kinidhamu Mhandisi wa Ujenzi na mkaimishe mwingine, kwani huyu ameshindwa kusimamia ujenzi wa madarasa na Ofisi ya Rais TAMISEMI itakuletea Mhandisi mwingine atakayesimamia miradi ya ujenzi ya miundombinu ya elimu,”Mhe.Ndejembi amesisitiza.

Baada ya ukaguzi wa Miradi ya Elimu katika Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Mhe. Ndejembi amebaini kuwa, miradi mingi katika Halmashauri hiyo haijakamilika wakati katika Wilaya nyingine ikiwemo Manispaa ya Moshi imeshakamilika na changamoto kubwa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi ikiwa ni kuwa na Mhandisi ambaye ameonekana kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

Aidha, Mhe. Ndejembi amesema amepewa taarifa kuwa katika shule ya Sekondari Ashira bweni moja halijajengwa licha ya kuwa fedha zilitolewa na Serikali na Mhandishi huyo kushindwa kusimamia ujenzi huo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Moshi Mhe. Kisare Makori amemshukuru Mhe. Ndejembi kwa kufanya ziara ya kukagua ujenzi wa miundombinu ya elimu na kuhimiza uwajibikaji katika Wilaya yake ili miradi yote ikamilike kwa wakati na kuwanufaisha wananchi kama ilivyokusudiwa na Serikali.

Sanjari na hilo, Mhe. Makori amemuomba Mhe. Ndejembe kumfikishia salamu za shukrani Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia fedha nyingi wilaya yake kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta ya elimu, afya na miundombinu ya barabara.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news