JKCI wamlilia Prof.Mahalu

DAR ES SALAAM-Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wamepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Prof. William Mahalu aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi hiyo na mmoja wa madaktari bingwa wa moyo wa kwanza hapa nchini.
Waziri wa Afya Mhe.Ummy Mwalimu akimkabidhi begi lenye vitendea kazi aliyekuwa Mwenyekiti wa bodi ya wadhamini ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. William Mahalu mara baada ya kuizindua bodi hiyo Agosti mwaka jana jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu akiwa jijini Arusha Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo, Dkt. Peter Kisenge alisema, Prof. Mahalu alikuwa amelazwa JKCI kwa ajili ya matibabu na alifariki usiku wa tarehe 20/08/2023.

Dkt. Kisenge alisema Prof. Mahalu ni miongoni mwa madaktari bingwa wa kwanza watatu wa moyo nchini ambao jitihada zao ziliwezesha kuanzishwa kwa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na kupatikana kwa matibabu ya kibingwa ya moyo nchini Tanzania.

“Kifo cha Prof.Mahalu ni pigo kubwa kwa Taasisi yetu licha ya kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya JKCI pia alikuwa daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu na mshauri mzuri katika kutekeleza majukumu yetu hii ni kutokana na uzoefu wake wa muda mrefu aliokuwa nao,”.

“Tumempoteza mwasisi wa upasuaji wa moyo hapa nchini, ni pigo kubwa kwetu sisi wataalamu wa magonjwa ya moyo kwani kupitia Prof. Mahalu wataalamu wengi wa afya walivutiwa kujiendeleza na kuwa madaktari bingwa wa upasuaji wa moyo hapa nchini,"alisema Dkt. Kisenge.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ambaye pia ni daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu Prof. Wiliam Mahalu akimsikiliza Katibu wa Bodi hiyo ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Dkt. Peter Kisenge wakati wa kikao cha kwanza cha Bodi hiyo kilichofanyika mwishoni mwa mwaka jana jijini Dar es Salaam.

Kwa upande wake daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Evarist Nyawawa alisema alimfahamu Prof.William Mahalu kuwa ni mmoja wa madaktari wa kwanza kabisa katika kusomea fani ya upasuaji wa moyo hapa nchini.

Daktari ambaye ni mzalendo kwani alipohitimu mafunzo yake ya upasuaji nchini Uingereza alirudi Tanzania na kutaka kuanzisha upasuaji wa moyo lakini kulingana na vipaumbele vya serikali kwa kipindi hicho hakuweza kufanya upasuaji huo na kwenda nchini Zimbabwe.

Dkt. Nyawawa alisema mara baada ya serikali kutia mkazo wa kutaka kuanzisha upasuaji wa moyo ikawachagua wataalamu 26 na kuwapeleka nchini India kujifunza upasuaji wa moyo wa fani mbalimbali na mara baada ya kurudi Prof. Mahalu kwa uzalendo wake alirejea nchini ili kujumuika nao na kuanza kufanya upasuaji wa moyo katika chumba cha upasuaji cha Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI).

“Prof. Mhalu ndiye aliyetuwezesha sisi kuanza upasuaji wa moyo hapa nchini kwasababu ukitoka kwenye mafunzo mara nyingi unahitaji mtu ambaye atakusimamia ili uweze kufanya upasuaji wa moyo,” alisema Dkt. Nyawawa.

“Baada ya kurudi hapa nchini Prof. Mahalu alikwenda Hospitali ya Rufaa Bugando na akiwa kule sehemu kubwa ya muda wake aliutumia kuja kujumuika na sisi kufanya upasuaji wa moyo, mbali na hapo alitufundisha na kutafuta wataalmu wengi ambao mpaka leo wapo hapa kwenye Taasisi ya Moyo wakihudumia wananchi,” alisema Dkt. Nyawawa.

“Prof. Mahalu alikuwa ni mzalendo,mshauri na mwenye maono makubwa na ndio maana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alimchagua kuwa mwenyekiti wa Bodi tangu Taasisi inaanzishwa, kutokana na maono yake katika fani hii ya upasuaji wa moyo kwa sasa Taifa linajivunia kuwa na Taasisi ya Moyo na kwa kiwango kikubwa karibu aina zote za upasuaji zinafanyika hapa nchini,” alisema Dkt.Nyawawa.

Licha ya kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mahalu pia alikuwa Mkuu wa Idara ya upasuaji wa moyo na mishipa ya damu wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afya na Sayansi Shirikishi Bugando (CUHAS).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news