Kamati ya Bunge yaipa kongole TANTRADE

DAR ES SALAAM-Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo imeipongeza Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania TANTRADE kwa kuboresha mazingira ya biashara hususani Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) 2023.
Vilevile Kamati hiyo imeiagiza TANTRADE kupitia Sheria na kuwa na mikakati mahususi ikiwemo ya uboreshaji wa miundombinu katika maonesho ya sabasaba na utafutaji wa masoko kwa bidhaa za Tanzania inayoendana na wakati na mabadiliko ya Teknolojia.

Hayo yamesemwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Mariam Ditopile (Mb.) Agosti 15, 2023 wakati ikipokea Taarifa ya Hali Halisi ya Utendaji wa Majukumu ya TANTRADE katika ukumbi wa Bunge jijini Dodoma.
Aidha, wajumbe hao walipata fursa ya kutoa maoni mbalimbali kuhusu uendelezaji wa biashara hususan mauzo ya nje, utafutaji wa masoko, biashara mtandao na mapendekezo ya kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika ukuzaji wa biashara. 
Naye Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe(Mb.) akijumuisha maoni na mapendekezo hayo ameihakikishia Kamati hiyo kuwa maelekezo na mapendekezo yote yaliyotolewa na Kamati hiyo yatatekelezwa ili kuendelea kuweka mazingira mazuri ya biashara, kukuza biashara na mauzo ya ndani na nje na hatimaye kukuza uchumi wa nchi.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara aliieleza Kamati hiyo kuwa Wizara imeanza kupitia na kurekebisha Sera na Sheria mbalimbali ikiwemo Sheria inayoaimamia TANTRADE ili ziendane na wakati na mabadiliko ya teknolojia.
Awali Mkurugenzi Mkuu wa TANTRADE, Bi Latifa Mohamed akiwasilisha taarifa ya Taasisi yake kwa Kamati hiyo, amesema jukumu kuu la TANTRADE ni kukuza na kuendeleza biashara ya ndani na nje ya nchi ili kuimarisha biashara yenye tija katika maendeleo ya kiuchumi nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news